SEHEMU YA *1-----------5*
Katika maisha yangu, sikuwahi kuwaza kuua hata nzi kutokana na huruma niliyokuwa nayo. Watu wengi walipenda kuniita mlokole japo historia yangu yote niliishi maisha ya kutokuwa na dini nikiamini Mungu wa Wakristo ndiye Mungu wa Waislamu kutokana na mafundisho ya dini zote niliyoyafuatilia.
Utashangaa kwa nini niliishi bila kuwa na dini ikiwa wazazi wangu wana dini, tena dini tofauti, baba Muislam na mama Mkristo. Katika maisha yao hakuna aliyekubali kumfuata mwenzake na kukubaliana kila mmoja aishi katika imani yake. Hivyo nikawa mtoto wa wazazi wa dini mbili. Pamoja na wazazi wangu kuishi kila mmoja na dini yake, waliishi katika upendo wa hali ya juu kwa kila mmoja kuheshimu imani ya mwenzake.
Nilipopata ufahamu nilijikuta nipo njia panda kwa vile sikutaka kumuudhi mmoja wa wazazi wangu kwa kumpendelea mmoja. Halafu kitu cha ajabu nilikuwa mtoto mmoja kama roho, hivyo niliamua kusimama katikati ya wazazi wangu kwa kutochagua dini yoyote. Lakini nilikuwa nafahamu kipi mwanadamu anatakiwa kukifanya ili asimuudhi Mungu.
Katika maisha yangu yote niliamini tofauti ya dini mbili ni ndogo sana lakini anayetakiwa kuabudiwa ni Mungu mmoja. Tangu hapo niliishi nikiwa sina dini na kuishi kama mpagani, tofauti yangu nilikuwa najua Mungu ni mmoja na ndiye anayetakiwa kuabudiwa, lakini sikwenda msikitini wala kanisani na malumbano ya dini hizi mbili mimi yalikuwa hayanihusu.
Wazazi wangu nao walikubaliana na mimi baada ya ushawishi wa kila mmoja kugonga mwamba. Huu ulikuwa muhtasali wa maisha yangu ya awali ya kunifanya nisiwe na dini kwa ajili ya mapenzi ya wazazi wangu. Kutokana na malezi mazuri ya wazazi wangu niliweza kuishi sehemu yoyote na mtu wa aina yeyote, siku zote heshima na ucheshi ndivyo vilifanya watu wanipende.
Kama nilivyosema awali, nilikuwa mtu wa huruma na heshima kwa wakubwa na wadogo, lakini mateso ya mapenzi yalinifanya nigeuke na kuwa na roho mbaya kuliko shetani. Kuna maelezo niliwahi kusikia wakati nakua kwamba kuna matendo mengine shetani alikimbia akimuona mwanadamu anatenda.
Baada ya kuteswa sana na mapenzi ilifikia hatua kutoa roho ya mtu kwangu ilikuwa kitu cha kawaida hata kwa kosa dogo la kuombana msamaha kwa kuamini hakuna kiumbe kibaya duniani kama mwanadamu ambaye hatakiwi kupewa nafasi kwa vile kama ukimchekea basi atakuumiza.
Mkasa wangu unaanzia pale nilipotimiza miaka 21 ambapo nilitoka kwa wazazi wangu na kusafiri nje ya mkoa kwenda kufanya kazi baada ya rafiki yangu kupata kazi ya ujenzi hivyo hakutaka kuondoka peke yake, akanichukua na mimi huku wazazi wangu wakiniasa niishi na watu kwa heshima na taadhima. Nami niliwaahidi wazazi wangu kuwa nitaishi kama walivyonilea.
Nilitengana na wazazi wangu kwa mara ya kwanza toka nitoke tumboni kwa mama yangu. Nilifika mkoani na kufikia kwa ndugu wa rafiki yangu. Kwa vile tulifika Jumamosi jioni sana, tulilala na kesho yake tulipumzika na kupata nafasi ya kupelekwa kwenye sehemu ya kazi.
Ulikuwa mradi mkubwa sana ambao tuliambiwa utachukua miaka mitano kuisha, siku ile tulipumzika na kesho yake tulikwenda kuanza kazi. Siku ya pili tuliamka asubuhi na mapema na kwenda eneo la ofisi ambapo ndipo mnapangiwa kazi. Kulikuwa na tofauti kubwa kwani vijana wengi tuliowakuta nje ya geti walikuwa wakisubiri kuitwa, lakini sisi tulikuwa na mwenyeji, mjomba wa rafiki yangu ambaye ndiyo alikuwa msimamizi mkuu wa mradi ule ambao ulikuwa chini ya Waitaliano.
Basi huo ndiyo ukawa mwanzo wa kuanza maisha ya kujitegemea, tulianza kwa kulipwa kwa kutwa kama wenzetu kwa wiki mbili, baada ya hapo tulichaguliwa vijana kama ishirini tuliopewa mkataba na kulipwa kwa mwezi na posho yetu kuongezeka tofauti na wenzetu waliokuwa wakilipwa kwa kutwa.
Maisha yalikwenda vizuri huku mimi na mwenzangu tukihama kwa ndugu zake na kupanga chumba kimoja na kukaa wawili. Wazazi wangu nao walikula jasho langu kwani kila mwezi niliwatumia robo ya mshahara wangu, wakazidi kuniombea kwa Mungu ili niendelee kupata zaidi.
Siku zilikatika huku nami nikipevuka kiakili na mawazo kufikia hatua ya kuhitaji mwenza. Nyumba tuliyokuwa tumepanga kulikuwa na binti mmojaambaye mwenyezi Mungu alimjalia umbile dogo lakini mzuri wa sura. Binti yule alitokea kunipenda sana kiasi cha kumueleza mama yake angependa aolewe na mimi.
Njia moja ya kuonesha ananipenda, aliniomba kazi zote za kike azifanye yeye kama kunipikia chakula cha jioni baada ya kazi, usafi wa nguo na chumba lakini sikumpa nafasi ile kwa kuhofia wazazi wake. Pamoja na mimi kumpenda sana bado sikumkubalia kutokana na kuwaheshimu sana wazazi wake ambao siku zote walinilea kama mtoto wao.
Siku moja majira ya usiku baada ya kutoka kazini, mama mwenye nyumba ambaye ni mama mzazi wa yule binti aliniita kwa kumtumia yule binti. Nami niliitikia wito ule, baada ya kuingia sebuleni nilikaribishwa kwenye kochi lililokuwa karibu na alipokaa mama mwenye nyumba.
“Kazala,” mama aliita kwa sauti ya chini.
“Naam mama,” niliitikia kwa unyenyekevu mkubwa.
“Nimekuita mwanangu nikueleze jambo moja la muhimu sana.”
“Sawa mama.”
“Kwanza wewe dini gani?”
“Sina dini,” nilimjibu kwa mkato.
“Mwongo, hebu niambie ukweli wewe ni dini gani?”
“Kweli mama sina dini.”
“Sasa kama ukipata mwanamke mwenye dini utafanya nini?”
“Sitafanya chochote, nitaiheshimu dini yake, lakini mi nitabakia sina dini.”
“Kwa nini?”
Sikumficha, nilimuelezea maisha ya wazazi wangu na kitu gani kilichonifanya nisiwe na dini.
“Lakini hata kiserikali mtu anapotimiza miaka kumi na nane ana haki ya kuamua chochote bila kuingiliwa, hivyo ulikuwa na nafasi ya kuchagua dini yoyote ya baba au ya mama.”
“Ni kweli, lakini bado kwa mimi sikutakiwa kufanya hivyo.”
“Kwa nini?”
“Nimesimama kati ya baba na mama yangu, wote nawapenda na sitaki kumuudhi mmoja kati yao.”
“Sasa mwanangu kuna kitu nimekuitia, mdogo wako Suzana anakupenda sana tena sana kapitiliza kukupenda. Siku zote amekuwa akikuonesha kwa vitendo lakini inaonekana kama humuelewi. Mpaka kuja kunieleza mimi mama yake basi ujue yamemfika shingoni. Kutokana na tabia yako ambayo imekuwa tofauti na wavulana wengi nimeamini unafaa kuwa mkwe wangu.
MKE WANGU ALISABABISHA NIKAWA MCHAWI
SEHEMU YA 2
“Nakuomba uwe mkwe wangu, muoe Suzy kwa kweli ni mwanamke mzuri ambaye utajivunia katika maisha yako. Najua utashtuka mama kumpigia debe mwanaye lakini kwa hili sikuwa na jinsi.”
“Nimekusikia mzazi wangu naomba unipe muda ili nami niwasiliane na wazazi wangu.”
“Kuwasiliana na wazazi wako si vibaya, lakini kwanza ni wewe kukubaliana na mwenzako.”
“Mimi nimekubali.”
“Nashukuru kwa majibu yako mazuri, basi nakuruhusu, uwasiliane na wazazi wako, usihofu gharama nitakusimamia mpaka mwisho wa harusi yenu.”
“Nashukuru mzazi wangu.”
Baada ya kutoka kwa mama mwenye nyumba nilirudi chumbani kujipumzisha, haikupita muda mlango uligongwa, alikuwa Suzy.
“Karibu,” nilimkaribisha bila kunyanyuka kitandani.
Alisukuma mlango na kuingia ndani akiwa na sinia lililofunikwa kawa.
“Karibu chakula Kazala.”
Sikutaka kubisha lakini nilitaka tule pamoja, Suzy hakukataa, tukala pamoja. Tangu siku ile Suzy akawa na uhuru wa kuja kwangu lakini sikuwa na tamaa ya mwili kwa kujiapia mpaka nimuoe kabisa. Mipango ilienda vizuri na Suzy akawa mke wangu, ndoa ilifungwa kwa mkuu wa wilaya kila mtu akiwa na imani yake.
Namshukuru Mungu maisha yalikuwa mazuri kwa mke wangu kuonesha mapenzi ya kweli nami pia nilimpenda kwa dhati.
Miezi sita baada ya kuoana tulihama nyumbani kwa wakwe zangu na kwenda kukaa kwenye nyumba nyingine ya familia yao iliyokuwepo umbali kidogo toka kwetu, wakati huo mke wangu alikuwa na ujauzito wa miezi minne.
Nyumba tuliyohamia ilikuwa na wapangaji wawili na sisi tulikuwa sehemu ya mbele ya nyumba ile ya kifamilia. Kazi nayo iliendelea vizuri, kila siku nikawa naondoka asubuhi na kurudi usiku. Maisha yalisonga mbele, miezi tisa ilipotimia mke wangu alijifungua mtoto wa kike.
Mtoto wetu alikua vizuri mpaka alipofikisha mwaka mmoja na miezi saba. Hata hivyo nilipatwa na mshtuko baada ya kuona siku zinazidi kusonga mbele lakini mtoto hatembei zaidi ya kuishia kujiburuza kwa matako. Katika maisha yangu, pamoja na kutokuwa na dini, bado sikuuamini uchawi hata kidogo japo niliusikia kuwa upo.
Hali ya mwanangu ya kutotembea ilinishtua sana. Katika kuulizia kwa watu waliomuona mtoto wangu, walisema mtoto wangu inawezekana amebemendwa. Kauli ile ilinishtua sana baada ya kuelezwa maana ya kubemendwa kuwa ni mtu kutoka nje ya ndoa wakati mtoto akiwa bado mdogo.
Kwa upande wangu sikuwa na shaka kwa vile sikuwa na mpenzi mwingine zaidi ya mke wangu mama Zawadi. Pia kwa upande wa mke wangu, hata kwa mtutu nisingekubali kuwa anatoka nje ya ndoa kwani nilimuamini sana.
Nikawa njia panda kuelewa hali iliyomkuta mwanangu inasababishwa na nini. Niliamini kama watu wanasema hali ile inatokana na mtu kutoka nje ya ndoa basi walikuwa wamekosea. Nilijipa moyo kuwa mwanangu hajabemendwa bali tatizo lake linafanana na hilo.
Siku moja ya Jumapili niliyokuwa nyumbani, nilitoka na mwanangu ambaye nilimpenda sana pamoja na kuchelewa kutembea. Nikiwa natoka dukani nilikutana na mama mmoja wa makamo na kusalimiana naye, nilipishana naye lakini sikupiga hatua mbili aliniita.
“Baba Zawadi.”
“Naam mama,” niliitika huku nikigeuka kumsikiliza.
“Samahani mwanangu.”
“Bila samahani mama.”
“Basi naomba tusogee pembeni tuzungumze.”
“Hakuna tatizo mama yangu.”
Nilisogea pembeni kidogo ya barabara na kusimama kwenye uchochoro wa kutokea mtaa wa pili.
“Naam mama,” nilianzisha mazungumzo.
“Mwanangu nimekuita ili tuzungumze kitu kimoja, nina imani hukijui kinachofanyika nyuma kwa vile unatoka asubuhi na kurudi usiku.”
“Ni kweli mama.”
“Unamuonaje mjukuu wangu Zawadi?”
“Kwa kweli mama hata mimi nashindwa kuelewa.”
“Unashindwa kuelewa nini ikiwa mwanao mnamtesa bila kosa.”
“Mama tunamtesa kivipi?”
“Unaona hii miguu ya mwanao ipo sawa?” aliniuliza huku akiishika miguu ya mwanangu iliyokuwa haina nguvu.
“Haipo sawa, kwa kweli nachanganyikiwa hata sijui sababu ni nini japo watu wananiambia kitu ambacho naamini si kweli.”
“Kitu gani hicho?”
“Achana nacho hakina umuhimu,” sikutaka kumwambia habari za kubemendwa ambazo niliona ni za kizushi.
“Kitu gani?”
“Utayaweza maneno ya watu mama, kila kukicha hawakosi ya kusema.”
“Maneno gani?” yule mama alikazania swali lake.
“Achana nayo hayana umuhimu.”
“Inawezekana uliyoambiwa ndiyo nitakayokueleza leo.”
“Nina imani si hayo.”
“Haya, tuachane na hayo, unajua matatizo ya mtoto kuchelewa kutembea inatokana na nini?”
“Kwa kweli sijui.”
“Yapo mambo mengi, moja kuchezewa na walimwengu na lingine kubemendwa.”
“Kwa hiyo tatizo la mwanangu linatokana na nini?”
“Mkeo atamuua mtoto huyu, kwa nini anakuwa na moyo wa kikatili kiasi hiki? Kama hawezi kumlea basi mpelekeni kwa bibi yake kuliko kumtesa bila sababu.”
“Mama sijakuelewa, mke wangu amemfanya nini mtoto?”
“Anambemenda.”
“Eti?”
“Anambemenda na mwisho wake atamuua.”
“Mmh! Una maana gani?”
“Mkeo si muaminifu, watu wote mtaani wanajua, ukitoka na yeye nyuma anatoka, anarudi jioni wakati wewe umekaribia kurudi.”
“Sasa mama kutoka kwa mke wangu kunaingiliana vipi na mwanangu kuchelewa kutembea?”
“Baba jasho la janaba ni baya kwa mtoto hasa ikiwa mliokutana si wazazi wa mtoto, mmoja wenu akikosa uaminifu na akamshika na uchafu wake lazima mtoto atadhurika.”
“Sasa mama mke wangu mbona ni muaminifu?” kauli ile ilinishtua.
“Baba acha kusema hivyo, sisi ndiyo tunaojua, isingekuwa huyu mtoto wala nisingenyanyua mdomo wangu, ningekuacha ili siku moja ujionee mwenyewe uchafu wa mkeo.”
“Kwa hiyo chanzo cha matatizo ya mtoto ni mke wangu?” nilijikuta nikikosa amani moyoni.
“Baba usiandikie mate, kwa vile mkeo hata aibu hana, siku moja rudi nyumbani mchana utajionea mwenyewe. Kabla ya kufanya lolote fanyia kazi haya niliyokueleza. Ukipata majibu ndiyo utajua mkeo ni muaminifu au siyo muaminifu na kupata kiini cha matatizo ya mkeo.
“Ila nakuomba kabla ya yote mtoto wako mpeleke kwa bibi yake kisha fanya uchunguzi wako.”
“Asante mama kwa maelezo yako.”
“Ila nakuomba ukienda kwako usioneshe mabadiliko yoyote, kuanzia Jumatatu siku yoyote rudi nyumbani ghafla mchana utaniambia niliyokueleza ni kweli na maendeleo ya mwanao utayaona kwa muda mfupi akiwa mbali na mama yake.”
“Asante mama.”
Niliagana na yule mama ambaye alikuwa mtu wa heshima na nilimheshimu sana pale mtaani. Nikiwa narudi nyumbani, njia nzima nilikuwa na mawazo mazito juu ya maneno niliyoelezwa na sababu ya matatizo yanayomfanya mwanangu ashindwe kutembea.
MKE WANGU ALISABABISHA NIKAWA MCHAWI
SEHEMU YA 3
Kwingine ambacho sikutaka kukikubali mara moja ni kuhusu kutoka kwa mke wangu nje ya ndoa. Kwa kweli sikuamini mke wangu kama angeweza kutoka nje ya ndoa hasa kutokana na ukimya pia kuonesha mapenzi mazito kwangu. Nilijifikiria kama ni kweli mke wangu ndiye chanzo cha matatizo ya mtoto ina maana hajui au anafanya kwa makusudi? Nilipofika nyumbani nilijitahidi kuficha mabadiliko. Nilipofika mke wangu alinichangamkia huku akimchukua mtoto ambaye siku zote alimuonesha mapenzi mazito.
Siku hiyo nilikuwa nyumbani kimwili lakini kiakili nilikuwa mbali sana kuwaza yote niliyoelezwa na wote walioguswa na hali ya mwanangu kuchelewa kutembea na watu kumtania kwa kumuita fundi majiko. Japo mwanangu alikuwa hatembei lakini maneno yote aliyamalizia alipokaa kama fundi majiko.
Kila nilipomuangalia mke wangu sikummaliza, nilivyomuamini na maneno yale niliyoyasikia, nilichanganyikiwa kabisa. Upande mwingine nilidhani hizo ni njama za kuivunja ndoa yangu. Mke wangu alikuwa mpole, hakuwa muongeaji kabisa, muda wote alikuwa mkimya mpaka nianze mimi kumsemesha.
Niliificha siri ile moyoni mwangu japo akili na moyo vilipingana, kimoja kilikubali na kingine kilikataa. Nilipanga kurudi mchana siku ya Jumatatu ambayo ilikuwa siku ya pili tangu siku ile. Siku ya pili nilipofika kazini, nilisingizia naumwa, kwa vile sikuwahi kuomba ruhusa nilikubaliwa na kurudi nyumbani majira ya saa sita kasoro mchana.
Nilipofika nyumbani nilikuta mlango umefungwa, nilipopiga simu ya mke wangu haikuwa hewani. Nilizunguka upande wa pili ambapo nilimkuta mtoto wangu Zawadi akichezea matope, hakuwa na muangalizi. Nilibisha hodi chumba cha jirani, alitoka na kushtuka.
“Ha! Shemeji leo umerudi mchana?” alisema huku akimtoa Zawadi kwenye matope akionesha kwa kipindi kile cha kuwa peke yake amekula matope mengi kutokana na mdomo kujaa matope.
“Sijisikii vizuri,” nilimjibu kwa sauti ya chini huku roho ikiniuma kwa malezi mabaya ya mwanangu. Hali ile ilianza kunipa picha ya maneno niliyoelezwa, jirani yangu mama Sonono aliingia kazi ya kumsafisha Zawadi matope, akaingia ndani kwake na kutoka na ufunguo, akanipa huku akisema:
“Shemu naomba unitolee na nguo za Zawadi.”
“Hakuna tatizo.”
Niliingia ndani huku nikijiuliza mke wangu atakuwa amekwenda wapi? Pia niliwaza kama nisingekuja mwanangu angekula matope na kuwa mchafu mpaka saa ngapi? Baada ya kumtolea nguo nilimuuliza:
“Mama Zawadi kaenda wapi?”
“Amesema ameitwa na mama yake.”
“Kila siku huwa anaitwa na mama yake?” nilimshtukiza kwa swali ambalo nilijua hakulitegemea.
“Siku nyingine huwa sijui.”
“Kwa hiyo akiondoka wewe ndiyo mlezi wake siyo?”
“Kwani vipi shemu?”
“Nakuuliza wewe ndiye mlezi wake, hebu angalia nimemkuta mtoto anakula tope, kwa siku zote anazoondoka kazi yako kumlisha mwanangu tope?” Nilimuuliza kwa hasira.
“Ha..ha..pana shemu.”
“Niambie ukweli mke wangu amekwenda wapi maana nimetoka kwao.”
“Si..si..jui akiondoka huniachia mtoto.”
“Hurudi saa ngapi?”
“Jioni kabla hujarudi.”
“Asante.”
Nilimchukua mwanangu na kumpeleka kwa mama mzazi wa mke wangu, nikamuuliza kama mke wangu amekwenda kule. Majibu yalikuwa hajakwenda, nilimuomba nimuache mtoto. Alikubali, kitu cha ajabu hakuniuliza swali lolote zaidi ya kumchukua mtoto. Nilirudi nyumbani kumsubiri mke wangu aniambie alikuwa wapi.
Majira ya saa kumi na mbili na nusu mke wangu alirudishwa na gari, kwa vile nilielezwa muda wa kurudi nilikaa nje na ufunguo nilimpa mama Sonono na kumwambia akija amwambie mtoto kachukuliwa na mama yake mzazi. Alipofika aliteremka na kukimbilia kwa mama Sonono kuulizia funguo.
Baada ya muda nilimuona akitoka barabarani akiwa kama anatafuta kitu na kupiga simu yake, baada ya muda gari lililomleta lilirudi. Kabla hajaingia kwenye gari nilijitokeza na kumwita.
“Mke wangu.”
Alishtuka kuniona mpaka simu ikamponyoka na kuanguka chini huku akisema kwa sauti kubwa:
“Ha! Mume wangu!”
“Vipi mpenzi ingia twende nina safari nyingine,” sauti toka kwenye gari ilimhimiza aingie kwenye gari.
“John nenda tu, mume wangu.”
“Mumeo kafanya nini tena mpenzi?”
“John ondoka mume wangu huyu hapa.”
“He!” Sauti ilitoka kwenye gari na gari kuondoka kwa kasi bila kufunga mlango mmoja. Sikutaka kutaharuki, nilimuuliza:
“Unatoka wapi?”
“Kwa mama.”
“Yule nani?”
“Bwana wa shoga yangu alinipa lifti.”
“Mmh! Sawa.”
“Vipi mbona mapema?”
“Kawaida tu kwani kuna ubaya?”
“Hakuna, samahani mume wangu, nilikwenda kwa mama na kupishana naye huku nyuma alikuja na kumchukua Zawadi, nilikuwa naomba nimfuate.”
“Sawa, hakuna tatizo, utanikuta.”
Alisogea mbele na kukodi teksi iliyompeleka kwao, niliingia ndani nikiwa nimefura kwa hasira nikiwa siamini nilichokiona. Nikaanza kuamini yote niliyoelezwa juu ya uchafu wa mke wangu ni kweli. Nilimsubiri kwa hamu kubwa arudi anieleze sababu ya kujifanya kondoo kwenye ngozi ya chui.
Kitu cha ajabu mezani kulikuwa kumeandaliwa kila kitu kuonesha kuwa kumbe mke wangu kabla ya kuondoka hufanya kila kitu kwa ajili ya chakula cha jioni ili akirudi hata kama amechelewa chakula kiwe tayari mezani. Siku zote niliporudi niliamini mke wangu hakutoka kwa vile chakula kilikuwa tayari.
Nilikwenda hadi chumbani na kujilaza kitandani, miguu ikiwa chini bila kuvua viatu, mikono niliiweka kichwani macho nikitazama juu. Sikutaka kuamini nilichokisikia kwa watu ambacho sasa nilikishuhudia mwenyewe kwa macho yangu. Nilipata mtikisiko mkubwa wa moyo kwa mara ya kwanza tangu niwe na akili timamu. Japo nilishawahi kuona na kusikia usaliti ndani ya ndoa za watu, kwangu ilikuwa ndiyo mara ya kwanza.
Nikiwa katikati ya mawazo, mke wangu alirudi akiwa na mtoto na kuja kukaa pembeni huku akijichekesha. Nilijiuliza mama amemwambia nini kutokana na kuwa katika hali ya kawaida tu.
“Vipi mume wangu?”
“Poa.”
“Mbona kama haupo sawa?”
“Nipo sawa,” nilimjibu kwa sauti ya chini.
“Hapana mume wangu lazima utakuwa na tatizo.”
“Nipo sawa.”
“Nakuja,” mke wangu alisema huku akinyanyuka na kwenda nje akimuacha mtoto pembeni.
“Baba,” mwanangu Zawadi aliniita.
“Mama,” nilipenda kumwita mama jina la mama yangu mzazi.
“Pipi api?”
“Nitakwenda kukununulia.”
“Tende dukani baba kanunue pipi,” mwanangu alisema huku akijivuta kwangu na kunishika mkono nimpeleke dukani.
Nilimuangalia mwanangu na kujikuta natokwa na machozi ya uchungu, alizidi kunilazimisha ninyanyuke. Nilinyanyuka kitandani na kumbeba mpaka dukani ambako nilimnunulia pipi na biskuti. Wakati napita kurudi ndani nilimsikia mke wangu akizungumza na mama Sonono. Kwa walivyokuwa wakizungumza niliamini kabisa alijua nimo chumbani.
“Dada umeniangushia jumba bovu,” nilisikia sauti ya mama Sonono ikilalamika.
“Jumba bovu kivipi, kwani anajua nilikwenda wapi?”
“Kurudi mumeo kuna sababu, hata maswali yake yalionesha anajua mengi juu yako, hata mtoto kwa mama yako kampeleka yeye.”
“Weee usiniambie!” sauti ya mke wangu ilionesha kushtuka.
“Kweli kabisa ila alinikataza nisikwambie.”
“Jamani kwa nini umenigeuka?”
“Sikuwa na jinsi, nilihofia kupigwa na mumeo kwa jinsi alivyokuwa angeweza kumtafuna mtu.”
“Akupige kwani wewe ndiye uliyetoka nje ya ndoa, wa kunipiga ni mimi, kwanza jeuri hiyo aitoe wapi?” mke wangu alizungumza sauti ya kujiamini.
Maneno yale yalionesha kabisa mke wangu kufanya vile kulikuwa na kitu anachokitegemea.
MKE WANGU ALISABABISHA NIKAWA MCHAWI
SEHEMU YA 4
“Dada ukitoka tena uondoke na mwanao sitaki ugomvi na mumeo na kuona labda mimi ndiye ninayekufanyia mipango.”
“Mi mtoto mdogo, nitaondoka naye kwani kazi anafanya yeye? Nitamuweka kwenye kochi namaliza haja zangu, hilo shoga lisikupe shaka, basi baadaye.”
Kwa vile ilikuwa giza alitupita na kuingia ndani, nami niliingia ndani na kukutana naye mlangoni, aliponiona aliniuliza:
“Vipi unatoka wapi?”
“Dukani.”
“Eti, umerudi saa ngapi?”
“Kwani vipi?”
“Nasikia umerudi mapema?”
“Tatizo nini?”
“Sasa umerudi mapema ili iweje?”
“Sina ruhusa ya kurudi nyumbani mapema?”
“Siyo hivyo.”
“Sasa tatizo nini?”
“Ujaji wako umeonekana umekuja kwa sababu.”
“Ndiyo umekuja na sababu.”
“Sababu gani?”
Nilijikuta nikipata nafasi ya kufungua yaliyo moyoni.
“Niambie ulikwenda wapi?”
“Kutembea.”
“Kwa ruhusa ya nani?”
“Nilisahau kukuaga naomba unisamehe kwa hilo.”
“Aliyekurudisha ni nani?”
“Ni rafiki wa shoga yangu.”
“Naomba uniambie ukweli la sivyo leo nitakufanyia kitu kibaya,” nilimtisha.
“Unataka kunifanyia kitu gani?” alishtuka.
“Usiponieleza ukweli nitakufanyia kitu kibaya ambacho hutakisahau maishani mwako.”
“Unataka ukweli gani mume wangu?” mke wangu aliingia woga.
“Ninaoujua kila siku, nitokapo nawe unatoka huwa unakwenda wapi?”
“Nani kakwambia?”
“Ishu si kujua aliyeniambia bali kunieleza ninapotoka nawe huwa unatoka kwenda wapi?”
“Waongo hao mi sijawahi kutoka, ni leo tu.”
“Mama Zawadi naomba uniambie ukweli,” nilipandisha sauti.
“Nilikwenda kwa shoga yangu na wakati wa kurudi mpenzi wake alinipa lifti kwenye gari lake.”
“Huyu mtoto kakukosea nini?”
“Kivipi?”
“Mbona unamfanya kama yatima? Kama unafanya uchafu wako basi mhurumie mtoto, unaridhika na hali ya mtoto kuteseka hivi?”
“Nimemtesa kivipi?” majibu ya mke wangu hayakuonesha kushtushwa na hali ya mtoto wetu.
“Kila ukiondoka unamwacha kwa mama Sonono mtoto hana matunzo, leo tu nimemkuta akila matope, kwani nini umekuwa mkatili kiasi hiki mke wangu?”
“Mume wangu mtoto kuchezea tope ni kitu cha kawaida tu.”
“Uchafu unaoufanya umesababisha mtoto aendelee kuteseka chini kama fundi majiko, au unataka azeeke amekaa?”
“Mwanao mvivu tu wala si mimi.”
“Taarifa zako za kumharibu mtoto kila mtu mtaani anazijua, wanamuonea huruma mtoto, ona miguu ilivyolegea kwa umalaya wako.”
“Sawa mimi malaya, basi nipe talaka yangu.”
“Tatizo si talaka bali kumuonea huruma mtoto.”
“Mi si malaya naomba talaka yangu.”
“Hapa talaka haitoki, kuanzia leo mtoto atakaa kwa mama na siku nikirudi nisipokukuta utanitambua.”
Kwa kweli mke wangu nilikuwa nampenda sana, sikumfanya lolote, tulilimaliza kwa kuniomba msamaha kwa kuondoka bila kuaga lakini suala ya kutoka nje ya ndoa alilipinga kwa nguvu zote huku akiniuliza:
“Lini tulipokutana kimwili ulikuta nimetumika? Mara nyingi mimi ndiye ninayekulazimisha kufanya mapenzi kama ningekuwa si muaminifu kulikuwa na haja gani ya kulazimisha mapenzi kwako?”
Kwa kweli sikuwa na jibu, kwa upande mwingine nilimuona kama mke wangu yupo sawa kwani tangu nimuoe hakuwahi kutoa udhuru kitandani. Tena kwa upande mwingine nilikuwa namuonea huruma kutokana na kazi zangu kurudi nimechoka. Suala la mtoto kumpeleka kwa bibi yake alikubaliana nalo.
Maisha yaliendelea huku nikiamini kabisa mke wangu amejirekebisha, kutoka nyumbani ikawa lazima aage ndipo atoke. Na safari zake nyingi zilikuwa kwenda kumuona mtoto kwa bibi yake. Hilo halikunipa shida nilijua ni sehemu ya upendo kwa mwanaye.
Miezi minne baada ya tukio lile hali ya mtoto ilibadilika, alianza kusimama kwa kunyanyua mguu mmoja. Hali ile ilinifanya niamini kabisa mke wangu hakuwa mwaminifu katika ndoa yetu pamoja na kujitetea kwa kuapa kwa miungu yote.
Kama kawaida, siku moja nikiwa kazini majira ya saa nane mchana, mke wangu alinipigia simu na kunieleza kuwa ameitwa na mama yake mara moja, nilimkubalia. Jioni niliporudi sikumkuta, sikuwa na wasiwasi niliingia ndani na kuoga, baada ya kuoga nilijipumzisha sebuleni kwenye kochi kumsubiri mke wangu arudi.
Kwa vile nilikuwa nimechoka nilipojilaza kidogo usingizi mzito ulinipitia. Nilishtuka usiku na kujiona nimelala muda mrefu, saa ya kwenye simu ilionesha ni saa tatu usiku. Nilishtuka na kwenda nje kulipokuwa na giza nene, nilijaribu kupiga simu yake lakini iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa. Niliporudia kumpigia simu haikupatikana tena.
Nilirudia zaidi ya mara tano lakini haikuwa ikipatikana, niliamini huenda chaji imekwisha, niliendelea kumsubiri nikiamini yupo njiani na angeweza kurudi muda wowote. Mpaka saa tano inaingia, bado alikuwa hajarudi. Wasiwasi ulikuwa mwingi, niliamua kwenda nyumbani kwao kujua kuna kitu gani kilichomfanya mke wangu mpaka muda ule awe hajarudi.
Kabla ya kwenda nilijaribu kupiga simu yake lakini bado haikuwa hewani. Niliondoka na kwenda ukweni kwa kukodi gari lililonipeleka mpaka nyumbani kwao. baada ya kuteremka nilielekea nyumbani kwa wazazi wa mke wangu sehemu niliyokuwa nimepanga wakati naanza maisha.
Nyumba ilikuwa kimya na taa zote zilikuwa zimezimwa kuonesha wamelala, akili ya haraka ilinifanya nifikiri huenda nimepishana na mke wangu ambaye ameondoka muda si mrefu na kufanya wazazi wake walale. Nilitaka kugeuza kurudi lakini niliona ni vizuri niulize ikiwezekana nijue kilichomchelewesha mke wangu kutoka kwa mama yake.
Nilisogea kwenye nyumba na kugonga mlango, baada ya kugonga kwa muda, sauti kutoka ndani iliuliza:
“Nani?” ilikuwa sauti ya mama mkwe.
“Mimi mama.”
“Nani baba Zawadi?” aliifahamu sauti yangu.
“Ndiyo mama.”
Baada ya muda mlango ulifunguliwa, akatoka akionesha alikuwa ameishapitiwa na usingizi.
“Karibu baba.”
“Asante mama.”
“Vipi mbona usiku?”
“Nimekuja kumuulizia mwenzangu.”
“Nani, mama Zawadi?”
”Ndiyo mama.”
“Alikuaga anakuja huku?”
“Ndiyo, alinipigia simu akisema umemwita, nimerudi nyumbani sikumkuta, nimemsubiri tangu nimerudi mpaka muda huu sijamuona na kunifanya niingiwe na wasiwasi.”
“Amekuomba ruhusa saa ngapi?”
“Saa nane mchana.”
“Mmh! Sasa atakuwa wapi, simu yake umempigia?”
“Iliita mara moja bila kupokelewa, niliporudia haikupatikana tena.”
Ulimpigia saa ngapi?”
“Majira ya saa tatu usiku.”
“Mmh! Mbona mtoto huyu ana matatizo!”
“Mama hukumwita?” nilimuuliza bibi Zawadi baada ya kuona hakukuwa na mawasiliano na mwanaye.
“Sijamwita,” alinijibu kwa mkato.
“Sasa atakuwa amekwenda wapi?”
“Kwa kweli sijui.”
“Bora simu yake ingekuwa hewani ingekuwa afadhali lakini ndiyo hivyo haipatikani.”
“Mtoto huyu kawaje jamani, hebu baba rudi nyumbani ukamuangalie huenda amerudi.”
“Sawa mama.”
“Basi utakalokuta lolote nijulishe.”
“Sawa mama.”
Niliagana na mama mkwe na kurudi nyumbani, njia nzima nilikuwa na maswali mengi juu ya ombi la ruhusa ya mke wangu kuwa ameitwa na mama mkwe. Ilionesha wazi msamaha alioomba mke wangu ilikuwa ni danganya toto. Nilijiuliza tabia ile mke wangu kaitoa wapi, toka nilipomfahamu alikuwa msichana mpole, mkimya tena mwenye heshima.
Nilipofika nyumbani sikumkuta mke wangu, niliingia ndani na kukaa kwenye kochi kwa kuhofia kama nitakwenda kulala na kupitiwa na usingizi mzito labda mke wangu anaweza kurudi muda wowote na mimi kushindwa kumfungulia hivyo akalala nje.
Mlango niliurudisha na kuzima taa ya sebuleni, nikakaa kwenye kochi ili kumsubiri mke wangu ambaye sikujua atarudi muda gani. Mpaka muda ule ilikuwa ni saa saba na nusu usiku. Nilijitahidi kukaa macho ili mke wangu akirudi na kugonga basi niwe macho. Kuna kipindi nilipitiwa na usingizi, niliposhtuka nilitoka mpaka nje nikiamini labda nitamuona mke wangu nje baada ya kuniita na kushindwa kumsikia.
Nilizunguka nyumba nzima bila kumuona mke wangu na kurudi tena sebuleni kumsubiri. Siku ya pili ilinikuta nipo sebuleni nikimsubiri mke wangu, nikiwa najiandaa kwenda chumbani mke wangu aliingia akionesha amekunywa pombe, kitu ambacho hakuwahi kukifanya katika maisha yake yote niliyomjua.
MKE WANGU ALISABABISHA NIKAWA MCHAWI
SEHEMU YA 5
Nywele zilikuwa timtim.
“Ooh! Mume wangu, habari za asubuhi?”
“Nzuri, habari za wapi?”
“Nilikwenda kwa mama wakati narudi shoga yangu alinipigia simu kuwa kuna harusi ya ndugu yake. Nilijua nitawahi kurudi kumbe sherehe ni sherehe, kuja kushtuka muda umekwenda na usafiri ulikuwa wa tabu nikaamua kulala huko huko.”
“Kwa nini hukunipigia simu?”
“Wakati unanipigia simu ilizimika hata kabla sijakujulisha.”
“Na mbona umekunywa pombe, umeanza lini?”
“Mume wangu, sherehe ina vishawishi vingi, lakini sikunywa sana.”
Nilijikuta kwa mara nyingine nikishindwa kumhukumu mke wangu, nilimsamehe kwa vile nilikuwa nampenda sana. Ila nilimuomba asiondoke nyumbani bila kuaga pia asinywe pombe. Mke wangu kama kawaida aliniomba msamaha na kuniahidi hawezi kuondoka bila kuaga pia hatakunywa tena pombe.
Kwa mara nyingine nilimsamehe mke wangu kwa vile nilikuwa nampenda sana na sikutaka kumpoteza maishani mwangu kwa kuamini yeye ni kila kitu kwangu. Baada ya tukio lile mke wangu alitulia na heshima ya ndoa ilirudi ndani kama kawaida.
Wakati huo mtoto wetu alikuwa amekaza na kutembea, kitendo cha mwanangu kutembea niliwashukuru sana majirani. Wiki moja baada ya tukio la mke wangu kulala nje aliniomba tuhame mtaa ule.
“Mume wangu naomba tuhame hapa.”
“Tuhame hapa twende wapi?”
“Sehemu yoyote lakini mbali na hapa.”
“Kodi si itatusumbua?” nilimwambia vile kwa kujua hali yangu ya kiuchumi.
“Mume wangu unafanya kazi, acha kujilegeza, inatakiwa sasa hivi tuishi maisha ya kwetu wenyewe bila kumtegemea mtu,” yalikuwa maneno ya kweli lakini yalitakiwa maandalizi ya muda mrefu hasa nikizingatia kulipa kodi ya miezi sita kwa haraka ulikuwa mtihani kwangu.
“Lakini mbona mama alisema hii ni nyumba yako amekupa baada ya kuoana?” ilibidi nihoji baada ya mke wangu kulazimisha kuhama.
“Kazala, husikii tunavyosimangwa kuhusu hii nyumba? Hasa wewe mume wangu maneno yao kwa kweli huwa yananiumiza sana pale wanapokusema vibaya eti nimekuoa badala ya kunioa, hayo ni maneno gani mume wangu?”
“Mmh! Sina jinsi kwa vile ni haraka sana, nipe wiki nijaribu kukopa kazini ili tutafute nyumba.”
“Kuhusu kodi ya kuanzia nitalipa mimi itakayofuata utalipa wewe.”
“Hakuna tatizo,” nilikubaliana naye bila kuhoji fedha ile kaitoa wapi kwa kuhofia kubadili uamuzi wake.
Siku ya pili nilipokwenda kazini, mke wangu alinipigia simu kunijulisha kuwa amekwishahama na kunielekeza nikitoka kazini niende sehemu gani. Nilipotoka kazini nilikwenda sehemu aliyonielekeza na kushtuka kukuta amepanga kwenye nyumba ya gharama, iliyokuwa imo kwenye fensi, kitu kilichonipa wasiwasi na kujiuliza kama kodi aliyolipa mke wangu ikiisha nitaweza kuilipa? Alinipokea kwa furaha mke wangu.
“Karibu mume wangu makazi mapya.”
“Asante.”
“Mbona kama unashangaa?”
“Nashangaa kwa mambo mawili, kwanza nyumba ni nzuri sana na pili nina wasiwasi kodi yake ni kubwa.”
“Ni kweli kodi ni kubwa lakini ni sehemu nzuri tutakayoishi bila bughuza za watu.”
“Nyumba yote kwa mwezi shilingi ngapi?”
“Laki moja na nusu.”
“Mke wangu laki moja na nusu kwa mwezi umelipa muda gani?”
“Mwaka mzima.”
“Ndiyo shilingi ngapi?”
“Hesabu unajua, zidisha laki na nusu mara kumi na mbili.”
“Sasa mimi nitaweza kulia fedha zote hizo?”
“Nitakusaidia, kuwa na amani moyoni mwako.”
Sikutaka kuhoji sana fedha zote hizo kazipata wapi, kwani Waswahili wana kauli yao kuwa ukimchunguza sana bata huwezi kumla na ukimchunguza sana mkeo huishi naye. Tulianza maisha ya kuishi uzunguni, sehemu waliyokuwa wakiishi watu wenye uwezo. Kwa kweli maisha ya makao mapya yalikuwa mazuri sana yenye furaha na amani.
Kwa muda mfupi afya yangu ilirudi katika hali ya kawaida baada ya kuteseka kwa muda mrefu kutokana na vituko vya mke wangu. Kutokana na mke wangu kuonesha kuwa amejirekebisha tulimchukua mtoto wetu na kuishi naye. Heshima aliyoonesha mke wangu ilimshtua hata mama yake mzazi.
Maisha yalisonga mbele huku mke wangu akishika ujauzito wa pili kitu kilichozidi kunipa faraja moyoni mwangu. Lakini ilikuwa tofauti kwa upande wa pili kwani mke wangu hakupenda kubeba ujauzito kwa vile mtoto wetu alikuwa bado mdogo.
“Mke wangu tatizo nini?”
“Huoni Zawadi bado mdogo.”
“Miaka mitatu si midogo na mpaka unajifungua atakuwa amesogea sana.”
“Kwa upande wangu nilipanga kuzaa baada ya Zawadi kufikisha miaka mitano.”
“Basi bahati mbaya, itabidi uzae hivyohivyo.”
“Siwezi lazima niitoe hii mimba.”
“Usiitoe mke wangu, Zawadi tutampeleka kwa bibi yake ili asipate shida.”
“Bado nina hamu ya kumlea mwanangu, kama mtoto utapata tu muda ukifika,” mke wangu bado alisimamia msimamo wake.
“Nakuomba usitoe mimba, nipo chini ya miguu yako mke wangu,” nilimbembeleza mke wangu mpaka nikampigia magoti asitoe mimba.
“Kwa hilo siwezi kukusikiliza, sihitaji senti tano yako nitatoa kwa fedha zangu.”
Kwa mara nyingine mke wangu alinizidi nguvu na kumkubalia kwa shingo upande. Siku ya pili yake nikiwa kazini majira ya saa tisa alasiri, mke wangu alinipigia simu kunijulisha amefanikiwa kuitoa mimba salama. Nilimkubalia lakini upande wa pili moyo uliniuma sana hata kazi ilinishinda na kwenda sehemu ya peke yangu na kulia sana kumpoteza mwanangu mtarajiwa.
Jioni niliporudi tulikutana na hali yangu ya unyonge ilimshtua mke wangu na kunifuata nilipokuwa nimekaa na kunibembeleza.
“Mume wangu, najua kiasi gani nilivyokuumiza, lakini sikuwa na jinsi nilifanya vile kwa maana kubwa. Kwa sasa ni vigumu kunielewa lakini amini nilichokifanya si kukukomoa bali kumpa nafasi Zawadi. Kumbuka makosa yangu ya awali yalimtesa mwanangu hivyo sasa hivi nina deni la kumlea.”
Kutokana na kumpenda sana mke wangu nilikubaliana naye, maisha yalisoga huku akionesha mapenzi mazito kwangu, kitu kilichofuta mawazo ya kutoa ujauzito.
Siku zote kimya kingi kina mshindo mkuu, mwezi mmoja baada ya kutoa ujauzito. Siku moja nilidamka asubuhi kwenda kazini hali yangu haikuwa nzuri. Lakini nilijitahidi kwa kuamini mwanaume si mtu wa kujilegeza. Nilipofika kazini nilijitahidi kufanya kazi lakini kutokana na kufanya kazi juani, hali ilibadilika na kuwa mbaya hivyo niliruhusiwa kwenda hospitali kupata matibabu.
Nilikwenda hadi hospitali ya wilaya na kupata huduma japo dawa nilikwenda kununua duka la madawa. Nilibeba dawa zangu na kurudi nyumbani kupumzika. Nilipofika nyumbani ndani ya geti nilikuta kuna gari ambalo kwangu halikuwa geni sana japo sikukumbuka nililiona wapi.....
Share
0 Maoni