Ticker

6/recent/ticker-posts

MKE WANGU ALISABABISHA NIKAWA MCHAWI*6----10*

SEHEMU YA *6-----------10*

Baada ya kutafakari niligundua lile gari ndilo lililomshusha mke wangu siku niliporudi nyumbani ghafla, nilishtuka kulikuta nyumbani na kujiuliza limefuata nini pale. Niliingia ndani na kukuta sebuleni kuna pombe kali juu ya meza na glasi mbili. 

Sikujishughulisha navyo nilielekea chumbani, nilipofika kwenye  mlango wa chumbani nilikuta umefungwa na ndani nilisikia sauti mbili, ya mwanamke na mwanaume. Sauti ya mwanamke ilikuwa ya mke wangu na ya kiume sikujua ni ya nani. Kwa haraka nilitoka mpaka nje na kuzunguka dirishani na kuchungulia ndani.

Niliyoyaona ndani nusura mapigo ya moyo wangu yasimame ghafla. Kitandani kwangu alikuwepo mke wangu na mwanaume mmoja ambaye hakuwa mgeni sana machoni mwangu japo sikukumbuka niliwahi kumuona wapi, wote wakiwa kama walivyozaliwa.

Ilionesha walikuwa wamemaliza kufanya uchafu wao muda si mrefu kwa jinsi walivyokuwa wamejilaza. Nilihisi miguu haina nguvu na kurudi chini bila kujieleza na kukaa kama mzigo. Nikiwa nimekaa chini huku  nimeegemea ukutani nilisikia homa ikipanda mara mbili na jasho likinitoka kama maji, nikajiona kama nakufa muda si mrefu.

Nikiwa nimekaa chini niliyasikia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea ndani.

“Sasa kwa nini uliitoa ile mimba, si uliniahidi utanizalia mtoto,” sauti ya kiume ilisema.

“Ni kweli, lakini damu yako ni kali sana ningeiacha ingeniletea matatizo katika ndoa yangu.”

“Matatizo gani?”

“Nilikuwa na wazo hilo, lakini siku niliyowaona watoto wako wanafanana kama mayai niliogopa. Nilikueleza niwe mke wako wa pili hutaki, ningejifungua humu ndani japo mume wangu asingejua kitu lakini walimwengu wangemweleza. Hata kutoka kwangu kuna watu wenye roho mbaya walimueleza.

“Bila kuhama kule mambo bado yangekuwa mabaya, japo inabidi kutokana na kukupenda lakini wakati mwingine namuonea huruma mume wangu. Toka tuhamie huku pamekuwa kama kwako, unakuja muda wowote unakula na kuvaa tofauti na kwako. 

“Ukitaka nikuzalie mtoto nitoe kwa bwana huyu haichukui hata mwezi nitakubebea mimba.”

“Nimekuelewa mpenzi wangu, lakini japo tunamfanya yule jamaa fala huwa sijiamini sana kuja hapa, unafikiri akitufumania tutafanyaje?”

“Hawezi kutufumania.”

“Kwa nini unasema hivyo?”

“Nimekueleza haruhusiwi kurudi nyumbani bila kunijulisha.”

“Kwa nini nisikupangie nyumba nyingine au uwe unatoka na kuwahi kurudi, huku nani anakufahamu?”

“John hebu acha kuniudhi, nilikulazimisha tuhamie huku ili tujitawale sasa unataka twende wapi?”

“Si unajua wewe mke wa mtu.”

“Hili umelijua leo, tuna muda gani toka tuhamie hapa?”

“Muda mrefu.”

“Basi naomba wazo la kufumaniwa uliondoe.”

“Sasa mpenzi acha nikukimbie.”

“Mbona haraka.”

“Nilipokuja nilikueleza nini?”

“Ooh! Nilisahau kwa hiyo mpaka kesho kutwa?”

“Ndiyo maana yake.”

“Basi twende tukaoge uwahi.”

Niliwasikia watu wakinyanyuka kwa sauti ya kitanda kupiga kelele. Nikiwa nimekaa chini. Niliamini kama mke wangu akigundua nimemfumania angeomba talaka kutokana na kauli aliyokuwa akiitoa ndani. Nilinyanyuka pale chini huku miguu ikiwa haina nguvu na kutoka nje ya geti kwa shida huku nikitetemeka. Nilisogea mbali na nyumbani ili kusubiri jamaa aondoke ili nipige simu kuwa nipo njiani.

Kutokana na hali yangu kuwa mbaya sikufika mbali sana kizunguzungu na kichefuchefu vikanibana. Nilisogea kwenye mti wa jirani na nyumbani na kutapika sana kisha nikalala kwenye matapishi kwa vile sikuwa na nguvu ya kujinyanyua. Huwezi kuamini, usingizi ulinipitia palepale kwenye matapishi mpaka niliposhtuliwa na msamaria mwema mmoja aliyekuwa akipita njiani na kunikuta kwenye hali ile.

“Vipi kaka?” aliniuliza akiwa amesimama pembeni yangu.

“Naumwa,” nilimjibu kwa mkato huku nikijinyanyua kwenye matapishi.

“Unakaa wapi?”

“Pale,” nilisema huku nikionesha ninapokaa ambako hapakuwa mbali.

“Unaweza kusimama?”

Nilijaribu kunyanyuka kidogo nilikuwa na nguvu, yule msamaria mwema alinisaidia mpaka nyumbani. Bahati nzuri mke wangu alikuwa nje, aliponiona alishtuka na kuja mbio.

“Jamani mume wangu, umekuwaje?”

“Naumwa,” nilimjibu kwa sauti ya chini.

Walisaidiana kuniingiza ndani na kunilaza sebuleni, baada ya kunifikisha msamaria mwema aliaga.

“Jamani mi niwakimbie.”

“Asante ndugu yangu,” nilimshukuru.

“Hakuna tatizo Mungu atakusaidia.”

“Asante kaka yangu.”

“Hakuta tatizo.”

Yule mtu aliondoka na kuniacha na mke wangu ambaye alionesha kushtushwa na hali yangu.

“Mume wangu vipi?” aliuliza huku akitokwa na machozi.

“Naumwa?” nilimjibu huku moyo wangu ukiniuma mpaka machozi yalinitoka kitu kilichomshtua mke wangu na kuzidisha kilio. 

“Maskini mume wangu, unaumwa nini baba Zawadi?”

“Malaria.”

Alinichukua hadi bafuni na kunivua nguo zote kisha alinimwagia maji, na kunisaidia kurudi ndani. Alinitengenezea uji haraka na kuninywesha, kila kitendo cha upendo alichonifanyia mke wangu kiliuumiza moyo wangu baada ya kuona ni unafiki.

 Lakini mke wangu ugonjwa wangu ulimgusa sana, muda wote alikuwa karibu yangu mpaka nilipopitiwa na usingizi. Nilipoamka nilimkuta pembeni yangu mkono shavuni.

“Mume wangu,” aliniita kwa sauti ya upole.

“Naam.”

“Poleee.”

“Asante.”

“Unaendeleaje kwa sasa?”

“Sijambo kidogo.”

“Nikutayarishie chakula gani?”

“Sijisikii kula,” pamoja na huruma yake ya mamba sikuipenda zaidi ya kumuona mnafiki.

“Mume wangu, kumbuka umemeza dawa kali, unatakiwa kula ili dawa zifanye kazi.”

“Nitakula baadaye.”

“Hapana, kuna ndizi na nyama nimekuandalia, naomba ule kidogo.”

“Hapana sijisikii kula.”

“Mume wangu.”

“Naam.”

“Mimi nani yako?”

“Mke wangu.”

“Unataka nani akubembeleze ili umsikie?”

“Wewe.”

“Kwa nini hutaki kunisikia?”

“Si nimekueleza nitakula baadaye.”

“Ni wazi huna mapenzi na mimi hata kunisamehe kwako kulikuwa kwa uongo.”

“Jamani mi si naumwa?”

“Kuumwa gani, ni wazi najilazimisha kwako huna mapenzi nami.”

Nilishangaa mke wangu akizungumza kitu ambacho hakikuwepo zaidi ya mimi kutojisikia kula. Niliamini kama nitaendelea kukataa naweza kuzalisha mapya, nilikubali kula kitu kilichomfurahisha mke wangu.

Baada ya kula nilijitahidi kulala lakini usingizi uligoma kunichukua, kila nilipofumba macho niliyaona matukio yote yakijirudia toka la mwanangu kuchelewa kutembea na siku niliporudi ghafla na kumkuta mwanangu akiwa katika mazingira mabaya.

Pia nilipomshuhudia mke wangu akiteremka kwenye gari na pia siku aliyorudi siku ya pili na kunidanganya kuwa alikuwa kwenye sherehe ya harusi kumbe alikwenda kulala na mwanaume. Na la siku ile nililoshuhudia kwa macho yangu akiwa na mwanaume kama walivyozaliwa katika kitanda changu na kuonesha walikuwa wameshafanya uchafu wao. Pia kusikia sababu ya kutoa mimba kwa kusingizio cha kumlea mtoto wetu Zawadi kumbe haikuwa mimba yangu bali ya yule mwanaume aliyempangia nyumba ile.

Kila yalivyojirudia akilini mwangu moyo uliniuma sana na kujikuta nalia peke yangu kitandani nikiwa nimejifunika shuka ili mke wangu asijue. Nilipata wazo la kuachana naye lakini moyo ulikataa kwa kuamini sitampata mwanamke mzuri kama yule.

MKE WANGU ALISABABISHA NIKAWA MCHAWI

SEHEMU YA 7 

Niliamua kufa Kizungu na tai shingoni, niliificha siri ile moyoni mwangu kwa kuamini kama ningeisema basi ningeachana naye kwa mazingira niliyoyaona na mazungumzo niliyosikia. Kwa kuwa sikupenda kuwepo nyumbani kutokana na kuumia kila nilipomuona mke wangu, niliamua kwenda kazini siku ya tatu japo sikuwa nimepona vizuri.

Baada ya tukio lile nilizidi kuteseka kwenye maisha yangu kwani kila nilipokuwa kazini, nilijua mume mwenzangu atakuja nyumbani. Moyo ulikuwa ukinilipuka kwa kujua  muda ule nilikuwa nasalitiwa. Kila nilipokuwa peke yangu nilijikuta nashindwa kufanya kazi na kuhama kimawazo, nikawa nahisi kama dunia nzima nimeibeba kichwani mwangu.

Kutokana na kuwa na wasiwasi wa moyo juu ya vitendo vya mke wangu, hali yangu ilianza kubadilika. Nilikuwa nikipungua mwili kila kukicha, suruali zangu zote niliongeza matundu ya mkanda matatu kurudi nyuma ili zikae kiunoni. Wa kwanza kunigundua  hali hiyo alikuwa mke wangu ambaye alitaka kujua nina tatizo gani.

“Mume wangu mbona upo hivi, una tatizo gani?”

“Nipo sawa,” nilijibu kwa mkato.

“Hapana mume wangu, kuna kitu kinakusumbua.”

“Mbona mimi nipo sawa.” 

“Si kweli, toka ulipougua hujarudi katika hali yako ya kawaida, pia hata ule uchangamfu wa ndani umepotea. Kama bado unaumwa turudi hospitali tujue una tatizo gani.”

“Hapana nipo sawa,” niliendelea kumkatalia mke wangu.

Nilimkatalia kwa kuamini chanzo ni yeye hata kama ningemwambia kuwa nilimuona akifanya mapenzi na mwanaume mwingine kwenye kitanda changu ningeongeza msumari wa moto kwenye kidonda. Nilijua lazima angeomba talaka kutokana na kunipa masharti nikirudi nyumbani nimpigie simu japo nilimpigia zaidi ya mara kumi bila kupokelewa. 

Pia niliyafuatilia maneno yake aliyomhakikishia yule mwanaume kuwa siwezi kurudi nyumbani kwa vile alinieleza nirudi kwangu kwa taarifa. Niliamini kama ningemueleza ningekuwa nimevunja masharti ya kurudi nyumbani bila taarifa japo simu haikupokelewa.

Kama angeamua kuniacha kwangu lingekuwa pigo kubwa kutengana na mke wangu ambaye pamoja na matatizo yote bado alikuwa mtu muhimu sana kwangu.

“Au bado una yaleyale?” mke wangu aliniuliza kwa sauti ya unyonge.

“Yapi hayo?” nilimuuliza kwa kuhofia ameshtukia kilichokuwa moyoni mwangu.

"Si kuhusu mgogoro wetu wa mi natembea nje ya ndoa.”

“Walaa yote mbona yaliisha.”

“Ndiyo maana nikaja kupanga huku tuishi kwa raha mustarehe, mume wangu toka tuhamie huku nimeisha ondoka bila ruhusa yako?”

“Hapana.”

“Au nimeishafanya jambo lolote baya?”

“Hapana.”

“Au la kutoa mimba bado linakutesa?”

“Walaa.”

“Sasa nini mume wangu?”

“Nina wasiwasi malaria bado haijaisha,” ilibidi nidanganye ili kumfanya mke wangu aachane na mimi kwa vile alikuwa kero mbele yangu.

“Basi mpenzi naomba ukaangalie afya yako kwa kweli hali yako ilivyo hata mimi sina raha,” mke wangu alisema kwa sauti ya huruma.

“Nina imani nitakuwa katika hali ya kawaida muda si mrefu.”

“Fanya hivyo mume wangu,” maneno ya mke wangu bila kumfumania nisingekubali kama anahujumu ndoa yetu, alikuwa na maneno matamu yenye kumfanya maskini kujiona tajiri na asiye na nguvu kujiona anaweza kuibeba dunia nzima peke yake.

Nilikubaliana naye ili kuwa mbali naye, lakini kazini moyo wangu ulikosa raha na kujuta  siku niliyokuwa naumwa kurudi nyumbani. Heri ningeendelea kuamini naibiwa bila kuwa na uhakika kama siku ile niliyoshuhudia kwa macho yangu.

Kila nilipokuwa peke yangu tukio la kumfumania mke wangu lilijirudia na kuwa mateso mazito moyoni mwangu. Kila kukicha mwili wangu ulikuwa ukikongoroka, kila aliyenijua aliniuliza nimekumbwa na kitu gani akiwemo bosi wangu ambaye alinibembeleza nimueleze nasumbuliwa na nini ili anisaidie hata kwa fedha zake za mfukoni.

Moyoni niliapa kufa na siri yangu kwa kutomwambia mtu yeyote aibu yangu. Hali yangu ya kiafya ilizidi kubadilika, mwili kila kukicha ulipungua uzito kwa mawazo, chakula nilikula lakini sikusikia ladha yake. Kuna kipindi nililaani kuwa maskini kwa kuamini kama ningekuwa na uwezo mke wangu asingechukuliwa na mwenye fedha.

Rafiki yangu wa karibu, Simon alinifuata siku moja baada ya kunikuta nimejisahau huku machozi yakinitoka.

“Kazala,” aliita kwa sauti.

“Ee..eeh?” nilishtuka kama nilikuwa usingizini.

“Kazala una tatizo gani rafiki yangu?” aliniuliza akiwa amenikazia macho.

“Sina tatizo,” nilimjibu huku nikifuta machozi kwa kiganja cha mkono.  

“Hapana Kazala kuna tatizo zito ulilonalo lakini hutaki kulisema.”

“Nipo sawa rafiki yangu,” nilikataa kwa kuamini kusema linalonisumbua nitakuwa nimejivua nguo hadharani.

“Kalaza unajiona ulivyo?”

“Kwani vipi?” nilijifanya kushtuka japo ukweli niliujua.

“Kazala haupo sawa, usiponieleza mimi swahiba wako utamueleza nani? Kumbuka mimi huku ndiye ndugu yako wa karibu. Japo tangu mlipohamia Uzunguni hutaki nifike kwako kwa kusingizio cha mkeo na kusahau ukifa sisi ndiyo wa kukuzika.”

Kauli ya Simon ilikuwa na ukweli kwani ndiye aliyekuwa mtu wangu wa karibu kwa kuelezana siri zetu za ndani. Lakini siri ya mke wangu sikumueleza japo ilikuwa ikifahamika mtaani lakini hakukuwa na mfanyakazi mwenzangu aliyekuwa akijua nini kilichokuwa kikiendelea ndani ya nyumba yangu.

Pia mke wangu baada ya kuhamia makao mapya alipiga marufuku rafiki zangu wote akiwemo mtu wangu wa karibu kama Simon wasifike kwetu, nami kutokana na mapenzi mazito nilimkubalia.

“Simon nipo sawa,” bado niliendelea kufa na siri yangu moyoni.

“Kazala nitazame.”

Nilimtazama, tulikaziana macho kwa muda kisha alisema:

“Kazala una tatizo zito, nakwambia utakufa kwa kihoro.”

“Kihoro?” nilishtuka.

“Ndiyo, kila kukicha utapungua mwisho utakufa umelala.”

“Una maana gani?” kauli ya Simon ilinishtua.

“Hujioni, hii ni hali yako?” ajabu Simon alikuwa mkali kama yeye ndiye mwenye tatizo.

“Sasa kipi cha ajabu?” nami nilikuwa mkali.

“Mkeo atakuua.”

“Eti?” nilishtuka kusikia vile.

“Unashtuka nini?”

“Umejuaje?”

“Siyo nimejuaje, kila mtu anakuonea huruma, kwa akili yako unaona ni siri kwa vile hutaki ushirikiano na kumuona mkeo ni kila kitu, watu wote wamekuacha waone mwisho wake. Lakini sipo tayari kukuona ukipotea kwa vile unanihusu Kazala.”

Yalikuwa maneno makali yaliyonifanya mwili wangu utetemeke na jasho kunitoka. Kauli ile ilikuwa kama mkuki moyoni mwangu, nilijikuta midomo na koo vikinikauka ghafla na kukosa la kusema, nikajiona kama mtu niliyekuwa nikitembea uchi siku zote na kujiona nimevaa kumbe watu wananiona sina nguo. Moyo uliniuma sana na kujiona kiumbe niliye na bahati mbaya.

Nikiwa nimeinama chini kama mwari machozi yakinitoka, Simon alinishika begani na kuniita jina langu.

“Kazala.”

Sikuitikia kwani midomo ilikuwa kama ina nta, kila nilipojaribu kuifungua ili niitikie iligoma kufunguka. Nilinyanyua uso na kumtazama Simon aliyekuwa akinitazama kwa jicho la huruma huku machozi yakinitoka.

“Kazala,” aliniita tena.

“Na.na..am,” niliitika. 

“Pole sana, najua kiasi gani mapenzi yanavyotesa.”

“Ninyi mmejuaje?” nilijikakamua na kumuuliza swali ambalo niliamini ni siri yangu.

MKE WANGU ALISABABISHA NIKAWA MCHAWI

SEHEMU YA 8

“Mbona siri ipo wazi, taarifa hizi zilinifikia muda mrefu tangu matatizo ya mwanao kuchelewa kutembea. Pale mtaani kwenu kila nilipokuja kukutembelea nilielezwa tabia chafu za mkeo lakini nilishindwa nianzie wapi kukueleza kutokana na wewe jinsi unavyompenda mkeo.

“Kwa kweli nilihofia kuitenganisha nyumba yako kutokana na wewe kumuamini sana mkeo. Huwezi kuamini kuna mtu mmoja wa nyumba mliyokuwa mnakaa zamani, kila nilipokuja na kuondoka alinifuata njiani na kunieleza unavyopelekwa na mkeo kwa tabia zake chafu na kuniomba nikueleze ili uweze kumdhibiti mkeo.

“Lakini bado ningeanzia wapi kukueleza unielewe? Bado kwangu ulikuwa mtihani mkubwa. Baada ya ninyi kuhama nilikutana naye tena yule aliyekuwa akinipa taarifa za mkeo, akaniambia kuwa nyumba uliyohamia umepangiwa na mwanaume mwenzio, bwana wa mkeo. 

“Kwa kweli habari zile ziliniumiza sana lakini vilevile sikuweza kukueleza chochote baada ya mkeo kukukataza usitembelewe na rafiki zako nikiwemo mimi mtu wako wa karibu. La kunikataza nisije kwako halikuniumiza kwa vile hata nilipoacha kuja kwako hakuna kilichopungua kwangu. 

“Hali yako ya sasa iliwachanganya sana watu wengi, najua uliulizwa na kila mtu akiwemo bosi, hakuna hata mmoja uliyemueleza tatizo lako. Juzi kuna kitu nilisikia sijui mkeo katoa mimba ya mwanaume wa nje na watu kusema huenda imekuchanganya sana. 

“Japokuwa nilikuwa najua kila kitu lakini nilitaka kauli toka kwako kwa kujitahidi kukubembeleza lakini umekuwa ukificha ukweli wakati unazidi kuteketea. 

“Lakini hali yako kila kukicha imekuwa ikizorota huku ukiwa mtu wa kuhama kimawazo kila dakika, unajisahau kama upo kazini.  

“Wengi wanakuonea huruma japokuwa matatizo yako wewe unajua ni siri yako, kutokana na kufanya siri wenzako waliamua kukuacha waone mwisho wako, wengi wanakuona mjinga kuendeshwa na mwanamke. “Hebu naomba unieleze kila kitu usinifiche mimi rafiki yako. Kwa nini umefikia hatua hii ikiwa kila kitu cha mke wako unakijua?” alisema Simon kwa uchungu.

“Simon, sijui hata nikwambie nini? Kwa kweli vitendo vya mke wangu vinaniumiza na kunitesa sana. Nilimuamini sana lakini aliyonifanyia nashindwa nifanye nini. Niliona aibu kukueleza mwanzo kwa kuogopa aibu hii, lakini kumbe natembea uchi nikiamini nimevaa nguo,” niliinama kwa uchungu huku machozi na kamasi vikinitoka.

 Moyo uliniuma na kujiona kwa hali ile sikuwa na faida ya kuendelea kuishi. Niliona heri nife kuliko aibu ile ambayo nilijiuliza kazini pale watanielewaje? Baada ya kuwaza na kukosa jibu, nilimuuliza Simon anaweza kunisaidia nini.

“Simon ndugu yangu hapa nilipo najiona kiumbe nisiye na faida duniani.”

“Kwa nini?”

“Hebu nieleze nitaficha wapi sura yangu ikiwa kila mtu anaijua siri yangu, kupungua kwangu si kwa sababu ya yote uliyosema ni kitu kingine kabisa, heri nife.”

“Ufe kwa ajili ya mwanamke?”

“Ndiyo Simon, jambo alilonifanyia kwa kweli limeniumiza sana sana.”  

“Kitu gani tena rafiki yangu?”

Kwa vile kila kitu changu kilikuwa wazi niliamua kumueleza ukweli nilivyomfumania mke wangu na mwanaume ndani ndipo aliponiuliza huku ameshika mdomo kwa mshtuko.

“Ha! Halafu ukafanyaje? Haki ya nani ningekuwa mimi, sasa hivi ningekuwa nasubiri hukumu ya kunyongwa. Ndani ya nyumba yangu tena kitandani kwangu? Dharau gani hiyo Kazala?” Simon aliniuliza, macho yakiwa yamemtoka pima.

Nilimueleza nilivyoondoka na homa yangu na niliyoyakuta na jinsi nilivyoshindwa kuingia ndani na kuondoka na kuzidiwa na kuanguka njiani kisha kulala kwenye matapishi.

“Kazala...kazala...Kazala huo ni uanaume gani? Unamuacha mgoni wako chumbani kwako tena kitandani kwako? Hata kama nyumba amepanga bado pale ni kwako. Kibaya umeondoka unaumwa unataka kufia njiani, rafiki yangu hayo ni mateso gani anayokutesa mkeo?”

“Ningefanyaje na mke wangu alinikataza nisirudi nyumbani mpaka  nimtaarifu. Kama ningerudi na kumfumania lazima ningekuwa nimevunja makubaliano yetu na angedai talaka.”

“Kazala umeoa au umeolewa?”

“Nimeoa.”

“Kwa nini mkeo akupande hadi kichwani na kukupangia atakavyo?” Simon alisema kwa uchungu.

“Siyo kunipangia ni makubaliano yetu,” nilijikuta nikimtetea mke wangu pamoja na yote aliyonifanyia.

“Acha ujinga, mwenye amri kwenye nyumba ni mwanaume, umeona sababu ya kupangiwa kurudi nyumbani? Ilikuwa ili ajiandae usimfumanie. Umerudi mara moja na kukuta yale, hebu jiulize tangu mhamie hapo ni mara ngapi yule mwanaume anakuja kama kwake na kufanya uchafu wake?”

“Nashangaa sasa hivi sijui amekuwaje, lakini siku zote mke wangu alikuwa mtu mwenye heshima, hata sijui kabadilika vipi?” bado niliendelea kumtetea mke wangu.

“Kazala mkeo si mtulivu tangu mwanzo, sema ulikuwa hujui kwa vile jambo usilolijua ni sawa na usiku wa giza. Lakini hafai kuwa mke wa mtu. ”

“Kwa hiyo unanishauri nini kwa hili?”

“Hapa hakuna chochote cha kufanya, kama umeyajua yote mabaya ya mkeo na mengine kushuhudia kwa macho yako unasubiri nini, unataka akuue?”

“Unanishauri nifanye nini?”

“Yule mwanamke hakufai, achana naye ujipange upya bila hivyo atakuua kwa kihoro. Hebu jiangalie, umeshuhudia uchafu wa mkeo mara moja tu, umekuwa hivi kama mgonjwa wa kifua kikuu. Ameshakujua wewe nyoka wa plastiki huumi, ipo siku atakuteremsha kitandani ili alale na mwanaume wake.”

“Wee atawahi?” nilijikakamua mwanaume.

“Utafanya nini?”

“Nitaua mtu.”

“Hukuua mtu ulipofumania watu wapo kitandani hawana nguo mwilini, utaweza kusema kitu mbele ya mwanaume mwenzako aliyewapangia nyumba?”

“Lakini nilimsikia akisema hata yeye hapendi kuja pale nyumbani ila mke wangu ndiye anayemlazimisha,” najua majibu yangu yatakufanya unicheke na kuniona zuzu, nioneeni huruma mwenzenu kweli nilikamatika, kupenda kubaya, nilikuwa zuzu kwisha kazi.

“Kazala majibu gani hayo? Mbona kupenda kumekugeuza zuzu, au umeinamishwa?”

“Sijainamishwa,” nilikataa katakata neno la kuinamishwa na mke wangu zaidi ya kumpenda tu.

“Basi ndugu yangu kwa usalama wako muache yule mwanamke kabla hajakuacha, la sivyo muda si mrefu utakufa au kuwa nwendawazimu.”

“Kwa kweli kuachana na mke wangu siwezi labda unipe njia nyingine ya kumtuliza.”

“Utamtuliza vipi?”

“Kwa vyovyote vile hata kwenda kumueleza yule jamaa aachane na mke wangu.”

“Mimi siwezi kufanya hiyo kazi, labda ukamueleze mwenyewe kwani mbaya wako si unamjua?”

“Basi nakuomba kitu kimoja.”

“Kitu gani,” kauli ile ilinifanya nikae vizuri kumsikiliza.

“Kuanzia sasa hivi amri zote za nyumba utoe wewe, kurudi nyumbani asikuwekee amri, mweleze mwenye uamuzi wa mwisho ni wewe. Kila kitu kitakuwa chini yako, pia omba mkopo ukatafute chumba ili mhame nyumba ile ya mwanaume mwenzio ili uweze kumdhibiti mkeo, bila hivyo utatwanga maji kwenye kinu.”

“Sawa nitafanya hivyo.”

Nilikubaliana na Simon, kwa vile muda wa kutoka ulikuwa umefika tulitoka kazini na mimi kurudi nyumbani nikiwa na mawazo tele jinsi ya kumueleza mke wangu. Nilijiuliza atapokeaje uamuzi wangu mpya? Lakini niliamini njia ile ya kuvunja amri pia kuhama nyumba ya mwanaume mwenzangu na kuhamia kwangu huku nikiweka amri mpya itaweza kunifanya nimdhibiti mke wangu.

Nilipofika nyumbani, kama kawaida mke wangu alinipokea kwa heshima zote huku akionesha upendo kwa kuongeza baadhi ya vitu kama kunichemshia maji ya kuoga na kula pamoja. Vitu vile ndivyo vilinifanya nipiganie kwa nguvu zangu zote kuhakikisha mke wangu anabaki mikononi mwangu.

MKE WANGU ALISABABISHA NIKAWA MCHAWI

SEHEMU YA 9

Baada ya chakula cha usiku tukiwa kitandani nilimuuliza mke wangu kwa sauti ya chini. 

“Mke wangu.”

“Abee mume wangu,” aliitika huku akifumbua macho yake makubwa kidogo ambayo nilipenda kuyatazama kila wakati.

“Mimi nani?”

“Mume wangu.”

“Nani mwenye amri huku ndani?”

“Mbona umeniuliza hivyo?” swali langu lilimshtua.

“Naomba unijibu swali langu siyo kuulizwa swali,” nilikaza sauti.

“Mmh! Mume wangu mbona leo mkali hivyo?”

“Mke wangu naomba unijibu swali si kuniuliza swali,” nilijikakamua  mwanaume huku mapigo ya moyo yakinidunda na kusema kwa ukali kidogo. 

“Wewe mume wangu.”

“Basi kuanzia leo mimi ndiye nitakayekuwa natoa amri humu ndani.”

“Mume wangu maneno gani hayo, lini ulitoa amri ikapigwa?” mke wangu aliniuliza huku akinitazama kama hanioni vizuri.

“Sijawahi kupingwa, lakini kuna mambo yanayoendelea humu ndani sikubaliani nayo.”

“Mambo gani mume wangu?”

“Ya kupangiwa kuwa nikitaka kurudi mapema nyumbani lazima nitoe taarifa.”

“Sasa hapo kuna ubaya gani?”

“Upo, kwa vile huwezi kunipangia nikirudi nyumbani mapema lazima nikutaarifu.”

“Sasa hapo kuna ubaya gani?”

“Upo, kwa vile siwezi kurudi kwangu kwa kutoa taarifa.”

“Nia yangu ilikuwa kuhakikisha ukirudi niwepo nyumbani.”

“Unakwenda wapi?”

“Labda naweza kuitwa na mama.”

“Nani wa kumtaarifu mwenzake kwamba anaondoka  nyumbani.”

“Mimi.”

“Pia hata nisipokukuta nyumba haiondoki.”

“Sasa ulikuwa unatakaje?”

“Nataka nirudi bila kukupigia simu.”

“Ni hilo tu mume wangu?”

“Ndiyo.”

“Basi, fanya uwezavyo, kwa nini tugombane kwa jambo dogo?”

Nilikubaliana na mke wangu ambaye niliamini tungebishana hata kutishiana kuachana, lakini alikuwa mwelewa kitu kilichonifanya niwaze labda wameachana na yule mwanaume. 

Siku ya pili niliporudi kazini, nilikwenda kwa mkuu wangu wa kazi na kumuomba mkopo kwa ajili ya kuhamia nyumba nyingine. Ilikuwa ajabu nilipofika tu alinikaribisha kitini kwa uso wa tabasamu lililojaa huruma iliyoonesha yupo tayari kunisaidia.

“Karibu Kazala,” alinikaribisha kwa sauti ya upole.

“Asante bosi.”

“Ndiyo, nikusaidie nini?” bosi aliniuliza huku akinitazama usoni.

“Bosi nilikuwa naomba mkopo wa kulipia nyumba ili nihame nilipokuwa nakaa, nina imani kila kitu unajua.”

“Najua, lakini hukutaka kuniambia.”

“Tusameheane mkuu wangu si unajua kuelemewa kubaya.”

“Najua, kwa hiyo hii itakuwa tiba ya matatizo yako?”

“Nina imani nipo katika mkakati huo kuhakikisha ninadhibiti kila sehemu.”

“Mmh! Sawa, unataka kiasi gani?”

“laki mbili na arobaini.”

Baada ya kusema vile bosi aliinama na kuandika kwenye kikaratasi na kunieleza nikipeleke uhasibu.

“Kampe mhasibu.”

“Asante bosi,”nilikipokea na kushukuru.

“Kawaida tu, chumba umeishapata?”

“Simon alinieleza nikipata mkopo kuna sehemu anaijua ina vyumba.”

“Unataka uhamie lini?”

“Ikiwezekana hata leo.”

“Basi una nafasi ya kuondoka kwenda kulipia ikiwezekana leo hii uitumie kwa ajili ya kuhama kabisa.”

“Nashukuru sana bosi.”

Nilitoka hadi uhasibu na kumpa kikaratasi mhasibu aliyekisoma kisha alivuta droo ya fedha na kuhesabu laki mbili na arobaini na kunipa. Baada ya kuipata ile fedha niliamini kabisa kila kitu kitakwenda kama kilivyopangwa. Nilijishangaa kujiona nimekuwa na nguvu za ajabu, hata hali yangu ya uchangamfu ilirudi kama zamani kitu kilichowashangaza watu wengi walioniona muda ule.

Wa kwanza kunifikia alikuwa Simon na kuniuliza:

“Vipi mwenzangu?”

“Aisee mambo yamekwenda kama ulivyoyapanga jana, huwezi kuamini kila ulichokisema kimekwenda vilevile.” Nilimweleza huku nikionesha uso wa furaha.

“Mkopo umepata?”

“Ndiyo, yaani nilipomuomba hakuniuliza kitu chochote zaidi ya kuniandikia karatasi kwenda kuchukua uhasibu.”

“Na nyumbani?”

Nilimueleza yote niliyokubaliana na mke wangu kitu kilichomshtua.

“Yaani mkeo kakubali kirahisi tu.”

“Hata mimi nimeshangaa japo mwanzo alitaka kupinga lakini kauli ya kiume ilimfanya akubaliane na matakwa yangu.”

“Japokuwa kazi ni nzito, lakini mwanzo unaonekana mzuri, vipi umemtaarifu mnahama?”

“Nimtaarifu ili iweje, yeye alipohamia kule alinitaarifu?” nilimjibu kwa kujiamini.

”Kwa hiyo?”

“Bosi katoa ruhusa ya kwenda kulipia na kuhamia leo.”

“Sasa mimi nitatokaje?”

“Nimekuombea ruhusa kabisa.”

Niliondoka na Simon hadi  sehemu iliyokuwa na hicho chumba na sebule, kwa kweli kilikuwa katika hali nzuri sana. Nililipia miezi kumi ili nibakie na fedha ya kubebea mzigo.

Baada ya kutoka kulipia chumba tulipita kwenye magari ya mizigo na kukodi gari hadi nyumbani. Nilipofika nilimkuta mke wangu akifua nguo, aliponiona naingia nimo ndani ya gari alishtuka sana.

“Vipi mume wangu?”

“Leo tunahama.”

“Na hapa?”

“Tunamuachia mwenyewe.”

“Mwenyewe nani?”

“Mke wangu huu si muda wa maswali, tupakie mizigo tuhamie makazi mapya.”

“Mume wangu mbona kodi yetu ndiyo ina miezi saba tu.”

“Hiyo iliyobaki atakaa mwenyewe.”

“Mume wangu mwenyewe nani, mwenyewe si sisi?”

“Mke wangu, hebu nyanyuka tuondoke.”

“Mume wangu mbona toka jana sikuelewi kuna nini?”

“Hebu kwanza tuhame kwanza muda si mrefu utanielewa.”

Tulikubaliana kuhama japo kwa shingo upande, tulipakia mizigo nikisaidiana na Simon, baada ya kupakia tuliondoka na kuhamia sehemu nyingine kwenye nyumba yenye wapangaji watatu na sisi kuwa wa nne. Baada ya kupanga vitu huku mke wangu akionekana kulazimishwa sikuiangalia ile hali.

Kwa vile siku ile nilikuwa na ruhusa, nilipumzika na  Simon aliondoka kwenda kwake. Tukiwa tumebaki wawili mke wangu aliniuliza:

“Sasa ndiyo unafanya nini? Tumetoka kwenye nyumba kubwa tunakuja kwenye vyumba viwili?”

“Ndiyo uwezo wetu.”

“Sasa kwa nini tumehama kule?”

“Ile siyo nyumba yetu.”

“Si tulikuwa tumepanga?”

“Na hapa tumepanga.”

“Kama tumepanga huoni tunapoteza fedha bure, si heri tungerudi kwenye nyumba yetu kuliko kuja huku?”

“Hatujapoteza ila yeye ndiye kapoteza.”

MKE WANGU ALISABABISHA NIKAWA MCHAWI

SEHEMU YA 10

“Mume wangu mbona sikuelewi nani kapoteza?”

“Mke wangu, we mkubwa si kila kitu nizungumze unatakiwa kutumia akili.”

“Una maana ile nyumba nilipangiwa na mwanaume?” mke wangu aliuliza macho yamemtoka pima.

“Wewe ndiyo unasema,” nilijifanya sijui kitu. 

“Lakini mume wangu kwa nini unapenda kusikiliza maneno ya watu?”

“Mke wangu tumia akili, utajua sababu gani imetufanya tuhame kule na tusirudi kwenye nyumba yako.”

“Najua tu watu wameshaanza kupenyeza umbea, nina imani nyumba hii muda si mrefu itanishinda.”

“Haiwezi kukushinda kama utanisikiliza.”

“Nikusikilize nini, kila siku unasikiliza maneno ya nje.”

“Kwani uongo?”

“Uongo nini?” mke wangu alishtuka.

“Yote yaliyotokea siku za nyuma?” nilimueleza ya nyuma sikutaka kumueleza niliyoyashuhudia mwenyewe yaliyosababisha nitake kutoka roho.

“Basi mume wangu, lakini kumbuka kusikiliza maneno ya watu tutaachana tunapendana.”

“Unanipenda?” nilimuuliza swali ambalo naamini hata wewe utaona la kijinga. Nilimuuliza kwa makusudi pamoja na kunifanyia yote bado mke wangu niliamini bado ananipenda, nilikuwa nina imani hata yeye ananipenda.

“Nakupenda sana mume wangu.”

“Kweli?”

“Tena sana, hebu nieleze toka tuhame Uswahilini nimekukosea kitu gani kibaya.”

“Hujawahi ila nakuomba iheshimu ndoa yetu,” niliamua kufunika kombe ili mwanaharamu apite kwa kuamini mke wangu hakuwa anajua lolote juu yake.

“Nimekuelewa mume wangu.”

Tulianza maisha mapya kwenye makazi mapya, kama ilivyokuwa kawaida ya mke wangu muda wote alikuwa mpole bila kuonesha mabadiliko yoyote mabaya. Kila nilipokuwa kazini alipoomba ruhusa ya kwenda kwa mama yake nilimkatalia na yeye hakulalamika japokuwa aliona kama nimemnyima uhuru. Nilimueleza yeye ndiye wa kunishawishi kumpa uhuru bila hivyo nilimhakikishia safari yake kubwa ni dukani na sokoni tu.

Mke wangu alionekana kunielewa kwa kufuata yote niliyomueleza, ili kupata uhakika kuna siku nilitoroka kazini na kurudi nyumbani bila taarifa na kumkuta mke wangu kapoa kama maji mtungini. 

Hali ile ilizidi kunijengea imani kwa mke wangu kuwa amebadilika. Nami kidogo mwili ulirudi taratibu na kuonekana mtu mbele ya watu. Japo si tabia nzuri ya kumchunguza mkeo lakini sikuwa na jinsi, siku mojamoja nilimdodosa Simon juu ya tabia ya shemeji yake.

Jibu lilikuwa hata yeye hajasikia lolote baya, hata mtu aliyekuwa akimpa taarifa zile alimweleza sasa hivi kweli mke wangu ametulia. Nilimshukuru Simon rafiki yangu kwa mpango wake uliomrudisha mke wangu kwenye mstari.

Kweli moyo ukipata furaha, hata kama huna kitu maisha utayaona mazuri. Nilipendeza na kuanza kupata kitambi kwa mbali, kila mmoja aliyeniona alinishangaa nilivyopendeza kwa muda mfupi. Niliamini kero za moyo na mateso mazito yanapoutikisa mwili lazima upukutike. 

Siku zilikatika huku nikifurahia maisha, kingine kilichonipa faraja ni kusamehewa deni langu na kampuni kutokana na ufanisi wangu wa kazi uliokuwa umelega na kurudia uwezo wangu wa zamani wa kujituma. 


Waswahili wanasema la kuvunda halina ubani, miezi sita baada ya kubadili makazi yaliyotawaliwa na utulivu na amani, siku moja nilirudi nyumbani majira ya saa moja na nusu usiku kama kawaida baada ya kazi. Nilipofika nilikuta mlango umefungwa, nilikwenda kuuliza kwa jirani chumba cha pili, alinieleza kuwa mke wangu ameondoka katika gari ambalo nilielezwa lilivyo na kuufanya moyo wangu upasuke pah! Lilikuwa ni lile gari la mwanaume aliyekuwa akimzuzua.

Kwa kweli nilichanganyikiwa na kubakia nimesimama kama zuzu, kitu kilichomfanya jirani yangu kunishangaa.

“Kwani vipi shemu, mbona hivyo kuna nini?”

“Hataa,” nilikataa mikono ikiwa kiunoni.

“Hapana shemu nilipokuelekeza gari lililomchukua mkeo umeshtuka na kupoteza hali yako ya kawaida na kutawaliwa na hali ya kutaharuki, kwani lile gari lina nini?”

“Ameondoka saa ngapi?”

“Saa tano asubuhi.”

“Alikueleza anakwenda wapi?” nilimuuliza huku nikiwa na shauku ya kujua.

“Hakuniambia ila aliniletea ufunguo na kunieleza ukirudi nikupe.”

“Na mtoto?”

“Ameondoka naye.”

“Alibeba nini?”

“Alikuwa na mkoba wa kawaida tu.”

“Mmh!” niliguna huku nikiinamisha kichwa na kukitikisa.

“Kwani kuna nini shemeji, mligombana?”

“Jirani si ungesikia?”

“Sasa mbona umeshtuka, msubiri akirudi umuulize, hakukuaga?”

“Asante shemeji,” niliachana na mke wa mpangaji mwenzangu na kuelekea ndani mwangu.

Nilipofika nilijitupa kwenye kochi na kutazama juu huku nikijiuliza yule bwana kampeleka wapi mke wangu. Moyo mwingine uliniambia huenda kapewa lifti tu hakuna kingine, labda amekwenda kwa mama yake. Nilipanga akirudi nisimuulize chochote kuhusiana na kupanda kwenye gari la mwanaume ambaye alionekana shida yake kubwa ni kuivunja nyumba yangu wakati na yeye ana familia yake.

Kupanda gari lile halikuwa tatizo bali kuondoka bila kuaga kama tulivyokubaliana. Kwa upande mwingine sikumlaumu sana mke wangu kutokana na msimamo wangu wa kumkatalia kutoka hata alipoomba ruhusa. Kingine kilichonishangaza kilikuwa kuacha nyumba bila kufanya usafi wa kitu chochote. Vyombo tulivyolia jana yake vilikuwa havijaoshwa, nyumba ilikuwa haijasafishwa, chumbani kitanda kilikuwa hakijatandikwa, mashuka yalikuwa yamekaa ovyo pia hata chakula kilikuwa hakijapikwa.

Nilijiuliza mke wangu atakuwa amepatwa na nini kilichomfanya atoke haraka na kushindwa kufanya majukumu ya ndani. Nilijikuta nikiingiwa na wasiwasi na kuamua kumpigia simu mke wangu, nilijikuta nikizidi kuchanganyikiwa baada ya simu ya mke wangu kutokuwepo hewani. Nilirudia zaidi ya mara kumi lakini jibu lilikuwa lilelile, simu niliyokuwa napiga haikuwepo hewani.


                          Share

Reactions

Chapisha Maoni

0 Maoni

'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();