Hizi Ndizo Hazina Saba (07) Muhimu Katika Maisha Ya Ndoa.
Mtu pekee unayeweza kumbadilisha na kumuongoza kama vile unavyotaka wewe ni wewe mwenyewe na wala siyo mwenza wako au watu wengine. Kama unataka kumpata mtu sahihi wa kuishi naye katika maisha ya ndoa anza kuwa wewe mwenyewe, kuwa mtu sahihi halafu utampata mtu sahihi anayeendana na wewe. Usipoteze muda kumtafuta mtu sahihi wakati wewe mwenyewe siyo sahihi. Usimbadilishe mwenzako wakati wewe mwenyewe hujabadilika hivyo basi, anza kubadilika kwanza wewe na wengine watabadilika.
Watu wengi kabla ya kuingia maisha ya ndoa wanakua na tabia tofauti, kila mtu anakua na tabia yake ambayo anaificha ili mwenzake asiione. Kwa lugha rahisi watu wanapoanza uhusiano wanakua wanavaa maski usoni yaani wanavaa nyuso za bandia. Hapa kila mhusika anakua anaficha makucha yake badala ya kuwa muwazi kwa wenzake. Badala ya kua wazi kwa mwenzako na kuonyesha udhaifu wako kama mwenzako atakupenda kulingana na udhaifu wako wewe unaficha makucha yako na matokeo mnakua mnatengeneza bomu nyie wenyewe na linakuja kuwalipua wakati mnapokua katika maisha ya ndoa.
Kama wewe unalalamika kuwa maisha ya ndoa ni magumu kuna wenzako wanafurahia na kuona maisha ya ndoa ni ya furaha. Kuishi maisha ya furaha katika ndoa ni uamuzi wako wewe mwenyewe wala huhitaji wahisani kutoka nje. Maisha ya furaha katika ndoa unayachagua wewe mwenyewe na maisha ya kutokua na furaha katika maisha ya ndoa unayasababisha wewe mwenyewe.
Mpenzi msomaji, maisha ni furaha na hujazaliwa kuja duniani kuteseka. Una nguvu kubwa sana ya kuchagua kuishi vyovyote unayotaka kuishi katika maisha yako ya ndoa. Mtu pekee anayeweza kuleta furaha katika ndoa yako ni wewe mwenyewe. Usisubiri kupewa ruhusa ndio uanze kuishi maisha ya ndoa yenye furaha, usisubiri ukamilifu katika ndoa yenu ndio muanze kuishi maisha ya furaha bali wakati sahihi wa kuishi maisha ya furaha ni sasa hivi na siyo kesho. Mna kila kitu cha kuwafanya muwe na furaha msiendeshwe na sababu za nje jitoe kulingana na nafasi yako. Kama maisha yenu ya ndoa yanaendeshwa na sababu za nje (external factor) basi, mpo katika hatari ya kuingia shimoni.
Kuna vitu vingi vinavyosababishwa na wanandoa wenyewe kufanya maisha yao kuwa machungu badala ya furaha. Mfano, kulalamika na kulaumiana. Utamaduni wa kulalamika na kulaumiana katika maisha ya ndoa unazaa mtazamo hasi mkubwa sana. Unakuta baba ni mlalamikaji na mama ni mlalamikaji sasa hapo unategemea ndoa kuwa na furaha? Badala ya kulalamika na kulaumiana mnatakiwa kukaa chini na kuchunguza kiini cha tatizo ni nini? Kulalamika na kulaumiana ndio kunafanya ndoa kukosa furaha, amani, upendo n.k. msitupiane mpira katika hili bali kueni watatuzi. Kulalamika na kulaumiana na kila mmoja kuona mwenzake ndio mkosaji na yeye hastahili ndio adui wa furaha yenu. Msilalamike kwani mnapoteza nguvu na muda wenu bure.
Ndugu msomaji, karibu sasa katika kiini cha somo letu la leo ambapo leo tutajifunza hazina saba muhimu katika maisha ya ndoa. Na hazina hizo ni kama ifuatavyo;
1. Kusaidiana; maisha ya ndoa yana hitaji hali ya kusaidiana sana katika shida na raha. Usimpende mwenzako wakati tu akiwa mzima. Mwenzako anapokua na tatizo mtu wa kwanza wa kumsaidia ni mwenza wake. Kama wenzako amepatwa na tatizo vaa viatu vya mwenzako msaidie kutafuta suluhisho la tatizo na siyo kumuacha peke yake. Tabia ya kusaidiana inaleta furaha, faraja katika maisha ya ndoa. Badala ya kugeuka kuwa mwiba kuwa msaada. Onesha hali ya kujali na kumsaidia mwenzako pale anapokua anaumwa, mhudumie kwa ukarimu wa hali ya juu mpaka ahisi anapona. Maisha ya ndoa yako kama biashara na mteja wako mkubwa ni mwenza wako hivyo hakikisha unamhudumia vizuri katika kiwango cha hali ya juu mpaka mteja wako asiwe na wazo la kwenda kutafuta huduma sehemu nyingine. Kama mteja wako unampatia huduma bora na ya uhakika na hakuna kitu anachokosa hawezi kuondoka. Hakikisha unampatia mwenza wako huduma bora. Kwa hiyo, maisha ya ndoa ni kusaidiana unatakiwa kuweka vyeo na nyadhifa mbalimbali ulizonazo kazini kwako na kujishusha na kuwa mnyenyekevu kwa mwenzako.
2. Kutiana moyo; mtu wa kwanza wa kukutia moyo katika jambo Fulani unalofanya ni mwenza wako wa ndoa. Mpe moyo mwenza wako. Kuwa kichocheo cha hamasa katika kile anachofanya. Mwenzako akiwa katika wakati mgumu mtie moyo na kumpa matumaini, muoneshe uko naye bega kwa bega. Kwa namna hii mtafanya ndoa yenu kua na furaha na wala siyo huzuni. Usigeuke kuwa kikwazo kwa mwenzako, bali kuwa mwanga wa kumuonesha njia ya kule anapotaka kwenda. Mpeane maneno ya faraja yenye kutia nguvu, hata kama mko katika wakati mgumu msikate tama, mtie moyo mwenzako. Na habari njema ni kwamba hakuna matatizo ya kudumu katika dunia hii changamoto haikai kwa muda mrefu, inakuja na kuondoka hakuna tatizo la kudumu. Mwenzako anapofanya vizuri unatakiwa kumpongeza katika kila jambo. Usiwe mchoyo wa pongezi kwani kutoa pongezi haina gharama. Hii ndio hazina ya kuifanya ndoa yenu kuwa na furaha.
3. Kusikilizana; Katika hali ya kawaida kusikiliza ni kazi kuliko kuongea. Kila mtu ana haki ya kusikilizwa. Mwache mwenza wako aongee mpaka amalize na wewe kaa kimya wala usimwingilie anapokua anaongea. Hata kama mwenzako hana cha maana cha kuongea wewe muheshimu tu na msikilize kwa unyenyekevu. Msikilize naye ajione anathaminiwa katika hii dunia. Katika maisha ya ndoa kuwa msikilizaji mzuri utafanya ndoa yako kuwa ya furaha. Kuna wengine wanahitaji kusikilizwa lakini hawapati nafasi ya kusikilizwa. Unatakiwa kuonesha ukaribu hata wa kuuliza swali kuonesha kuwa uko karibu naye. Kusikilizana huleta ukaribu wa pamoja.
4. Kukubaliana; katika maisha ya ndoa mnatakiwa kukubaliana kulingana na mapungufu yenu au madhaifu yenu. Kwanza hakuna aliye mkamilifu kwenye kila kitu katika hii dunia. Unatakiwa kumpokea mwenzako jinsi alivyo. Mfundishe pale anapoenda vibaya. Usimhukumu mwenzako kwa sababu ya madhaifu yake. Hakuna aliyekua sahihi kuliko mtu mwingine. Mnatakiwa kuondoa hali za kujiona kuwa wewe unastahili zaidi kuliko mwenzako. Mnatakiwa kuchukuliana madhaifu yenu na kila mmoja aheshimu madhaifu ya mwenzake na siyo vinginevyo.
5. Kuaminiana; uaminifu ni hazina katika maisha ya ndoa. Uaminifu siku hizi umekua adimu sana kwenye kila kitu siyo tu maisha ya ndoa. Kile unachomfanyia mwenzako na wewe utafanyiwa. Unatakiwa kuwa mwaminifu kwa mwenzako na kumuamini mwenzako katika maisha yenu ya ndoa. Kama kuna kitu unakiona kinakosekana katika ndoa yenu kiwekeni wazi badala ya kuacha tatizo kuendelea kuwa tatizo. Kama mwenzako ni mwaminifu unatakiwa kulipa uaminifu. Imekua ni mazoea na kama vile ni fasheni siku hizi watu kuwa na michepuko ndio dili na kusahau kuwa ndoa yako ndio dili hivyo unatakiwa kurudi katika mstari. Uaminifu ni tunda adimu sana linalotafutwa katika maisha ya ndoa. Kila mtu anahitaji uhuru wa kufanya mambo yake hivyo kuwa na uaminifu katika maisha yenu ya ndoa na kila mmoja ampe mwenzake uhuru kwani kama uaminifu upo basi ndio silaha kuu katika ndoa yenu.
6. Kuheshimiana; kila mtu anahitaji kuheshimiwa. Usimdhalilishe mwenzako mbele ya watu kwani ni fedheha kubwa. Unatakiwa kuheshimu kile anachopenda mwenzako na wala usimlazimishe kufanya kile unachopenda wewe kufanya. Kila mtu ana machaguo yake na kuchagua ni maamuzi pia. Kama ukiwa na heshima siku zote utatenda kwa heshima. Unatakiwa kuheshimu mawazo ya mwenzako. Unatakiwa kuheshimu hisia za mwenzako. Usigeuke kuwa mtawala na kumuongoza mwenzako kwenye kila kitu bali unatakiwa kumpa mtu uhuru wa kufanya kile ambacho anapenda ili mradi tu asitoke nje ya utaratibu na kutovunja sheria nyingine za ndoa. Matatizo huanzia pale unapomlazimisha mwenzako kufanya vile unavyotaka wewe.
7. Kuvumiliana na kusameheana; siri ya maisha ya ndoa ni kuvumiliana na kusameheana. Tatizo linapotokea siyo kukimbiliana katika kutalakiana bali mnatakiwa kutatua na kuvumiliana. Kama umekosa uvumilivu katika maisha ya ndoa basi hata safari ya kufikia mafanikio makubwa katika maisha yako itakushinda. Kila kitu kinahitaji uvumilivu. Mwenzako akikukosea mnatakiwa kusameheana na kufutiana hatia iliyo kati yenu na siyo kulipiana visasi. Msamaha unaondoa uchungu ulioumbika katika mioyo yenu na unarudisha mahusiano mapya ya awali.
Kwa hiyo, tunatakiwa kuishi maisha ya furaha kwa kutumia hazina hizi saba tulizojifunza leo. Wanandoa wengi wanakabiliwa na changamoto ya kutoridhishana katika tendo la ndoa. Kuridhishana katika tendo la ndoa ni kushirikishana zawadi ya tunda la ndoa. Kila mlengwa anapaswa kumhudumia mteja wake vizuri ili kuepuka matatizo ya mara kwa mara.
Kwa masomo kama haya na mengine mengi Download App ya MAHABA ipo play store au fuata link hapo chini
https://play.google.com/store/apps/details?id=mahaba.acrt
Pia unaweza kutoa maoni yako hapo chini
Share
0 Maoni