Ticker

6/recent/ticker-posts

SIKUACHI BABY EP 04


 SIKUACHI BABY EP 04


“Najitahidi kukaa nacho moyoni, nisikiseme lakini kuna muda nashindwa, nahisi nahitajika kukisema ila nitakisemea wapi wakati mazingira sio rafiki na licha ya mazingira muhusika mwenyewe anaonekana kutokuwa sawa na mimi,” nilimwambia maneno ya kuuzunguka mmbuyu.
“Sasa unavyoendelea kuzunguka na kunifumba unadhani nitafahamu ni nini kinachokusumbua?” aliniuliza.
“Samira wewe ni mtu mzima najua una akili ya kufikiria baya na zuri. Sitaki kuamini kuwa lugha ya Kiswahili imekutupa mkono na wenda asili yako ni ya Ughaibuni. Sitaki kuamini hilo kabisa,” nilimwambia huku nikiamini  bado hajang’amua lolote nililokuwa namaanisha.
“Metusela hutaki kuniambia au?” aliniuliza kwa sautiya kukata tamaa, alitamani kusikia kile kilichokuwa kikinisumbua lakini kwa muda ule ni kama vile nilikuwa namficha.
“Samira nimetokea kukupenda halafu hata sielewi hisia hizi zimetokea wapi yani nashindwa kuelezea,” nilimwambia huku nikiwa nimejikaza mwili mzima, nilihisi baada ya kumwambia maneno hayo labda angeweza kunitukana nikajipanga kuyakoga matusi kisawasawa.
Nilimsikia akivuta pumzi ndefu na kuziachia, akabaki kuwa kimya cha muda wa sekunde kadhaa, nikahisi labda atakuwa amekata simu, nikaitazama bado alikuwa hewani.
“Samira,” nilimuita.
“Niambie.”
“Mbona umekaa kimya tena huongei?”
“Hapana Metu hivi nikuulize kitu.”
“Yeah! niulize.”
“Hivi umefikiria nini mpaka ukaniambia hivyo.”
“Hakuna nilichokifikiria zaidi ya mapenzi ya dhati niliyokuwa nayo kwako, nimejikuta nikitamani kuwa na wewe, uwe mwanamke wangu wa maisha na nitakupenda siku zote za uhai wa maisha yangu.”
“Metusela.”
“Naam!”
“Sidhani kama itawezekana.”
“Kwanini?”
“Mimi na wewe ni kama dada na kaka halafu isitoshe nina mpenzi wangu japo siishi naye lakini nampenda sitaki kumuumiza.”
“Nahisi nimekukosea nisamehe sana.”
“Usijali Metusela nafahamu kila kitu kuhusu mapenzi, naelewa jinsi hisia zinavyomuingia mtu kwa haraka. Wala hujanikosea, najua ni hisia zimekutuma uniambie hivyo, unastahili kuniambia lolote ila kwa wakati huu umechelewa mimi nina mpenzi wangu tayari.”
“Mpenzi wako ni yupi?”
“Mbona umeniuliza hivyo au unataka kumfahamu?”
“Ndiyo lakini kama itawezekana maana tangu nilipokufahamu sijawahi kukuona ukiwa na mwanaume labda wa kuniambia kila siku mdomoni.”
“Kwa sasa hayupo nchini amesafiri yupo Marekani kikazi.”
“Anafanya kazi gani?”
“Mbona unataka umfahamu sana wewe elewa kuwa yupo kikazi.”
“Sawa nimekuelewa Samira basi acha nilale, nahisi sipo sawa kabisa.”
“Una nini?”
“Nahisi homa halafu natetemeka.”
“Umemeza dawa?”
“Hapana.’
“Kwanini?”
“Sijanunua mpaka kesho Mungu akipenda.”
“Metu ujue unahatari wewe yani unaumwa halafu hununui dawa kweli?”
“Ningefanya nini wakati Muda wote niliutumia kwa ajili yako.”
“Kwa ajili yangu?”
“Ndiyo ila usijali nitakuwa sawa, acha nilale pia nikutakie usiku mwema,” nilimwambia kisha nikakata simu.
Licha ya maumivu niliyoyapata ghafla! baada ya Samira kuniambia alikuwa na mpenzi wake ambaye alikuwa nchini Marekani lakini sikutaka kuamini kama kweli nilimkosa, niliona kushindwa kumfuata kesho yake kwa ajili ya kumpeleka kazini kama ilivyokuwa kawaida yangu, niliutumia uongo wa kuumwa homa ili siku inayofuata nisiende kumchukua. Niliona haya kukutana naye.
Nikamkumbuka Sesilia ambaye ni siku chache zilipita tangu nilipomtukana na kumpa maumivu makali ya mapenzi, nilimkosea sana na kwa kitendo kile kilichokuwa kimenitokea cha kushindwa kumpata Samira nikaanza kumkumbuka.
Akili ikaniambia nichukue simu kisha nimuandikie ujumbe mfupi wa kumuomba msamaha lakini nilishindwa kufanya hivyo. Ni kama vile kulikuwa kuna nafsi inakuja na kuniambia ‘aliyepita amepita mtazame mwingine.’ Nikaghairi na sikutaka kuishika simu tena nikaamua kulala.
****
Niliamka asubuhi ya siku nyingine, nikakutana na ujumbe wa Samira aliyoniandikia kuwa siku hiyo nipumzike, nisiende kumchukua kutokana na kuumwa kwangu, hakuacha kunikumbusha katika ujumbe huohuo aliyonitumia kuwa nisisahau kwenda hospitali kupima kujua ni nini kilichokuwa kikinisumbua. Nilitabasamu baada ya kuusoma ujumbe wake aliyoumalizia na maneno ASUBUHI NJEMA.
Nilishindwa kuelewa kulikuwa kuna kitu gani kilichokuwa kikiendelea, ghafla! Samira alitokea kuwa mtu wa kunijali sana kitendo ambacho sikukitegemea kabisa.
“Unatumia usafiri gani?” nilimtumia ujumbe wa kumuuliza.
“Nitachukua bajaji usijali.”
“Leo unapanda bajaji?”
“Ndiyo sina jinsi itabidi nipande, sitaki nikusumbue Metu unaumwa.”
“Lakini sijazidiwa.”
“Hata kama lakini inabidi upumzike Metu.”
“Sawa.”
“Jioni nikirudi nitakuja kukusalimia ili nijue kama kweli umeenda hospitali na dawa unionyeshe.”
“Sawa karibu,” nilimjibu.
Sikutaka kuumiza kichwa juu ya vipimo na dawa za kumzugia Samira, nilichoamua kukifanya nilimpigia simu rafiki yangu ambaye alikuwa ni daktari, nilimueleza shida yangu na aliahidi kunisaidia.
Nilipomaliza kuweka mambo sawa nilienda kufanya kazi yangu ya bodaboda huku nikiwa makini kutazama muda ambao Samira alikuwa akitoka kazini.
Ilipofika majira ya saa tisa nilirudi nyumbani kwangu, sikupika wala kuandaa chochote zaidi ya kufikiria jinsi ya kumdanganya pindi atakapokuja kuniona. Nikajilaza kitandani.
Baada ya kupita lisaa limoja ghafla! nilisikia mtu akibisha hodi, nilitabasamu baada ya kuisikia sauti ya Samira.
“Karibu,” nilisema kisha nikaenda kufungua mlango.

ITAENDELEA Alhamisi Ijayo

Reactions

Chapisha Maoni

0 Maoni

'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();