Ticker

6/recent/ticker-posts

MKE WANGU ALISABABISHA NIKAWA MCHAWI *26----30* MWISHO

SEHEMU YA *26--------30* mwisho

“Kabla sijatoka nje kaanza kulalamika kichwa kinamuuma kama kinataka kupasuka. Mpaka baba yako anatokwa machozi ujue kashikika kweli. Kichwa kilipoanza kumuuma alikuwa akilalamika, lakini kauli ilikata ghafla kila nikimwita hakufumbua mdogo waka kujigeuza alitulia tu kama unavyomuona,” mama alisema kwa huzuni.
“Mmh! Utakuwa ugonjwa gani unaobadilika kama kinyonga?”
“Ninavyo utazama si wa kawaida yaani kilichotokea ni muda mfupi, lakini mpaka sasa ukimuangalia baba yako kama kaugua wiki nzima.”
Niliiangali hali ya baba kwa kweli ilikuwa mbaya, sikuamini kauli ya mama eti baba kaumwa muda mfupi ndiyo kawa vile. Niliamini ananidanganya kwa vile nimetokea nyumbani ghafla bila taarifa.
“Mama si kweli, inaonekana baba kaumwa muda mrefu, kwa leo tu ndiyo awe hivi? Haiwezekanani ugonjwa wa muda mfupi awe hivi,” sikukubaliana na mama.
“Mwanangu nikudanganye ili iweje? Kawaulize hata majirani kuhusu hali ya baba yako. Wao nao hawajui kama yupo kwenye hali hii. Nina imani wakimwona hataamini. Mwanangu hiki ni kitu cha kunishangaza sana.”
“Sawa mama nimekuelewa, basi tumuwahishe baba hospitali.”
“Ngoja nikamwite rafiki yake baba Pasko akusaidie, mimi hata nguvu sina,” mama alionekana amechanganywa na ugonjwa wa baba.
“Basi mama wahi.”
Baada ya mama kutoka nje, nilimsogelea baba na kuushangaa uso wake ulikuwa umekonda na midomo kumkauka. Hali ile ilionesha baba hakuumwa muda mfupi kama mama alivyosema. Niliamini alikuwa akiumwa kawaida ila siku ile ndiyo alizidiwa sana. Nilimwita baba aliyekuwa amekata kauli kwa sauti ya chini.
“Baba..baba..amka, mimi Kazala mwanao nipo hapa,” lakini baba hakunyanyua mdomo wala kukapua macho.
Nilijiuliza baba yangu anaumwa nini mpaka kuwa katika hali kama ile. Mama alirudi na mzee Samweli baba Pasko na kuingia ndani.
Mzee Samweli alipomuona alishtuka na kuhoji.
“Jamani mzee mwenzangu kapatwa na nini?”
“Kama nilivyokueleza,” mama alimjibu mzee Samweli, kwa vile mimi nilikuwa sijui chochote juu ya ugonjwa wa baba.
“Ha! Kazala umekuja saa ngapi baba?”
“Hata dakika tano sina nimefika na kukutana na hali hii, shikamoo baba.”
“Marahaba, Jamani si nimepita nimewaacha mnazungumza hapo nje?” Ilionesha mzee Samweli naye alishtuka sana kuiona hali ya baba ilivyokuwa.
“Kama nilivyokueleza,” mama alijibu akiwa amejikunyata kwa hofu ya ugonjwa wa baba.
“Mama, baba alikuwa akiumwa kabla ya leo?” nilijikuta nikimuuliza mama swali la awali ambalo jibu lake sikukubaliana nalo.
“Mwanangu muulize hata baba Pasko kama baba yako alikuwa akiumwa hata kidole.”
“Kazala baba yako alikuwa mzima wa afya njema, asubuhi tulikwenda wote kwenye kahawa na kurudi. Baada ya muda nilipita nikielekea ofisini kulikuwa na kikao cha kata, wakati wa kurudi nimewakuta mama na baba yako wapo nje mama yako akiosha vyombo na baba yako akisoma gazeti na kumuomba akimaliza kusoma aniazime. Nashangaa kuelezwa anaumwa tena amekata kauli na kushangaa zaidi kuonekana kama ameumwa muda mrefu,” kauli ya mzee Samweli ilinishtua sana.
“Sasa hii itakuwa nini?” niliuliza baada ya kuchanganywa na taarifa ile.
“Tumwahishe kwanza hospitali tu,” mzee Samweli alitoa wazo.
Nilitoka kwenda kufungua gari kisha nilirudi ndani kusaidiana na mzee Samwel kumbeba baba kumpeleka nje kwenye gari. Baada ya kumweka vizuri kwa kumlaza kwenye miguu ya mama,  nililiondoa gari kuelekea hospitali. Mzee Samweli alitusindikiza.
Sikutaka kwenda hospitali ya wilaya niliamua kwenda moja kwa moja hospitali ya taifa, ambako kulikuwa na rafiki yangu aliyekuwa mkoani na baadaye kuhamishiwa hospitali ya rufaa.
Tukiwa njiani alisikia baba akikoroma kwa muda kisha alivuta mkoromo mrefu na kutulia. Hali ile ilinishtua na kunifanya nimuulize mama.
“Mama vipi tena?”
“Hakuna tatizo, twende tu.”
Niliendesha gari kwa kasi, kidogo nipate ajali lakini nilimshukuru Mungu nilifika salama. Nilipofika tulichukua kitanda haraka na kuja kumchukua baba aliyekuwa amelegea sana. Nilishtuka kumuona mama akizidi kutokwa na machozi. Nilijua ni kutokana na uchungu wa ugonjwa wa ghafla wa baba. Baada ya kufanikiwa kumlaza kwenye kitanda cha mataili, tulimuingiza moja kwa  moja kwa daktari hata bila kukata cheti.
Daktari aliacha kazi zote na kumuhudumia baba  ambaye ilionesha wazi yupo mahututi. Baada ya kumwagalia huku akimpima kwa kumminya baadhi ya sehemu ya mwili. Baada ya muda aliomba wote tutoke nje, wote tulitii amri na kutoka nje kumuacha daktari afanye kazi  yake.
Kilichokuwa kikinishangaza machozi ya mama yaliyokuwa yakiendelea kububujika, pamoja nami kuwa na uchungu nilijikaza huku nikimuombea kwa Mungu.
“Mama usilie baba atapona tu,” nilimsogelea mama kumliwaza.
“Tumuombe Mungu lakini...” mama hakumalizia alinamisha kichwa chini na kuendelea kumwaga machozi na kunifanya nizidi kuwa katika wakati mgumu.
“Mama nini? Baba atapona tu.”
Baada ya muda daktari alitoka na kuuliza:
“Nani muhusika wa mgonjwa?”
“Wote, mimi mtoto na huyu ni mama yangu mke wa mgonjwa,” nilijibu mimi.
“Basi nakuomba wewe ndani mara moja.”
“Mimi,” niliuliza huku nikijishika kifuani.
“Ndiyo.”
Niliingia chumba cha daktari ambako baba alikuwa amelazwa kwenye kitanda kilichokuwa kimezungushwa pazia za kijani. Baada ya kuingia ofisini nilikaribishwa kwenye kiti na kutulia kwa muda huku daktari akiandika kwenye karatasi.
“Samahani ndugu yangu, mzee anaitwa nani?”
“Hasani Kazala.”
“Mzee ameumwa kwa muda gani?”
“Kwa maelezo ya mama,  saa moja iliyopita alikuwa haumwi kitu chochote.”
“Wewe unakaa wapi?”
“Mkoani.”
“Umefika lini?”
“Kama robo saa iliyopita na kukuta hali ya baba imebadilika nusu saa iliyopita.”
“Una ndugu zako?”
“Nipo peke yangu kama roho kwa wazazi wangu.”
“Kwa vile wewe ndiye kichwa na mwanaume nataka kukueleza ukweli kuhusu hali ya baba yako,” daktari alinyamaza na kuvuta pumzi na kunifanya nimtazame usoni.
“Wewe mwanaume, baba yako amefariki.”
“Eti baba kafanya nini?” nilishtuka kidogo nianguke kwenye kiti.
“Jikaze ndugu yangu, wewe mtoto wa kiume kwani unatakiwa kumpoza mama ambaye anakutegemea.”
“Daktari kweli baba amekufa?” niliuliza kama sikumsikia mwanzo.
“Kitambo, mmemleta hapa akiwa tayari ameisha kata roho.”

 MKE WANGU ALISABABISHA NIKAWA MCHAWI 

SEHEMU YA 27

“Nini kimemuua?” nilimuuliza huku nikijifuta jasho la mshtuko.

“Kwa kweli mpaka tumfanyie uchunguzi wa kitaalamu.”
“Mmh! Sawa.”
“Basi mweleze mama vizuri ili asipate mshtuko.”
“Sawa nimekuelewa, japokuwa najua ni kazi kumweleza bila kupata mshtuko.”
“Jitahidi wewe ndiye unayetegemewa kwa sasa baada ya baba yako,” maneno ya daktari yalinijaza nguvu.
Nilitoka hadi nje huku nikijikaza kiume ili kuhakikisha mama namweleza kwa utaratibu ili asipatwe na mshtuko. Pamoja na kujikaza moyoni nilikuwa na uchungu wa kumpoteza baba yangu kipenzi. Nilikwenda kumweleza mama hali halisi iliyokuwa ndani.
Nilishangaa kumkuta mama ameinama kwenye kifua cha mzee Samweli kuonesha anabembelezwa.
“Mama..mama,” nilimwita huku nikijitahidi kuficha maumivu makali moyoni.
“Kazala mwanangu kuna mabadiliko?” mama aliniuliza huku akinitazama macho yake yalikuwa yamejaa machozi.
“Ya nini mama?”
“Ya hali ya baba yako.”
“Mama..ba.b..,”
“Kazala najua.. najua kila kitu najua mwanangu, nilichokiona najua ndicho ulichokutana nacho ndani, pole mwanangu,” kauli ya mama ilinishtua na kujiuliza anamaanisha nini.
“Kipi mama?”
“Hakuna chochote naijua hali ya baba yako ndiyo maana mwanangu unatokwa na machozi.”
“Ma..ma.m.ma,” kauli ya mama ilinifanya nishindwe kuzungumza na kuhisi maumivu upya.
Nilikumbatiana na mama kila mtu alitokwa na machozi tulilia kilio cha kimyakimya.
“Jamani najua tumeumia wote, lakini muda huu tunatakiwa tujue marehemu wetu tunamhifadhi vipi?” mzee Samweli alisema.
“Wanataka kumfanyia uchunguzi ili kujua kifo chake kimetokana na nini?” nilijibu huku nikiachiana na mama.
“Hapana mwanangu baba yako alikataa kumlaza mochwali au kufanyiwa  uchunguzi wa kifo chake. Aliwahi kusema akifa azikwe tu, kwa vile kila mwanadamu kifo ni haki yake.”
“Mama ni ghafla sana, lazima tujue sababu ya kifo chake.”
“Ukijua ndiyo utamrudisha duniani?” mama aliniuliza swali akiwa amenikazia macho yaliyojaa machozi.
“Hapana mama, ila ni muhimu kujua.”
“Siwezi kwenda kinyume na agizo la baba yako, hata mimi mama yako nikifa nizikwe siku hiyohiyo sitaki kilazwa kwenye mafriji au kufanyiwa uchunguzi wa kifo changu.”
“Sasa tutafanyaje ukiwa amefariki muda huu? Hatuwezi kumzika leo, lazima tuwataarifu ndugu na jamaa, mazishi lazima yawe kesho.”
“Hilo halina tatizo.”
“Sasa mwili wa baba tutaufanya nini?”
“Tunatakiwa tuuchukue leo ukalale nyumbani ili uzikwe kesho.”
“Sawa mama,” nilikubaliana na mama.
Tuliingia chumba cha daktari ambako mwili wa baba ulikuwa umelazwa kwenye kitanda na kuzungushiwa pazia za kijani. Tulitaka kuutengeneza kabla ya kumchukua. Wote watatu tulisogea kwenye kitanda kilichokuwa na mwili wa baba.
Kitu kilicho tushangaza wote kilikuwa uso wa baba kuwa katika hali ya kawaida. Uso wake haukuwa na mkunjo wowote, haukuwa uso uliokonda alikuwa yuleyule baba yangu ninaye mtambua.
Hali ile ilitufanya tutazamane, mzee Samweli hakuvumilia alisema.
“Hapana hii mpya, sijawahi kuona mgonjwa akonde akifa anenepe.”
“Hata mimi nashangaa!” mama alisema.
“Hapa si bure, kuna sababu,” nilichangia.
“Wee! Koma, maneno gani hayo,” mama alinikomesha, siku zote hakuamini ushirikina aliuita mambo ya kishenzi.
“Mama hii si hali ya kuiacha ipite hivihivi, lazima kuna kitu baba kafanyiwa kama ameugua kwa muda mfupi na kukonda uso na kufa kisha kurudi kwenye hali ya kawaida, hata ukikataa kuna kitu.”
“Kazala achana na  mawazo ya kijinga, baba yako amekufa tumzike na tumuombee kwa Mungu.”
“Sawa mama,” nilikuba kishingo upande.    
Baada ya taratibu zote za kuustiri mwili wa baba na kuchukua kalatasi ya taarifa ya kifo. Tuliuchukua mwili wa baba kwa kukodi pick up. Mama na mzee Samweli walitangulia na mwili wa baba mimi niliondoka na gari nililokuja nalo.
Njiani roho iliniuma sana baba yangu kushindwa kuiona nyumba yangu, heri angeingia hata mara moja kwenye nyumba yangu, ambayo ndiyo niliiandaa kwa ajili ya kuwalea wazazi wangu.
Lakini nilichopanga kilienda tofauti, niliumia sana tena sana kumpoteza baba yangu aliyekuwa mtu muhimu sana kwenye maisha yangu. Ndiye aliyekuwa taa na dira yangu, siku zote alinipa nguvu sehemu niliyokata tamaa na kujiona ninacho hata kama sina.
Bado nilitakiwa kumshukuru Mungu kuniachia mama yangu ambaye niliamini ndiye nitaye ekeza nguvu zangu zote kwake baada ya kumpoteza baba kipenzi.
Kingine kilichonipa wakati mgumu wa taarifa ya ugonjwa wa baba wa kuugua ghafla kisha kukonda kama mtu aliyeugua kipindi kirefu na baada ya kufa, uso wake kurudi kwenye hali ya kawaida.
Kwangu mimi nilijua ule ni mchezo nimechezewa bila kujua nimechezewa na nani. Roho iliniuma sana kufariki kwa mzee Kidereko kwangu ningejua kila kitu.  Moyoni mwangu sikumuafikiri mama kukubali kirahisi kiasi kile, ingekuwa mimi, mwili wa baba nisingeuzika haraka ungekaa hata mwaka mzima mochwali ili nipate uhakika wa kifo chake. Niliamini kifo kile hakikuwa cha kawaida na pengine baba yangu hakufa aligeuzwa msukule.
Nilipanga baada msiba kwisha nisafiri kuchunguza kifo cha baba ambacho kwa upande wangu sikukubaliana nacho.
                                  ****
Siku ya pili tulimzika baba, msiba ulioudhuliwa na watu wengi sana, wafanyakazi wenzangu walikuwa miongoni mwa watu waliokuja kumzika baba yangu na kunipa faraja kubwa. Msibani kulikuwa na minong’ono ya chinichini ikisema, msiba ule si bure lazima kutakuwa na mkono wa mtu. Mama hakukubaliana na minong’ono ile kwa kuamini kifo cha baba pamoja na vitu vya kushangaza  kutokea bado aliamini ni amri ya Mungu.
Baada ya mazishi na kukaa siku mbili nilimuomba mama niondoke naye ili tukamalizie msiba nyumbani kwangu. Lakini mama alikataa na kusema msiba ataumalizia palepale nyumbani kwake. Sikuwa na jinsi kwa vile alikuwa ameamua ilibidi niiache familia yangu ikae na mama kipindi chote cha mama kumaliza msiba wa baba.
Wiki moja ilikatika na muda wa kurudi kazini ulifika. Nilirudi zangu kwangu na kumwacha mke wangu amtunze mama kwa kipindi chote cha kumalizia msiba wa baba. Nilirudi zangu nyumbani siku ya jumapili na jumatatu asubuhi nilikwenda kazini. Nilianza kazi nikiwa bado na kitendawili kizito kichwani mwangu kutokana na kifo cha baba. Pamoja na mama kusema kifo cha baba ni amri ya Mungu sikutaka kukubaliana naye japokuwa nilimkubalia ili kumlizisha. Nilipanga siku ya Ijumaa niondoke na gari la kampuni kwenda Malalo. Niliamini hata kama nitalala Tewe siku ile na kesho yake lakini siku ya jumapili. Lazima niwe nimerudi kwa muda wowote ili mradi jumatatu inikute kazini.
Wiki nzima niliyokuwa kazini nilikuwa katika dimbwi la mawazo kuhusiana na mazingira ya kifo cha baba yangu. Wengi walijua kukosa kwangu raha kazini kulitokana na maumivu ya kifo cha baba yangu, ambaye siku zote alikuwa mtu wangu wa karibu. Japokuwa kifo cha baba kiliniuma sana kutokana na kipindi kile ndicho nilikuwa nikiwahitaji sana wazazi wangu kula jasho langu. Kilichonichanganya zaidi na kuupa moyo wangu wasiwasi kilikuwa mazingira ya kifo cha baba. Niliamini utatuzi wake ningeupata kwa mtoto wa mzee Kidereko. Bado safari yangu ilibakia siri yangu sikutaka kumshirikisha mtu yeyote.
Mwisho wa wiki niliomba gari kama nakwenda kumuona mama. Kwa vile nilikuwa naivana na bosi, alinikubalia niondoke na gari. Siku ya ijumaa niliondoka kazini saa tano asubuhi, watu wote walijua nimekwenda kumuona mama.
Niliondoka kazini saa tano na nusu, nilitumia saa mbili na nusu kufika Chalinze kutoka na mwendo kasi niliokuwa nikitembea nao. Niliunganisha moja kwa moja kuelekea Lushoto. Kwa mwendo niliokuwa nakwenda nilifika Tewe saa kumi na mbili jioni. Nilikuta bado mwanga wa jua bado haujazama vizuri na kuamini mambo yangu kama yatafanikiwa yatakwenda vizuri ningeweza kurudi siku ileile na kuelekea kwa mama kisha ningerudi kazini.
Ugeni wangu wa ghafla uliwashtua, baada ya kunipokea walitaka kujua ujaji wangu wa siku ile.
Kwa vile muda ulikuwa bado nilipata muda wa kuzungumza na mtoto wa mzee Kidereko. Palepale nje chini ya mti, wote walitupisha kutuacha tuzungumze wawili.
“Ndiyo ndugu zangu za siku?” mtoto wa mzee Kidereko aliniuliza.
“Nzuri kiasi,” nilimjibu huku nikimtaza na kukutanisha macho yalionesha anashauku ya kujua kilichonipeleka pale.
“Hata mimi ujaji wako umenionesha kuna kitu, ehe, ndugu yangu tatizo nini?”
Nilimuelezea utata wa mazingira ya kifo cha baba yangu. Baada ya kunisikiliza alimwita msaidizi wake, alimwita kijana mmoja kati ya wasaidizi wa baba yake mzee Kidereko.
“Hamis njoo.”
“Naam.”
“Niletee unga wa kutazamia mbali.”
Juma alikwenda ndani na kurudi na chupa ndogo aliyomkabidhi. Baada ya kumkabidhi alifungua chupa na kujimiminia unga mweupe mkononi. Kisha aliumwaga kwa kuusambaza na kutulia kuutazama ule unga aliopeperuka kwa upepo.
Aliutazama ule unga uliokuwa ukipepea kwa upepo kama anaangalia kitu ambacho mimi sikukiona. Baada ya kutulia kwa muda alishusha pumzi ndefu na kusema:
“Kuna vita nzito sana.”
“Vita?” nilishtuka kusikia vile.
“Tena nzito, mmh! Kuna kazi!”
“Kazi?” nilizidi kushtuka na maneno ya mganga.
“Tena nzito, hii kwangu.mmh, sijui!” mganga alinikatisha tamaa bila kujua hiyo ni vita gani na uzito wake ni upi.
“Mbona unanitisha?”
“Sikutishi, ndiyo ukweli wenyewe, vita hii ingenoga mzee angekuwepo.”
“Una maana gani?”
“Kifo cha baba yako kina siri nzito.”
“Mganga hebu nieleze tatizo kuliko kunizungusha na kunitisha.”
“Inaonesha hapa kifo cha baba yako kimetokana kisasi.”
“Kisasi?” nilishtuka.
“Ndiyo.”
“Kisasi kipi tena?”
“Baada ya kifo cha mgoni wako wa pili, ndugu zake hawakukubali kama kile kifo cha amri ya Mungu. Kutokana na mazingira ya kifo chake, aliamua kukifanyia uchuguzi ndipo walipo kukuta. Hawakukubali kumpoteza ndugu yao, waliamua kulipa kisasi.
“Inavyoonekana waganga wengi wa nchini wamechemsha hivyo wakaamua kutoka nje ya nchi kuhakikisha wanakulambisha mchanga. Inaonesha uchawi waliotumia kukuroga umetoka mbali sana.
“Naweza kusema mshukuru sana mzee Kidereko kwa kinga aliyokupa. Uchawi waliotumia tungekuwa tumekwisha kukuzika muda mrefu. Unakumbuka siku moja ukiwa kazini uliumwa sana kichwa kisha ulitoka damu puani?”
“Ndiyo nakumbuka.”
Nilikumbuka siku moja ambayo nina imani katika kusimulia sikulisema hili.  Ni kweli siku moja nikiwa kazini baada ya kazi ya kutoa vifaa ambayo vilikuwa vingi na kunifanya nisimame kwa muda mrefu.
“Nilipokaa kichwa kilianza kuniuma kama kinapasuka kikifuatiwa na kutokwa damu nyingi puani.
Nilikimbizwa hospitali ambako nilikutwa na maralia. Baada ya matibabu nilijisikia vizuri na kuruhusiwa kutoka hospitali. Hali ile haikujirudia tena na kuamini yale yalikuwa maralia tu.
“Basi yale hayakuwa maralia ilikuwa ndiyo safari, shukuru kupelekwa kwenye mizimu, uchawi uliofanyiwa mbaya sana. Kutoka damu puani ilikuwa safari isiyo na kwaheri. Lile lilikuwa jini la kutumwa, jini Makata lilikuwa likukate palepale.

 MKE WANGU ALISABABISHA NIKAWA MCHAWI 

SEHEMU YA 28

“Baada ya kuona kwako ngoma nzito walibadilisha mashambulizi na kuyaelekeza kwenye familia yako. Wameanza na baba yako baada ya hapo atatafutwa mtu mwingine.”
“He! Ina maana wamepanga kuiteketeza familia yangu yote?” nilishtuka kusikia vile.
“Ndiyo.”
“Wanatumia uchawi wa ndizi, wanaroga kwenye mkungu wa ndizi wenye ndizi mbichi, ikiiva  ndizi moja na kundoka, basi katika familia yako anaondoka mtu mmoja.”
“Mungu wangu!” nilishika kichwa kwa mshtuko.
“Mtego wao haukuwasumbua kukunasa kwa vile kilikuwa kisasi cha kuuawa ndugu yao, hivyo ilikuwa rahisi kukupata.”
“Sasa utanisaidiaje?”
“Kazi hii kwa uwezo wangu nzito sana, ila nitakuelekeza kwa mzee mmoja ambaye alikuwa swahiba wa  baba ambaye naye yupo vizuri kama mzee Kidereko.”
“Anakaa wapi?”
“Maeneo ya mbele kidogo japo kuna kamwendo kadogo.”
“Tunaweza kwenda leo?”
“Tunaweza kwa vile muda bado.”
“Tunaweza kutumia gari?”
“Hatuwezi kwenda na gari kutokana na eneo lenyewe, lazima tupande kilima na kushuka.”
“Usiku hakuna wanyama wakali?”
“Hakuna.”
Tulikubalia kwenda kwa mganga mwingine baada ya ngoma yangu kuwa nzito kwake. Tuliongozana wawili kuelekea kwa mganga, ilikuwa safari ya kupanda na kushuka milima mpaka kufika kwa mganga nikiwa nimechoka na kutokwa na jasho chapachapa.
Toka nilipouachia mwili nilikuwa mzembe, safari na nusu saa ilikuwa kama nimetembea zaidi ya saa sita.  Tulipofika kwanza nilikaa chini kupumua, kwani hata kuongea nilishindwa kutokana na kifua kujaa pumzi.
Mtoto wa mzee Kidereko aliniacha nimepumzika kwenye gogo la mnazi na yeye kuingia ndani kwa mganga. Ilionesha pale ni mwenyeji kwa jinsi walivyo mpokea.
Nilitulia kwenye gogo huku giza likianza kuimeza nuru ya mchana. Baada ya muda alirudi na kunieleza jambo ambalo lilinishtua kidogo.
“Ndugu yangu tumefeli.”
“Una maana gani?”
“Mzee amekwenda mkoani, kuna watu wamemchukua jana.”
“Atarudi lini?”
“Mmh! Haijulikani.”
“Kwani ndiyo mara yake ya kwanza kusafiri kikazi?”
“Mara nyingi, huwa akiondoka kwenda kufanya kazi za watu mikoani, anaweza kumaliza hata mwezi mzima.”
“Mmh! Sasa itakuwaje, hana msaidizi?”
“Yupo, lakini kazi yako si ya kutumwa mtu mwepesi, unaweza kumpoteza kama mchezo.”
“Kwani ni nzito sana?”
“Hauna tofauti na uliyosababisha ugonjwa kwa baba uliopelekea sababu ya mauti yake.”
“Mmh! Sasa nitafanyaje, hakuna waganga wengine?”
“Kwa kweli mimi niliyekuleta kwake ndiye niliyekuwa naye karibu pia nina mahusiano mazuri. Hata kazi zao walikuwa wakisaidiana na marehemu baba.”
“Uliniambia uchawi wao ni wa ndizi, kwa hiyo kuna mkungu unaendelea kuiva?”
“Ndiyo, tena uchawi huu ni mbaya sana unaweza kumaliza ukoo wako kwa muda mfupi.”
“Mungu wangu sasa nitafanya nini ikiwa hakuna mtu wa kunisaidia?” nilijikuta nazidi kuchanganyikiwa.
“Mmh! Hebu turudi nyumbani nataka nikajaribu kutafuta ufumbuzi,” mtoto wa mzee Kidereko aliniambia.
“Ukishindwa?”
“Tumuombe Mungu nisishindwe, shida yangu ni kuzuia, kwani ukifanya mzaha wiki nzima unaweza kuzika familia nzima.”
“Eti?” kauli ile ilizidi kunitisha.
“Uchawi waliotumia ni mbaya sana, ule haubakizi ukoo.”
Tukiwa katika ya mazungumzo alitoka kijana mmoja aliyeonekana amevalia nguo za kiganga na kunisalimia.
“Za saizi kaka?”
“Nzuri.”
“Pole sana, nimefuatilia mazungumzo yako na maneno aliyoniambia Maghinde kwa kweli yamenishtua. Wakati nyinyi mkizungumza, niliangalia tatizo lako. Kwa kweli ni vita nzito sana.”
“Jamani badala ya kunisaidia mnazidi kunikata maini,” nilitamani kulia na kuiona kama dunia imeniinamia na hakuna wa kunipa msaada.
“Nia kubwa ni kukusaidia, kuna kitu nimekiona kimenitisha sana.”
“Mungu wangu kitu gani tena hicho?” kauli ya Bwaza ilizidi kunitia hofu.
“Hebu twendeni kwanza ndani, hili si jambo la kulizungumza hapa.”
Tuliongozana ndani huku nikihisi mwili kupoteza nguvu, moyoni nilijuta kujiingiza kwenye vita ya ushirikina. Moyo wangu uliingia hofu ya kupoteza familia yangu yote kutokana na maelezo ya uchawi wa ndizi unavyoua watu kwa mpigo.
Baada ya kuingia ndani alichukua unga kama alivyofanya Maghinde mtoto wa mzee Kidereko. Baada ya muda alisema:
“Kama ulivyoambiwa vita hii ni nzito, hali inavyojionesha ni mbaya sana upande wako. Inaonesha wiki hii na ijayo lazima upande watu watatu.”
“Watu watatu?”
“Ndiyo, hapa panaonesha ndizi tatu zimeiva tayari zinaweza kuanguka wakati wowote.”
“Ndiziii?”
“Ndiyo, inaonekana imedondoka moja ambayo ni baba yako. Zilizobaki zitadondoka wakati wowote ila moja itadondoka wakati wowote kuanzia sasa.”
“Mungu, sasa nitafanyaje jamani, ina maana na mama anakufa?”
“Hatujajua ila wakati wowote tegemea kupata taarifa za kukushtua.”
“Jamani mbona imekuwa hivi?”
“Mzee angekuwepo nina imani kila kitu kingekwenda vizuri.”
“Jamani mtanisaidiaje, Mungu wangu ina maana na mama nampoteza?” nilianza kulia kwa uchungu.
Mara simu yangu iliita, nilipoangalia ilionesha inatoka kwa mke wangu. Moyo ulinilipuka na jasho kunitoka, moyoni niliomba jisipokee habari mbaya. Niliipokea huku nikiuliza kwanza hali ya mama kabla ya salam.
“Haloo mke wangu, mama anaendeleaje?”
“Anaendelea vizuri, ndiye uliyemuacha peke yake huku nyumbani?”
“Nisamehe mke wangu, za huko watoto hawajambo?”
“Mwanao mdogo ndiye anaumwa hapa tupo hospitali tumepewa kitanda.”
“Nini zaidi?”
“Anachemka sana na kuhema kwa shida.”
“Hali hiyo imeanza lini?”
“Hebu subiri kwanza..” mke wangu alisema upande wa pili huku akikata simu.
Nilikata simu kusubiri maelezo ya mke wangu.
“Vipi?” Maghinde aliniuliza.
“Mke wangu anasema mtoto ameumwa ghafla ila mama hajambo.”
“Ameumwa ghafla yupo wapi?”
“Hospital.”
Kauli yangu ilifanya wote watazamane kisha walishusha pumzi nzito. Kitendo kile kilinishtua sana na kujiuliza kulikoni kufanya vile.
“Kazala, hapa panaonesha ndizi tatu zimeiva ila moja tayari imedondoka.”
“Sijakuelewa si unasema zimeiva ndizi tatu na moja imedondoka?”
“Ndiyo, katika zile ndizi tatu kuna moja imedondoka na kufanya upoteze watu wawili mpaka sasa.”
“Mungu wangu mnataka kuniambia tofauti na baba kuna mtu amekufa?”
“Tena sasa hivi,” Bwaza alinijibu kwa sauti ya upole.
“U...u..nataka ku..kuni..”
Nilikatishwa kauli na sauti ya mlio wa simu yangu, nilinyamaza na kuangalia simu ilikuwa ya mke wangu. Huku mapigo ya moyo yakinienda mbio nilipokea.
“Haloo mke wangu.”
“Mume wangu...maskini mwanangu,” ilikuwa sauti ya kilio ya mke wangu kuonesha mambo yameharibika.
“Mtoto kafanya nini?” niliuliza pumzi zikiwa juu.
“Ame...me..fariki.”
Nilipatwa na mshtuko na kujikuta napoteza fahamu, nilipozinduka nilijikuta nimelazwa nje kwenye mkeka huku nikipigwa na baridi kali. Muda huo kiza kilikuwa kimeingia ila mwezi ulikuwa ukiangaza. Pembeni yangu alikuwepo Maghinde na Bwaza.
“Kazala,” Maghinde aliniita.
“Naam,”
“Msikilize Bwaza kuna kitu anataka kukuambia cha muhimu sana.”
“Jamani naomba niondoke usiku huu nirudi nyumbani,” kwa kweli baada ya kupata fahamu sikutaka kitu kingine zaidi ya kurudi nyumbani usiku ule kuwahi msiba wa mwanangu.
“Sasa kama ulijua hivyo, huku umekuja kufanya nini?”
“Nilichokifuata sijakipata mnafikiri nifanye nini zaidi ya kurudi kusubiri tufe wote,” kwa kweli nilikuwa nimekata tamaa kwa kauli niliyoambiwa na kilichokuwa kikiendelea.
“Sikiliza Kazala ndiyo maana kikakwambia msikilize Bwaza kuna kitu anataka kukueleza.”
“Haya nieleze mbona mwaka huu nitakoma.”
“Ni hivi bwana Kazala, kweli kama tulivyokueleza hali ni mbaya na ndizi kweli zimeonesha zimeiva na moja imeisha dondoka muda mfupi na zingine mbili zitafuata. Katika kuangalia inaonesha nguvu zinazo kulinda wewe ni za mizimu na majini ya mti mkuu.
“Naamini kabisa majini na mizimu inakutambua, nina imani kilio chako mbele yao kitaweza kukulinda na balaa linalokuja mbele.”
“Sasa jamani, nitawezaje kwenda kwenye mizimu na kuwahi mazishi ya mwanangu?”
“Tulichokipanga tutaondoka usiku huuhuu hadi kwenye mti wa mizimu na mbuzi mwekundu na mweupe na vitu vingine tutakusaidia kuvitafuta ili kutoa sadaka itakayokusaidia kupata msaada wa haraka wa mizimu na majini.”
“Jamani hao mbuzi usiku huu nitawatoa wapi?”
“Wewe utatoa fedha kila kitu tumekipanga wakati tukikusughulikia ulipoanguka.”
“Kwa hiyo shilingi ngapi mbuzi wote?”
Walinitajia fedha ya mbuzi wote, kwa vile nilikuwa nayo niliwapa. Hatukupoteza muda tuliwachukua wale mbuzi wawili na baadhi ya vitu wanavyojua wao kwa kazi yangu na kuelekea porini. Tulitembea kwa saa mbili mpaka kufika kwenye mizimu.
Tilipofika pale Bwaza msaidizi wa mganga rafiki wa mzee Kidereko alifanya kama alivyofanya mzee Kidereko siku aliponipeleka pale enzi ya uhai wake.
Alichukua maji yaliyokuwa kwenye chupa na kuyaweka mdomoni kisha aliyapuliza kuelekea kwenye ule mti mkubwa. Baada ya kumaliza zoezi lile alichukua unga wa dawa na kuurusha sehemu nne za dunia na kusema kwa sauti.
“Hodi mizimu.. hodi majini yote kuanzia Kibwengo na majini yote katika mti huu..hodi tumekuja kutaka msaada wenu.. tunajua ninyi mna nguvu, mizimu yote na majini tupokeeni mtusaidie shida zetu,” Baada ya kusema maneno yale ulifuatia muungurumo ambao haukudumu muda mrefu ulinyamaza pia haukuwa na tofauti na mwanzo nilipokuja kwa mara ya kwanza Kidereko 

 MKE WANGU ALISABABISHA NIKAWA MCHAWI

SEHEMU YA 30

                                   ****
Mwezi mmoja baada ya kifo cha mwanangu, katika kuulizia sehemu gani kuwa waganga wakali. Jamaa yangu mmoja pale kazini aliyekuwa dereva wa magari makubwa aliyeaminika kwa ushirikina, ambaye alijiamini sana hata alipofanya makosa hakufukuzwa kazi. Nilimfuata na kumuuliza jeuri ile anaipata wapi. 
“Kazala maisha kuangaika, nimeteseka sana, walimwengu si watu. Haki yangu mwenyewe ilinifanya nipoteze mke na watoto,” Kanyenye alinieleza kwa majonzi.
“Haki yako ipi na tukio hilo limetokea lini?”
“Miaka saba iliyopita ilikuwa miaka miwili kabla ya wewe kuja kufanya kazi hapa. Baada ya kupata kazi nilidunduliza vijisenti ambavyo nilipeleka  kijijini kwetu kununua shamba. Nilifanikiwa kununua shamba ambalo nilikodisha  watu kunilimia. Baada ya muda nililetewa taarifa kuwa jirani yangu kaingia eneo langu.
“Nilifunga safari hadi kijijini kuonana na jirani yangu, jamaa alikuwa kama alikuwa ananitafuta. Baada ya kufikishana serikali ya kijiji na kumshinda, aliapa kunionesha. Baada ya muda nilianza kuandamwa na mabalaa magonjwa vifo vya mke na wanangu kwa mpigo.
“Huwezi kuamini nimezika watu watatu kwa mpigo, vifo vyao vilipishana kwa masaa, nilitaka kuwa mwendawazimu lakini nashukuru Mungu alinipa nguvu.
“Hakuishia hapo, nami akanilaza kitandani kwa miezi mitatu nikiwa sijui nini kinaendelea. Nimekwenda kuponea Mlandizi sehemu moja inaitwa Disunyala kwa mtaalamu mmoja ambaye ndiye aliyeninyanyua kitandani. Ila alikataa kuua, alisema yeye anatibu tu. “Nilimshukuru kwa msaada wake baada ya kupona vizuri, nilitafuta waganga wa kunilipizia kisasi wengi walichemka, ilionekana jamaa kajidhatiti.
“Ndipo nilipo mpata jamaa mmoja aliyenielekeza kwenda sehemu moja ipo ndani kidogo ya nchi ya Msumbiji inaitwa Silver Makua. Kwa vile nilitaka kulipa kisasi niliuza sehemu ya shamba langu na kumfungia safari. “Nilipitia Mtwara kuingilia boda ya Namoto mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.
Nilitumia usafiri land lover za kizamani na kufika kwenye kijiji hicho. Nilifanikiwa kuonana bibi mmoja mzee sana. Baada ya kumweleza na yeye kuangalia aliniambia atanisaidia. Usiku wa siku ule nilichimbiwa shimo na kufukiwa nakabakia kichwa nje.
“Nilikaa nje peke yangu mpaka asubuhi huku fisi na wanyama wa kutisha wakipita karibu yangu bila kuinifanya kitu. Bundi walitua juu ya kichwa changu bila kufanya kitu na kuondoka. Nilipewa masharti nisipige kelele kwa chochote nitakachokiona. Bila hivyo vitu nilivyoviona usiku ningekufa kwa presha. Kazala uchawi upo na unatisha.
“Alfajili ya siku ile nilinyweshwa dawa nikiwa bado sijafukuliwa baada ya kunyweshwa nilifukuliwa na kuoshwa. Kisha lipelekwa kwenye makaburi na kupewa kisu nichome katikati  ya kaburi nilifanya vile.
Baada ya zoezi lile niliambiwa naweza kuondoka.”
“Basi huo ndiyo uganga uliofanyiwa baada ya kusafiri umbali mrefu?”
“Yule bibi aliniambia, hakuna wa kuniua nitakufa kwa amri ya Mungu na kila aliyeshiriki kuiua familia yangu lazima na yeye atazikwa. Nilirudi nyumbani, wiki moja baada ya kurudi familia ya jirani yangu ilianguka kama kuku wa mdondo, hivi sasa nyumba na shamba limebakia gofu wanaishi paka na popo.”
“Aisee naomba na mimi unipeleke,” nilijikuta nikiwa na hamu ya kwenda huku ambako niliamini ndipo fanaponifaa sana.
“Ni muda mrefu lakini nitakuelekeza, ukifika pale kijijini jina la yule bibi ni maalifu sana hakuna asiyemjua, Ulizia Nyangunda.”
“Hakuna tatizo mwisho wa mwezi nikipokea mshahara nitaomba likizo lazima nami niendende nikawabakize watu nyumba zao magofu waishi paka na popo.”
Japokuwa sehemu niliyotaka kwenda ni mbali lakini nilijua ile ndiyo dawa niliyokuwa nikiitafuta. Muda wa kumaliza msiba ulipofika mama alihamia kwenye nyumba yangu mpya na kukaa na mkwewe na wajukuu. 
Moyoni nilibakia na siri nzito ambayo sikutaka kumweleza mtu yeyote, kwa vile vita ile ilikuwa siri yangu, basi niliendelea kuifanya siri yangu  bila familia yangu kujua kilichokuwa kikiendelea. Nilijipanga kwenda Silver Makua kutokana na maelezo ya Kanyenye safari yake japokuwa ilikuwa ya nchi jirani lakini zilikuwa zinahitajika siku tatu, ya kwanza unaishia Mtwara siku ya pili unafika unapokwenda tena mapema saa tano asubuhi kama ukiwahi kuondoka alfajiri.
Baada ya kila kitu kukamilika niliomba ruhusa kazini ya wiki nzima, nyumbani niliwaaga nakwenda kuangalia mradi mpya wa kufungua mkoani, walinikubalia. Niliondoka siku ile jioni na mabasi yanayotoka Mwanza na kufika Dar saa nne usiku, nilala kwenye nyumba ya wageni iliyokaribu wa kituo cha mabasi cha Ubungo ili alfajiri nipande mabasi ya Mtwara.
Asubuhi ya siku iliyofuata niliondoka na basi kuelekea Mtwara ili niunganishe kwenda Msumbiji kwenye mji wa Silver Makua. Niliwasili Mtwara saa kumi jioni sikukaa  niliunganisha na magari madogo mpaka Namoto kwa ajili ya asubuhi niunganishe kwenda Silver Makua.
Nililala Namoto Asubuhi ya siku ya pili baada ya kuchenji fedha na kupata za Msumbiji, kutokana na maelezo niliyopewa na Kanyenye lazima niondoke na kijana mmoja pale mpakani anayejua Lugha ya kule kunisaidia kuwasiliana na wenyeji.
Nilimchukua kijana mmoja ambaye alikuwa akizungumza lugha zaidi ya zaidi ya moja. Alikuwa akizungumza kiswahili kireno kitindiga na kingereza cha kuungaunga. Tulipanda gari dogo kuelekea Silver makua. Nilifika Silver Makua saa tano na nusu asubuhi. Bila kuchelewa tulimuulizia bi Nyangunda kwa kumtumia mkalimani wangu aliyeuliza kwa lugha ya kitindiga. Tuliambiwa alifariki muda mrefu zaidi ya miaka miwili iliyopita akiwa mzee sana.
Nilianza kuiona nuksi  mbele yangu, mzee Kidereko kabla ya kukamilisha kazi yangu alifariki, naye bi Nyangunda  alifariki miaka miwili iliyopita. Nilijiuliza nini hatima ya maisha yangu.
Nilimweleza mkalimani wangu aulize kama tunaweza kupata mganga eneo lile.
“Mmh! Kwa hapa hakuna mganga kama yule bibi, baada ya kufa watoto na wakujuu zake walikataa kurithi mikoba yake.” Alijibu na mkalimani wangu alinitafasilia.
“Hakuna mwingine?” niliuliza nikiwa nimekata tamaa baada ya safari ndefu, lakini imekuwa haina matumaini.
“Mmh! Hebu subiri,” jamaa aliondoka kwenda kumuuliza mtu wa jirani aliyekuwea akitengeneza bai, baada ya muda alirudi.
“Sikilizeni, kama mnaweza panda gari mpaka Msibwa Daplaya, pale muulizeni mzee mmoja anaitwa Ngugude, wanasema ni kiboko kuliko hata marehemu bi Nyangunda.”
“Anasema kweli?” nilishtuka.
“Yule mzee kiboko.” Alitujibu yule kijana.
“Amesema yupo wapi?”
“Msimbwa Daplaya.”
“Kuna umbali gani toka hapa?”
“Mwendo wa saa tatu.”
“Kiasi gani?”
“Mnasema mmetokea Namoto?”
“Ndiyo.”
“Nauri yake haipishani sana kama kuzidi ni kidogo sana.”
Tulimshukuru na kuagana na yule kijana, tulielekea kwenye kituo cha basi kilichokuwa mbele kidogo na tulipokuwa. Haukupita muda ilisimama Toyota Coaster iliyokuwa ikitokea Silver Makua.
Baada ya kuteremka abiria zaidi ya watano  kituo kile tulipata nafasi ya kukaa. Tulifika Msibwa Daplaya saa tisa alasiri.
Niliteremka na kusogea kwenye duka ambalo alikuwa kijana mmoja, mkalimani wangu aliuliza na kuelekezwa, alinifuata na kunieleza.
“Itabidi tupande baikeli tupelekwe kwa mganga aliyekuwa akikaa nje kidogo ya mji.”
“Hakuna tatizo.”
Tulielekezwa sehemu panapokodiwa baiskeli, tulikodi mbili na madereva wake. Safari ya kutoka nje ya mji ilianza. Tulijikuta tukipanda na kushuka milima huku vijana waliotupakia wakionesha uwezo wa kuendesha baiskeli kwa masafa marefu tena kwenye barabara mbovu.

                  Share

Reactions

Chapisha Maoni

0 Maoni

'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();