SEHEMU YA *16---------20*
Pale nyumbani palikuwa kimya kila mtu aliendelea na shughuli zake kama hakikutokea kitu chochote cha hatari. Jioni ya siku ile tulizunguka kwenye baadhi ya vijiji, giza lilipoingia tulirudi nyumbani. Tulikuta mzee Kidereko bado hajaamka, kitu kilichotutia wasiwasi kwani alilala kuanzia asubuhi mpaka jioni. Nilijiuliza usingizi gani huo au ndiyo kapitiliza kabisa?
Hali ya utulivu uliokuwepo ilizidi kutupa wasiwasi na kujiuliza nini hatma ya yote. Majira ya saa tatu usiku tulifuatwa na yule binti aliyetupokea siku ya kwanza tuliyofika.
“Mzee anawaita.”
“Mzee gani?” nilijikuta nikiuliza.
“Jamani kaka Kazala hapa nyumbani kuna wazee wangapi?’
“Mmoja.”
“Basi ndiye anayewaita.”
“Ameamka?”
“Ndiyo.”
“Saa ngapi?”
“Muda mrefu ameoga amekula na kupumzika.”
“Lakini hajambo?”
“Hajambo mbona hali ile ya kawaida tumeizoea kazi hii yataka moyo la sivyo utaiacha.”
Tuliongozana na yule msichana hadi ndani ya nyumba ya mzee Kidereko, ilikuwa tofauti na siku zote ambazo huzungumzia nje, chini ya mwembe au kilingeni kwake. Alipotuona alitukaribisha.
“Karibuni vijana wangu.”
“Asante mzee, shikamoo.”
“Marahaba karibu mketi.”
“Asante.”
Tulikaa kwenye viti vya kukunja na kusubiri alichotuitia. Baada ya ukimya mfupi alizungumza.
“Vijana wangu.”
“Naam mzee,” tuliitikia kwa pamoja.
“Kwanza poleni kwa kuwachelewesha tofauti na tulivyokubaliana na matarajio yenu.”
“Kawaida mzee, tukupe pole wewe kwa matatizo uliyokutana nayo,” nilimpa pole kwa kuamini hata kama angekufa mimi ndiye ningekuwa chanzo.
“Wala usihofu ile ni moja ya kazi zetu, kazi nyingine lazima ujitolee uhai ufe wewe au afe yeye.”
“Kwa hiyo kazi imekuwa nzito?”
“Ilikuwa si nzito sana japo kidogo iondoke na roho ya mtu.”
“Unamaanisha nini?”
“Baada ya kafara ya mbuzi mwekundu, kazi iliyokuwa imebakia ni kummaliza kabisa kumbe katika sehemu ya uhai wake kuna ulinzi mkubwa uliomzunguka yaani atakayegusa lazima aondoke.
“Baada ya kuingia porini ili kumalizi kazi, kilikuja kitu cha ajabu ambacho nimepambana nacho mpaka alfajiri. Ilikuwa vita nzito ambayo kwangu ilikuwa mara ya pili japo hii ilikuwa kubwa kidogo. Lakini mpaka naishiwa nguvu nilikuwa nimemaliza kazi, kama ningeishiwa nguvu sijamaliza ningekufa mimi.”
“Mungu wangu,” nilishtuka.
“Usishtuke ni jambo la kawaida kwetu waganga.”
“Kwa hiyo?”
“Kesho mnaweza kurudi kazi imeisha.”
“Kuhusu yule jamaa itakuwaje?”
“Kazi imeisha hivi mkirudi mtakuta msiba.”
“Msiba?”
“Ndiyo.”
“Wa nani?”
“Wa adui yako.”
“Kafa lini?”
“Alfajiri ya leo.”
“Mmh! Umejuaje?”
“Ndiyo kazi yangu, wewe umeleta si juu yako kujua kila kitu kinachofanyika zaidi ya kufanikisha kilichokuleta.”
“Nini kilichomuua?”
“Wewe ulitaka afe kwa nini?”
“Ajali.”
“Basi kafa kwa ajali leo alfajiri, asingekufa ningekufa mimi.”
“Mmh!”
“Basi nina imani kazi imekwisha japo ilikuwa nzito nashukuru imeisha salama. Japokuwa kuna wakati nilianza kuchanganyikiwa. Lakini niliamini nitamuweza tu asingeweza kushindana na mimi huku ndiko Tewe hakujawahi kushindwa kitu.”
“Basi tunashukuru, na mke wangu?”
“Atarudi mwenyewe wala hakuna haja ya kutumia dawa kwa vile aliyekuwa akimzuzua ameshakufa.”
“Mmh! Mzee kweli atarudi?”
“Baada ya kifo kafukuzwa na ndugu wa huyo mwanaume na kumuona yeye ndiye nuksi.”
“Kwa hiyo?”
“Utamuona mwenyewe anarudi kuomba radhi, nina imani atatulia kwani kama ni adhabu atakuwa ameipata.”
Tuliagana na mzee Kidereko nikiwa siamini na kuona kama vile mzee kazi imemshinda na kuamua kutuondoa kijanja. Tulikwenda kulala kujiandaa na safari ya kesho alfajiri kurudi tulipotoka ili tuwahi kazini japo tulikuwa tumepitisha siku mbili.
Tuliamshwa alfajiri ya siku ya pili kwa ajili ya safari, kwa vile kulikuwa na baridi kali hatukuweza kuoga, tulinawa uso tu.
“Kazala mwanangu kazi yangu japo ilikuwa ngumu lakini nimeimaliza vizuri sana. Ningekuwa mtu mwepesi pale uliponikuta mngekuta mzoga wangu.”
“Ukisema mzoga una maana gani?” nilimuuliza.
“Mngekuta nimekufa.”
“Mmh!” niliguna.
“Kazi ilikuwa nzito tofauti na nilivyofikiria kumbe mtu yule naye amejidhatiti kwa miti shamba lakini Tewe ni kila kitu hatujawahi kushindwa na kitu.”
“Nashukuru mzee wangu, na kuhusu mke wangu?”
“Atarudi tu haitakiwi kutumia nguvu, mkewe anakupenda sana Kama nilivyokueleza jana alipokwenda kunawaka moto.”
“Asante mzee wangu nitashukuru sana.”
“Ila nakuomba kitu kimoja, ulilofanya huku libakie siri yako watu wao ndiyo watakaozungumza yao kuhusiana na kifo cha mgoni wako. Na kifo hiki ni vigumu mtu kujua kwa vile mazingira ya kifo chake hakuna mtu atakuwa na wasiwasi kwa kuamini ni amri ya Mungu.”
“Sawa mzee wangu, nitafanya hivyo.”
“Haya nawatakia kazi njema,” mzee Kidereko alimpatia Shedu kifurushi kidogo na kumwambia:
“Hii ni zawadi yako.”
“Asante,” Shedu alipokea kile kifurushi nikijua ni cha dawa japo sikutaka kujua dawa ya nini. Sikutaka kuhoji kapewa nini kwa vile ile ilikuwa hainihusu, baada kila kitu kwenda kama kilivyopangwa tulisindikizwa na vijana wa mzee Kidereko kwa baiskeli mpaka Mlalo ambako tulifika saa moja kamili asubuhi, kabla magari ya kuelekea Dar hayajaondoka. Tulibahatika kupata tiketi kwenye basi la Umba kwani basi la Shambalai lilikuwa limejaa. Tuliingia na kukaa kwenye siti ya watu wawili.
Saa mbili gari liliondoka Mlalo na kuelekea Dar es Salaam, Shedu alionesha alikuwa na usingizi kwani safari ilipoanza tu aliuchapa usingizi, mimi niliendelea kuuangalia Mji wa Mlalo. Akili yangu ilikuwa njia panda nisipate jibu kuhusu mwanaume aliyemchukua mke wangu kufariki dunia kwa ajali kama ni kweli.
Akili yangu haikuamini, nilijua yule mzee katutoa kisiasa ili tu tusiondoke tukiwa hatuna imani naye. Sifa alizonipa Shedu na niliyoyakuta niliona kuna tofauti kubwa. Lakini sikutaka kuumiza kichwa, ukweli na uongo wa mganga nilijua ningeujua baada ya kufika mjini.
Kwa vile nami niliamka alfajiri pia usingizi wa sehemu usiyoizoea huwezi kulala vizuri, nami usingizi ulinipitia bila kujijua. Nilishtuliwa usingizini na Shedu ambaye alionekana ameamka kipindi wakati mi bado ninachapa usingizi.
“Kazala amka tupate chakula cha mchana.”
“Wapi hapa?” niliuliza baada ya kuona tumefika kwenye kituo cha basi.
“Korogwe.”
“Sasa ni saa ngapi naona jua kali?”
“Saa saba.”
“He! Kumbe nimelala sana!” nilijishangaa kulala muda mrefu bila kuamka.
Tuliteremka Korogwe na kupata chakula cha mchana kisha tulirudi kwenye basi kuendelea na safari ya kurudi kwetu. Tulifika Chalinze saa tisa na nusu alasiri, kwa vile tulikuwa tukirudi nyumbani tulipanda basi linalotoka Dar saa kumi na nusu jioni. Tuliingia kwetu usiku wa saa nne.
Kwa vile muda ulikuwa bado Shedu alikwenda kwake na mimi nilirudi kwangu. Nilichoshukuru siku ya pili ilikuwa Jumamosi hakukuwa na kazi hivyo niliamini ningelala sana. Baada ya kula chakula nilichonunua nilioga na kulala kutokana na kuwa nimechoka sana.
Nilipopanda kitandani nilishtuka siku ya pili tena kwa kugongewa na jirani yangu. Nilifungua mlango na kutoka nje.
“Vipi jirani za asubuhi, ulisafiri?”
“Nzuri, ndiyo.”
“Mbona hukuaga?”
“Ilikuwa haraka sana samahani kwa hilo.”
“Jana mkeo alirudi,”
“Eeh!” nilishtuka kusikia vile.
“Basi juzi jioni alikuja mkeo na mwanao na kukusubiri mpaka usiku bila kutokea, ilipofika usiku ilibidi alale kwenye korido asubuhi ya jana ndiyo kaondoka. Jana tena alikuja hapa bila mtoto alikaa mpaka saa tatu usiku akaamua kuondoka.”
“Atakuwa amekwenda wapi?”
“Mmh! Kwa kweli sijui ila ameondoka na kuniomba mizigo yake niiweke vizuri na kusema atarudi kesho. Nia yake kuingia ndani amesema anaweza kuja na fundi ili amfungulie mlango. Kwa nini hukuacha funguo?”
“Safari ilikuwa ya ghafla sana.”
“Basi kwangu kuna mizigo ya mkeo,”
“Sawa,” nilichukua mizigo ya mke wangu na kuiingiza ndani.
Baada ya kuweka vitu vya mke wangu vizuri nilikaa kwenye kochi nikiwaza na kuwazua kauli ya mganga na niliyoyasikia muda mfupi kuhusu mke wangu kurudi nyumbani. Nilijiuliza kama mke wangu karudi ni kweli yule mwanaume amekufa kwa ajali kama alivyonieleza.
Nikiwa katikati ya mawazo Simon alibisha hodi, nilimkaribisha apite ndani kwa vile mlango ulikuwa wazi. Simon aliingia akionesha kuna kitu anataka kusema, baada ya kuketi alisema:
“Pole na safari.”
“Asante.”
“Mmh! Mzee unatisha.”
“Kivipi?”
“Jamaa tumemzika jana.”
“Jamaa gani?”
“Si mgoni wako.”
“Muongo!”
“Kweli tumemzika jana, kwa kweli mimi na wote tuliosikia sababu ya kifo chake tulijua ni kifo cha kawaida lakini aliyonieleza Shedu nimeshtuka sana.”
“Unashtuka nini wakati hata mgoni wa Shedu naye alilamba udongo.”
“Ni kweli alilamba udongo, kifo chake wengi walijua kilitokana na kumchukua mke wa mtu hata kufa kwake vilevile kulikuwa kama miujiza fulani. Lakini kifo cha mbaya wako kilikuwa cha ajali, gari lake liligongana uso kwa uso na gari la mafuta. Waliofika kwenye tukio wanasema wala hakuomba maji alifia palepale.”
“He! Kumbe kweli?” nilijikuta nikishtuka baada ya kusikia vile.
“Unashangaa nini?”
“Unajua aliyosema yule mzee mimi nilijua ametupa moyo baada ya kuonekana kazi imemshinda.”
“Kaniambia yote Shedu yaliyotokea huko, lakini ukweli unabaki palepale yule mzee ni tishio hasa kwenye kazi za visasi.”
“Lakini naamini adhabu aliyopewa ni kubwa sana.”
“Si ndiyo uliyochangua?” Simon aliniuliza amenikazia macho.
“Adhabu hii sikuichagua bali walinichagulia ili kumkomesha jamaa.”
“Basi tena ni kujipanga upya, shemeji amerudi?”
MKE WANGU ALISABABISHA NIKAWA MCHAWI
SEHEMU YA 17
“Nasikia amerudi juzi jioni na kulala hapa, asubuhi inaonekana labda ameenda kwao.”
“Sasa ndo mkeo atulie kama umemuua huyo, akiendelea na tabia yake utaua wangapi?” Simon aliniuliza swali.
“Kwanza Simon hebu ondoa neno hilo la kusema nimeua, kazi yote kafanya mganga,” nilijitetea.
“Kwa sababu ya nani?”
“Yangu, lakini kwa uamuzi wa wengine mi nilitaka mke wangu tu.”
“Basi ndiyo hivyo mkeo atarudi jipange kuhakikisha kosa la awali halirudiwi.”
Tukiwa katika ya mazungumzo mlango uligongwa hodi, ilikuwa sauti ya mke wangu. Nilitamani ninyanyuke nikampokee lakini niliona aibu mbele ya Simon.
Nilimkaribisha kwa sauti aingie ndani.
Mke wangu aliingia na kuja moja kwa moja nilipokuwa nimekaa na kuja kupiga magoti kuomba msamaha.
“Samahani mume wangu najua nimekukosea kwa yote niliyokutendea, nimeamini yote ni matawi shina ni wewe. Najua nimekuumiza mume wangu kiasi cha kukufanya uchanganyike. Yote ni kiburi cha nazi kushindana na jiwe, leo hii nimegeuka bundi kila kona nafukuzwa familia ya nilipokwenda hawataki hata kunisikia mama naye hataki kuniona nitakuwa mgeni wa nani,
“Mume wangu kazala nakuomba nipo chini ya kiguuu yako wewe ndiye kimbilio langu la mwisho nawe ukinifuikuzwa sina pa kwenda. Kazala mume wangu naomba unipokee tumlee mtoto wetu Zawadi. Najuta kukukimbia mume wangu nimeamini si wajinga waliosema usiache m,bachao kwa msala upitao...Shemeji Simon nsakuomba niombee msamaha kwa mume wa ngu kazala ambaye nilimkosea kwa kuondoka bila kuaga zilikuwa ni hasira lakini leo hii zimekuwa hasara kwangu.
“Kazala bado nakuhitaji katika maisha yangu, rudisha moyo wako nipokee tena nakuahidi kuwa mke mwema katika maisha yangu yote yaliyobaki chini ya jua, nakupoenda kazala nakupenda baba Zawadi nipo chini ya miguu yako akinifukuza na wewe nitakuwa mgeni wa nani,” Mke wangu alilia kilio cha machungu kuonesha kweli ameumizwa na yaliyotokea.
Yote yaliyotokea kwangu hayakuwa tatizo kwangu zaidi ya mke wangi kurudi tena mikononi mwangu. Nilimnyanyua na kumkumbatia na kumweleza nimemsamehe. Nilimkumbatia mwanangu ambaye alikuwa kwenye afya nzuri na mke wangu.
Pamoja na kuumizwa roho na kifo cha mgoni wangu, lakini nilipata faraja ya ajabu mke wangu kurudi mikononi mwangu. Kwa mara ya kwanza niliamini uchawi upo na unafanya kazi.
Maisha yalianza upya huku mke wangu kila kukicha akijutia alichokifanya, nami nilimweleza yote aliyofanya nimemsamehe toka moyoni mwangu. Hali ya utulivu ilirudi ndani bila mtu kunitilia wasiwasi juu ya kifo cha mgoni wangu kuwa nimekisababisha mimi, wengi waliamini ile ilikuwa amri ya Mungu.
Maisha nayo yaliendelea huku nikirudi katika hali yangu za zamani kutokana na mapenzi mazito niliyopewa na mke wangu. Haikuchukua muda toka arudi kubeba ujauzito mwingine ambao huu hakuwa na matatizo nao hakuuzungumzia kuutoa zaidi ya kuulea kwa ajili ya kusubiri siku ya kujifungua .
Hali ile ilinifanya niamini mke wangu kweli tukio lililotokea limempa fundisho. Muda ulipofika alijifungua mtoto mwingine wa kike ambaye nilimwita Happy kutokana na kuraha ya kurudi kwa utulivu ndani ya nyumba yetu. Watoto wetu Zawadi na Happy walikua vizuri huku mama yao akionesha kuwapenda na kuwajali tofauti na Zawadi alipokuwa mdogo alivyo bemendwa na mama yake.
Siku zilizidi kwenda nami nikizidi kuyafurahia maisha, mke wangu alichukua miaka mitatu na nusu toka arudi kuanza mambo yake. Nakumbuka aliniomba sana tutafute msichana wa kazi kwa ajili ya kumsaidia kazi za nyumbani. Kwa vile sikutaka kubishana na mke wangu nilikubaliana naye na kumpa ruksa ya kutafuta mfanyakazi.
Haikuchukua hata siku tatu msichana wa kazi alipatikana kuonesha alimuandaa hata kabla ya kunieleza. Kwa vile sababu zake zilikuwa na uzito nilimkubalia kumleta na kuanza kazi. Tuliendelea na maisha huku familia yetu ikiwa imeongezeka mtu mwingine.
Waswahili wanasema kaniki hata ukiifua na mito na bahari zote dunia na sabuni zote hata siku moja haiwi nyeupe. Pia hawakukosea kusema la kuvunda halina ubani. Toka aliporudi alikuwa na tabia ya kunywa pombe kitu ambacho mwanzo nilikikemea lakini alinibembeleza kwani alikuwa ameizoeshwa na alipokwenda.
Kwa vile nilikuwa nampenda nilimkubalia awe anakunywa siku mojamoja.
Sehemu tuliyokuwa tukiishi kulikuwa na Glosary karibu. Mara nyingi alimtuma msichana wa kazi na kumletea ndani na kunywa. Siku nyingine niliporudi sikumkuta ndani msichana wa kazi alinieleza kama nitarudi kabla hajarudi akamwite.
Nilimtuma akamwite japo muda ule alitakiwa kuwa nyumbani, alimfuata na baada ya muda alirudi akiwa amechangamka kidogo.
“Vipi mume wangu umerudi zamani?”
“Kama dakika tano, vipi umeanza lini kwenda baa kunywa?”
“Samahani mume wangu, leo jirani yetu God alinipa ofa hapo nje kwenye Glosary.”
“Hakuna tatizo ila usiiendekeze sana pombe.”
“Mume wangu si leo tu, tena nimepewa ofa na jirani.”
“Hakuna tatizo ila usiendekeze sana, kunywa siku mojamoja siyo mbaya.”
Kumbe ukaribu na jirani yangu ulikuwa na maana pana zaidi ya ujirani, mke wangu alianzisha uhusiano na jirani yangu ambaye nikiwa kazini alimgeuza mke wake. Nakumbuka siku moja usiku nilishtuka kitandani na kujikuta nipo peke yangu. Sikuwa na wasiwasi kwa kuamini huenda amekwenda msalani.
Kwa vile choo na bafu vilikuwa nje nilijua amekwenda kujisaidia tu, nilijilaza sikuchelewa nilipitiwa na usingizi. Niliposhtuka mke wangu alikuwa pembeni yangu katikati ya usingizi.
Siku ile kabla ya kulala nilipomgusa mke wangu aliniomba radhi kuwa tumbo limemshtuka ghafla. Kwa vile ile haikuwahi kumtokea nilimwacha na kuendelea kulala.
Siku ya pili tena nilipomgusa alinieleza bado tumbo linamuuma:
“Mke wangu umetumia dawa gani?”
“Si..sijatumia dawa yoyote mume wangu.”
“Mke wangu sasa utailea hali hii mpaka lini, kumbuka mumeo hamu zangu lazima nilizimalizie kwako.”
“Najua mume wangu, samahani kwa hilo mume wangu kesho nitakwenda hospitali.”
“Mmh! Sawa.”
“Nisamehe mume wangu,” mke wangu alisema huku akinibusu na kunifanya mwanaume nilegee.
Tulilala kama kawaida yetu kwa kukumbatiana kupeana joto la usingizi mpaka kila mmoja alipolala tuliachiana na kupeana migongo. Kama kawaida nilishtuka tena katikati ya usingizi na kujikuta tena peke yangu kitandani. Pia sikuwa na wasi nilijilaza kitandani lakini usingizi ulichelewa kunichukua nilitulia kitandani nikiwa nimetulizana macho nikiangalia dalini.
Muda ulikatika bila mke wangu kurejea kitu kile kilinitia wasiwasi na kuona labda yupo msalani tumbo limemzidia. Nilinyanyuka kitandani na kutoka nje kwenda kumuangalia mke wangu. Nilikwenda hadi msalani na kumwita kama yupo akijisaidia.
Hakukuwa na jibu lolote, niliingia msalani hapakuwa na mtu nilitoka nje na kujiuliza mke wangu atakuwa amekwenda wapi. Nilizunguka nyumba vilevile sikumuona niliamua kurudi ndani nikiwa na mawazo kibao kukosekana kwa mke wangu usiku mkubwa kama ule.
Nilikaa kitandani nikijiuliza mke wangu usiku ule amekwenda wapi au amezidiwa na kuamua kwenda kwao. Lakini nilijua lazima angenijulisha kuliko kuondoka kimyakimya akijua mumewe nipo.
MKE WANGU ALISABABISHA NIKAWA MCHAWI
SEHEMU YA 18
Nikiwa bado nimekaa kitandani niliuona mlango ukifunguliwa taratibu, alitulia kutaka kuona nani anayeingia vile kwa kunyata huenda ni mwizi. Baada ya mlango kufunguliwa ulitangulia mguu kisha mwili. Kumbe alikuwa mke wangu katika vazi la kanga moja.
Aliponiona alishtuka mpaka kanga ilimdondoka na kubakia mtupu, hakuiokota alibaki amesimama kama mwanga aliyekamatwa akiwanga. Nilimwangalia mke wangu na kushindwa kumuelewa kuwa katika hali ile ya kutahayali.
“Vipi mke wangu?” nilivunja ukimya baada ya kutazamana kwa muda.
“Sa.sa...” alishindwa kuzungumza.
“Unatoka wapi?”
“Msalani, tumbo lilinizidia nikachelewa kutoka.”
“Ulienda choo kipi?”
“Cha nje.”
“Kweli?”
“Ndiyo mume wangu.”
“Na sasa hivi ndiyo unatoka huko?”
“Ndiyo mume wangu,” alijibu vidole vikiwa mdomoni.
“Wakati mi naingia chooni wewe ulikuwa wapi?”
“Wee umekwenda chooni saa ngapi?”
“Hebu kwanza vaa nguo.”
Mke wangu aliinama na kuokota kanga na kujifunga kisha alirudi kusimama alipokuwa awali vidole akirudisha mdomoni kama namtomgoza.
“Mke wangu ulikuwa wapi?”
“Chooni mume wangu,” mke wangu aling’ang’ania jibu lake.
“Si kweli nimeshtuka usingizini na kukaa macho kwa muda mrefu nikawa na wasiwasi labda umezidiwa na tumbo. Nimekuja chooni sikukuona nimzunguka nyumba yote sikukuona sasa hicho choo gani ulichokwenda?” nilimuuliza nikiwa nimesimama karibu yake huku nikiyaona mapigo ya moyo yakimwenda mbio.
Mke wangu alishindwa kunijibu kitu kilichozidi kunipandisha hasira na kuona kuna mchezo mchafu ninachezewa. Nilimuuliza mke wangu kwa hasira huku niivuta kanga aliyojifunga ambayo yote ilibakia mkononi kwangu na kumbakiza tena mtupu..
“Niambie ukweli ulikuwa wapi, kama utanidanganya nitakacho kufanyia hutasahau mpaka unaingia kaburini. Ni mwaka wa tatu na nusu toka moyo wangu upone majeraha. Hujaridhika unauchubua tena, niambie ulikuwa wapi?”
“Samahani mume wangu nilipokuwa narudi toka chooni nilipofika kwenye mlango wa God, aliniita kwake mara moja lakini sijafanya kitu chochote mume wangu.”
“Leo hukufanya kitu, siku zote ulizokuwa ukienda kwake mlifanya nini?” Majibu yake yalinipa nguvu ya kutengeneza uongo unaofanana na ukweli
Swali langu lilimpa wakati mgumu kujibu na kubakia kuuma meno, nami nilipata nafasi ya kuongeza maneno yangu ya uchungu.
“Mke wangu wewe ni kiumbe gani, umefanya nimechuma dhambi kwa ajili yako, tumetulia umeanza tena kibaya zaidi nyumba tunayoishi. Wewe ni kiumbe gani? Mke wangu umerogwa na nani mpaka kuwa katika hali hii?”
“Nisamehe mume wangu ni shetani tu nipo chini ya miguu yako sitarudia tena,” mke wangu alipiga magoti kama mwanga akiwa hana kitu mwilini.
“Haya nieleze ukweli umeisaliti ndoa yetu toka urudi mara ngapi?”
“Kwa haki ya Mungu mara nne.”
“Na wanaume wangapi?”
“Mmoja mume wangu ni God tu, ukweli wa Mungu toka nimkubali ni wiki ya pili. Nimejitahidi kumkatalia lakini amekuwa akinisumbua ikiwemo kunipa ofa na fedha na pombe. Siku zote shetani ana nguvu nimejikuta nikimkubalia na kukusaliti kwa mara nyingine mume wangu.
“ Najua jinsi gani ninavyokuumiza lakini nakuomba usiniache, pombe ndiyo sababu mume wangu nitaiacha. Siku aliyonipa ofa ya pombe ndiyo ukawa mwanzo wa kunisumbua kimapenzi, kwa kweli nilijitahidi sana lakini nilijikuta nimemkubalia bila kujua. Naomba mume wangu usiniache, mama aliisha niambia siku nikifanya ujinga kwako na wewe kunifukuza basi nitafute pa kwenda nisirudi kwake. Nakuahidi mume wangu sitafanya ujinga tena na pombe leo ndiyo mwanzo na mwisho.”
Japo kauli ya mke wangu haikuwa na nguvu ya kunishawishi kumsamehe hasa baada kujua ametoka kwa mwanaume baada ya kunikimbia kitandani na kwenda kufanya uchafu wake. Kikubwa kichoniuma kilikuwa jirani yangu kuonesha dharau kwa kutembea na mke wangu akijua ni mke wa mtu. Kilichoniuma zaidi kilikuwa kumshawishi kunitoroka kutandani na kuniacha peke yangu nimelala.
Roho iliniuma kufanywa bwege kiasi kikubwa, kwangu ilikuwa dharau kubwa sana ambayo iliuumiza sana moyo wangu kwa jinsi alivyonidhalilisha kumchukua mke wangu nikiwa nimelala naye kitandani ile ilikuwa dharau mbaya sana ambayo ilitakiwa kulipa kisasi cha historia.
Mke wangu niliamini hana kosa ila kuna watu walitaka kuniona mimi ni nani. Nilipanga mwisho wa wiki niende tena kwa babu kumtia adabu. Tena mtu huyo sikuwa na huruma naye hata kidogo niliapa kumbakisha jina. Nilimsamehe mke wangu na kumuomba abadilike la sivyo sitamuuliza kitu chochote tena na wala sitamfukuza.
Mke wangu alinihakikishia kutulia hata rudia tena kosa kama lile, siku ile niliiacha ipite lakini moyoni nilikuwa na maumivu na hasira kama nyoka aliyekanyagwa mkia. Nilijitahidi kuficha kilichonikuta kwa watu wote huku nikiomba mwisho wa wiki ufike upesi.
Siku zote mke wangu hakuacha kuniomba msamaha, nilimueleza nimemsamehe toka moyoni na si mdomoni. Jirani yangu baada ya kugundua nimegundua hila zake ya kumchukua mke wangu, akawa anatoka alfajiri na kurudi usiku tumelala. Moyoni nilijisemea wyeye arukeruke lakini siku zako ya kuishi duniani zilikuwa zinahesabika nikifika kwa mzee Kidereko lazima uulambe udongo.
Moyoni niliapa siri ile hataijua mtu yeyote, baada ya kumsamehe mke wangu nilijilazimisha kuishi maisha ya kuilazimisha furaha huku moyoni nikiwa na maumivu makali kutokana na tabia za watu kumgeuza mke wangu jamvi la wageni.
Kwa vile dawa yao niliijua sikutaka kubishana na mtu zaidi ya kupanga safari ya kwenda kwa Mzee Kidereko Tewe. Hakuna aliyegundua mabadiliko yangu kazini na nyumbani. Wengi walijua uhusiano na mke wangu ni mzuri pia tabia yake alikuwa ameilekebisha.
Hata safari yangu niliyoipanga mwisho wa wiki ilikuwa siri yangu sikumwambia hata mwenyeji wangu Shedu aliyenipeleka Tewe kwa mzee Kidereko. Moyo wangu ulikuwa umeingia woga kuiogopa aibu ya kuonekana bwege kama wamejua mke wangu karudia makosa yaleyale.
MKE WANGU ALISABABISHA NIKAWA MCHAWI
SEHEMU YA 19
Siku ya ijumaa baada ya kazi niliianza safari yangu huku nikimuaga mke wangu kuwa nakwenda nyumbani kwa wazazi nimeitwa ghafla. Mke wangu alinitakia safari njema huku akinihakikishia kwa maneno mazito.
“Mume wangu najua huniamini tena moyoni mwako, lakini nakuahidi mbele ya muumba ambaye hakosekani kila sehemu, yeye ndiye shahidi yangu kwa haya nitakayo yasema mbele yako muda mfupi kabla hujaenda kuwaona wazazi. Ni kwamba nimekuwa kama kaniki isiyobadilika rangi hata ukifuliwa na kusuguliwa vipi.
“Lakini hili ninalo lisema mbele yako kama nitarudia tena kosa mume wangu basi Mungu anigeuze kiumbe chochote cha ajabu au kuyachukua maisha yangu,” mke wangu alisema kwa sauti ya uchungu.
Mke wangu alizungumza maneno mazito ambayo yalinitoa machozi na kuamini kile kiapo kilitoka moyoni mwake na kujutia alichokifanya. Pamoja na kutaka kumuamini bado nilimuona kama mjusi asiyeweza kugeuka kuwa nyoka hata ukimpaka unga.
Nilijua kile kilikuwa ni kilio cha majuto lakini mke wangu alikuwa na akili za mbuzi kujisahau baada ya tukio kutulia. Kwa upande mwingine kiapo cha mke wangu nilikiona kizito ambacho alijichagulia adhabu kama atarudia upumbavu wake.
Wazo la kubadili safari yangu lilikuja na kuona hakuna haja ya kwenda kwa mzee Kidereko nitulie tu na kufanya mambo mengine. Wazo lile nilitaka kulipa nafasi lakini aibu ya mtu kutembea na mke wangu ilikuwa kubwa kwangu, kwa kuamini kila nitakapokutana na mgoni wangu moyo wangu ungekosa amani. Baada ya kusimama kwa muda nikishauriana na moyo wangu nilishtuliwa na mke wangu aliyeonekana kunifuatilia kwa karibu.
“Mume wangu najua huniamini lakini namuomba Mungu tena na tena aniepushe na tabia hii ambao imekuwa chukizo kwako bado umenisamehe mume wangu japokuwa sijui unaniwazia adhabu gani kunipa. Lakini narudia tena kuapa mbele yako na muumba wangu kama nitarudia tena nitakuwa sifai kuishi Mungu ayachukue maisha yangu.”
“Mke wangu nimekusamehe toka moyoni mwangu wala sina nilichokipanga kukufanyia. Ila huyu mshenzi ataniona.”
“Mshenzi gani mume wangu?”
“God lazima awe mfano kwa mtu yeyote atakayekugusa nimechoka..nimechoka kila siku kuwa mimi tu,” nilisema kwa uchungu japokuwa sikupenda mke wangu aijue dhamira yangu.
“Mume wangu nimekuahidi haitatokea tena madhara yake nimeyaona, nikifanya tena heri Mungu anigeuze mnyama sifai kuwa mwanadamu.”
“Nimekuelewa mke wangu, wacha niwahi usafiri japo sina uhakika nitaondoka na gari gani muda umekwenda sana.”
“Nikutakie safari njema mume wangu, wasalimie baba na mama mashemeji na wifi zangu.”
“Salamu zimefika.”
Niliwaaga na wanangu kisha niliondoka na nguo chache za kubadili kwa siku moja mbili nitakazo kuwa huko na kuomba Mungu nilirudi jumapili usiku ili jumatatu niamkie kazini.
Niliondoka nyumbani saa kumi na moja jioni had sokoni na kununua vitu vya kumpelekea mzee Kidereko. Baada ya kununua mahitaji muhimu nilikwenda njia panda ambako nilibahatika kupata basi la kutoka Mwanza ambalo lilikuwa limechelewa kidogo.
Kutokana basi kuchelewa njiani baada ya kuharibika dereva aliendesha kwa mwendo wa kasi tuliingia Chalinze saa nne na nusu za usiku. Niliteremka na kwenda kutafuta nyumba ya wageni. Nililala mpaka asubuhi ya siku ya pili saa mbili asubuhi, nilipanda basi la Shambalai kutoka Dar kwenda Lishoto. Niwasiri Mlalo majira ya saa kumi na moja jioni.
Kwa vile niliisha kuwa mwenyeji nilikodi baiskeli mbili moja ilinibeba mimi na nyingine ilibeba bidhaa nilizonunua kwa matumizi ya kijijini ambazo alizipenda mzee Kidereko.
Nilipofika nilipokelewa kwa furaha na yule msichana aliyetupokea siku za nyuma. Litokana na muda mrefu kupita bila kufika kule kijijini, nilimkuta ana mtoto mdogo wa kama mwaka na nusu. Baada ya kupokelewa nilikaribishwa chini ya mti na kupewa mkeka nijipumzishe kwanza.
Mzee Kidereko sikumuona nilijiuliza atakuwa amekwenda kwenye kazi zake za porini au sehemu gani.
Baada ya muda nilimuuliza mtoto wa mzee Kidereko ambaye nilikuwa nikizungumza naye habari za safari.
“Vipi mzee yupo wapi?”
“Yupo ndani amelala siku hizi amekuwa mgonjwamgonjwa sababu ya uzee na kazi za mikiki. Kuna kazi moja ilikuwa nzito sana huwezi kuamini tulijua mzee amekufa. Kazimika kwa wiki nzima kitandani na alipopata ufahamu amekuwa mgonjwamgonjwa muda mwingi anapumzika na kazi nyingi za mzee anafanya kaka.”
Habari zile zilinishtua baada ya kusikia mganga anaumwa kufikia hatua ya kushindwa kuzifanya kazi zake na kumpa mtu mwingine. Niliamini uwezo wa mzee Kadereko ni karama toka kwa Mungu lakini mwanaye ni uganga wa kujifunza hauna nguvu sana. Nilihoji uwezo wa kaka yake kwa wateja waliokuja.
“Umesema kaka yako anashika mikoba ya baba yenu, kweli ana uwezo kama mzee?”
“Kwa kweli sijasikia malalamiko yoyote kutoka kwa wateja ila kazi ikiwa kubwa sana anaifanya mwenyewe.”
“Kwa hiyo kazi zingine anazifanya mwenyew?”
“Ndiyo, bado hajaiacha rasmi kwa vile bado anamkomaza kaka ila akikomaa kazi zote atazifanya yeye.”
“Nikitaka kazi yangu aifanye yeye itakuwaje?”
“Utakusikiliza kama itakuwa nyepesi ataifanya kaka, sema tu hujafanya naye kazi lakini kila kukicha amekuwa akiivaa sawasawa kofia ya baba.”
“Na mzee huamka saa ngapi?”
“Muda wake umekaribia.”
“Kwa hiyo mgeni akifika anaonana na kaka yako?”
“Hapana, mgeni yeyote aliyetoka mbali lazima aonane kwanza na mzee ili kumpa faraja ya safari yake ndefu ya kuja kijijini.”
“Mmh! Kama hivyo sawa.”
Tukiwa katika ya mazungumzo alitumwa mtu kuniita naitwa na mzee ndani. Nilinyanyuka hadi sebuleni kwake, aliponiona alinyanyuka kwenye kiti chake cha uvivu na kunikaribisha.
“Kazala karibu baba.
”MKE WANGU ALISABABISHA NIKAWA MCHAWI
SEHEMU YA 20
“Asante baba, shikamoo.”
“Marahaba, karibu sana.”
“Asante, pole na matatizo.”
“Asante, lakini ndiyo maisha tuliyochagua hatuna budi kukubaliana nayo.”
“Vipi unaendeleaje?”
“Ndiyo nimeisha kuwa mgonjwa sina kingine zaidi ya kusubiri tu mauti unichukue.”
“Hapana baba, nina imani ukitumia dawa utakuwa sawa tu,” nilimpa moyo.
“Hapana, pigo nililokutana nalo ni Mungu tu, lakini namshukuru hata nikifa leo kuna mrithi nimemuacha japo si kwa kiwango changu lakini atawasaidieni sana. Ningekufa na kinyongo kama dhoruba lile lingeniua bila kuacha mrithi wangu. Lakini sasa hivi wala sina wasiwasi mauti yanichukue tu.”
“Baba maneno gani hayo ya kuchoma moyo,” maneno ya mzee Kidereko yalinitisha.
“Kukuchoma moyo kivipi Kazala? Wakati kila mwanadamu lazima atakufa hakuna atakaye ishi milele.”
“Ni kweli baba, lakini basi tupe maneno ya kutupa moyo si unajua tunakutegemea.”
“Kazala usiogope kufa kwa vile kifo kipo hata usipotaka kukisikia.”
“Kwani mzee wangu hiyo kazi ilikuwa nzito kuliko ya kwangu?” nilimuuliza.
“Hii mwanangu temea chini, unajua tunafamnya kazi na watu wengi wenye nyadhifa serikalini na watu wa kawaida. Kuna kigogo mmoja wa serikalini ambaye nilimsaidia kupata ubunge na kumweleza ipo siku atakuwa mtu mkubwa serikalini.
“Kwake aliona kama ndoto ya mchana basi baada ya kupata ubunge tu kwenye baraza la mawaziri na yeye akatajwa. Alikuja hapa akiwa haamini kilichomtokea kwa kweli alichanganyikiwa. Nilimwambia bado namtengenezea mazingira ya urais.
“Kwa kweli nyota yake ikawa inang’ara kila kukicha hata vyombo vya habari vikawa vikimtaja sana kama mrithi wa rais anayemaliza muda wake. Kumbe kuna watu wakawa wanamtafuta ili kumzima kama kibatari. Kuna siku aliingia ofisini asubuhi bila kujua kuna bomu limetegwa. Alipokaa kitini alikutana na bomu alikuwa afie palepale kwenye kiti.
“Lakini kinga niliyompa ndiyo iliyomsaidia. Kwa vile familia yake ilikuwa ikijua kila kitu wamchukua na kumleta huku mara moja akiwa nusu mfu. Baada ya kuletwa nilifanya kosa kubwa kwa kufanya kazi kimazoea bila kuangalia uzito wa tatizo lile.
“Nilijua tatizo lile si kubwa kutokana na nilivyomkinga kumbe watu walihangaika na kufuata uchawi mpaka Nigeria ili kummaliza baada ya waganga wa hapa kuchemsha. Baada ya kuletwa nilimhudumia bila kujikinga nilifanikiwa kulitegua bomu alilotupiwa. Wakati likitoka kikanipamia kwa vile sikuwa sawa lilinitishisha si kitoto.
“Kutokana na uzito wa kitu kile na mimi nilivyo kidharau nilikuwa nife lakini nami nilikuwa sawa ndipo liliponilaza wiki nzima nikiwa sijitambui nusu mfu.
Vijana wangu walishindwa ilibidi afuatwe mganga mwingine kuja kunizindua. Toka nilipozinduka hali yangu su nzuri mwili umekuwa mgonjwamgonjwa. Lakini mshukuru Mungu hali yangu inaendelea vizuri.”
“Una muda gani toka upatwe na matatizo haya?”
“Mwaka sasa.”
“Mbona muda mrefu huna mabadiliko yoyote?”
“Ninayo makubwa sana, ehe za siku?”
“Nzuri mzee wangu, za miaka na wewe?”
“Kama ulivyozikuta, ila nashukuru sana kwa kutukumbuka kila mara, vitu vyako unavyotutumia tunavipata kwa kweli umekuwa kijana wa ajabu kukufanyia kazi moja lakini umekuwa akitukumbuka tofauti na watu niliowawezesha kimaisha hawatukumbuki mpaka wawe na shida.”
“Kila mtu ana roho yake, wapo wasiojua kushukuru hata wakipewa.”
“Ni kweli mwanangu, haya leo kwetu una tatizo gani tena?”
“Kama la awali.”
“Mkeo katoka nje ya nyumba tena?” mzee Kidereko alishtuka.
“Ndiyo mzee wangu.”
“Kwa hiyo unatakaje?”
“Kwa vile yule jamaa kanifanyia dharau ya kutembea na mke wangu nataka afe kifo cha mateso na aibu.”
“Hakuna tatizo, japo kazi hii si kubwa lakini nitakufanyia mwenyewe.”
“Nitashukuru mzee wangu.”
“Unataka kifo cha aina gani?”
“Chochote ili wadoezi wa wake za watu wakome.”
“Kwa vile mkeo haaminiki nitakufundisha baadhi ya adhabu atakazowapa wagoni wako ili usisumbuke kuja huku kila mara. Nitakupa zawadi moja kubwa sana nina imani huenda utakaporudi usinikute.”
“Unataka kwenda wapi?”
“Na uzee huu ukiuondoa si kifo, nataka nikifa nikuachia zawadi ya kukusaidia katika maisha yako.”
“Zawadi gani?”
“Tego ya mtu anayetembea na mke wa mtu na vitu vingi nitakupatia ili uweze kujilinda hata kuwasaidia waliokuzunguka.”
“Nitaweza kweli?” kazi ile niliona kama nzito.
“Utaweza tu wala si kazi ni vitu vyepesi kama utakuwa tayari.”
“Haya baba hakuna tatizo.”
Tulikubaliana siku ya pili anipeleke porini akanionesha baadhi ya dawa za kuwakomesha wadoezi wa wake za watu. Siku ya pili alfajiri tuliondoka nyumbani na kuelekea porini, ajabu siku ile tulikuwa wawili tu mimi na mzee Kidereko ambaye pamoja na maradhi umri nao ulimtupa. Tulikwenda kwenda wa taratibu kwa mwendo wa saa nne bila kupumzika hadi kwenye pori kubwa ambalo lilikuwa na miti mingi.
Mzee alioninesha miti mingi na kazi yake kwa ajili ya kutibu maradhi pia alinionesha baadhi ya miti ukiitumia hugeuka kuwa uchawi wa kumzuru mtu. Nilijiuliza miti ile nitaijuaje kwa mara moja kwa vile sikuwa mganga wala mzoefu wa kazi ile. Kwa upande wangu niliona kama vile mzee Kidereko alikuwa akipoteza muda wake kunionesha vitu ambavyo nilijua siwezi kuvikumbuka.
Alinitembea hadi kwenye mti mkubwa mfano wa mbuyu, tulipofika pale tulisimama na kunieleza niweke mkoba chini na kuniomba nivue shati, nilivua shati na kubakia na suruali kisha akinipa kaniki kujifunga kwa chini na kukiacha kifua wazi.
Alichukua maji yaliyokuwa kwenye chupa na kuyaweka mdomoni kisha aliyapiliza kuelekea kwenye ule mti mkubwa. Baada ya kumaliza zoezi lile alichukua unga wa dawa na kuurusha sehemu nne za dunia na kusema kwa sauti.
“Hodi mizimu.. hodi majini yote kianzia Kibwengo na majini yote..hodi tumekuja kutaka msaada wenu.. tunajua ninyi mna nguvu, mizimu yote na majini tupokeeni tufanye kazi yetu,” baada ya kusema maneno yale nilisikia kitu kama muungurumo ambao haukudumu muda mrefu ulinyamaza.
Baada ya hali ile kutulia nilimsikia mzee Kidereko akisema:
“Asante mkuu wa mti huu asante mizimu yote asante majini yote.”
Alipomaliza kusema vile alinieleza nikae chini kwenye mwinuko miguu nikiinyoosha kuuelekea ule mti mkubwa. Nilikaa chini na kuuelekea mti mkubwa kama nilivyoelekezwa na kutulia kusubiri maelekezo mengine.
Share
0 Maoni