SEHEMU YA *11--------15*
Nilijikuta nikijiuliza kuna tatizo gani lililomkuta mke wangu kiasi cha kushindwa kupatikana kwa simu yake. Muda nao ulikuwa umekwenda sana, nikaamua kumsubiri nikiwa na imani kubwa kuwa atarudi muda si mrefu. Mara ilifika saa mbili za usiku akiwa bado hajarudi, nikazidi kuchanganyikiwa.
Ilipofika saa tatu bila kumuona mke wangu nilijaribu kupiga tena simu lakini bado haikuwa ikipatikana. Niliamua kwenda kwa wazazi wake kutaka kujua kuna kitu gani kimetokea kiasi cha mke wangu kuondoka haraka na simu yake kutokuwa hewani kipindi kirefu.
Niliamua kumfuata kwao, nilitoka na kuegesha mlango, sikutaka kuufunga kwa kuhofia kupishana naye. Nilikwenda ukweni kumuulizia mke wangu, nilikodi gari mpaka kwa wakwe zangu. Bahati nzuri nilikuta bado hawajalala, baada ya kugonga hodi mama mkwe alinikaribisha kwa vile aliifahamu sauti yangu.
“Karibu baba Zawadi.”
“Asante mama, shikamoo,” niliamkia huku nikiingia ndani na kukaa kwenye kochi.
“Marahaba, kwema utokako?”
“Namshukuru Mungu, sijui mwenzangu amefika huku?”
“Mmh! Kwa leo sijamuona,” kauli ile ilinishtua sana lakini nilificha mshtuko wangu.
“Sasa atakuwa amekwenda wapi?” nilijikuta nikimuuliza swali mama mkwe lisilomhusu.
“Nitajuaje baba, kwani alikuaga anakwenda wapi?”
“Mama, yaani nimerudi nyumbani nimekuta ufunguo kwa jirani bila maelezo yoyote.”
“Zawadi yupo wapi?”
“Ameondoka naye.”
“Mmh! Sasa atakuwa amekwenda wapi?”
“Hata mimi nashangaa tena nasikia kaondoka na ile gari ya yule mwanaume wake.”
“Mmh! Unasema kweli?” mama mkwe alionesha kushtuka.
“Kutokana na maelezo ya mtu aliyemuona.”
“Kwa hiyo hukumuona kwa macho yako?”
“Sijamuona mama nimeambiwa.”
“Basi usifikirie moja kwa moja kuwa ameondoka na mwanaume wake wa zamani, kwani ameondoka tangu saa ngapi?”
“Saa tano.”
“Saa tano, sasa atakuwa amekwenda wapi na mtoto, kwani hali hii imetokea mara ngapi?”
“Ni leo tu mama toka tumalize yale matatizo yetu.”
“Nakuomba rudi nyumbani ukapumzike, akirudi atakueleza alikuwa wapi kama maneno yake hayaeleweki mlete kwangu. Nimechoka na upumbavu wake, hawezi kutuchezea akili kiasi hiki,” mama mkwe naye alionekana kukerwa na kitendo cha mke wangu kuondoka bila kuaga.
“Sawa mama.”
“Nina imani hakufika mbali angekuwa amekwenda peke yake ningekuwa na wasiwasi, lakini kwa vile ameondoka na mtoto atawahi kurudi tu huenda mmepishana amesharudi nyumbani.”
“Nitashukuru mama.”
“Basi baba rudi nyumbani, nina imani mpaka muda huu atakuwa amerudi tu.”
“Sawa mama,” nilikubaliana na mama mkwe na kugeuza kurudi nymbani nikiwa na matumaini ya kumkuta.
Nilikodi gari ili niwahi nyumbani nikiamini huenda mke wangu amerudi na kutonikuta na kumfanya awe na wasiwasi wa kutaka kujua mimi nipo wapi. Nilikwenda hadi nyumbani na kuingia ndani, nyumba ilikuwa kimya kuonesha hakukuwa na dalili za kuwepo mtu ndani.
Wazo langu lilikuwa labda amerudi na kuingia kulala, nilikwenda chumbani. Chumba kilikuwa kitupu na hali ilikuwa ileile ya chumba kuwa katika hali ya uchafu. Nilibakia nimesimama kwenye mlango wa kuingilia chumbani kwa dakika kadhaa nikiwa siamini kilichokuwa mbele yangu.
Nilijiuliza mke wangu atakuwa wapi?Nilirudi sebuleni na kukaa kwenye kochi nikiwa sijui mke wangu amekwenda wapi. Hata hivyo, nilikuwa na wasiwasi kwamba mama mkwe alikuwa akijua kila kitu ila alinificha. Ilikuwa ni mateso juu ya mateso kwani siku ile nilikuwa nimefanya kazi nzito kwa muda mrefu hivyo niliamini nikirudi nyumbani ningepumzika. Lakini tangu nilipofika nilikuwa juujuu kwa ajili ya kumtafuta mke wangu, tena bila kula.
Njaa iliyokuwa ikiniuma kama kidonda ilitoweka kutokana na mshikemshike wa kuzunguka kumtafuta mke wangu. Saa ya ukutani ilionesha tayari ni saa sita na nusu usiku, bado hakukuwa na dalili za mke wangu kuonekana. Bado sikukata tama, nilirudia kumpigia simu lakini hali ilikuwa ileile, hakuwa akipatikana hewani.
Nilijikuta nikiwa na wasiwasi kuhusu mke wangu na kujiuliza kipi kimemsibu mpaka muda ule awe hajarudi. Ingekuwa ameondoka peke yake ningejua amerudia matatizo yake. Lakini alikuwa ameondoka na mwanangu wa pekee Zawadi, nilijiuliza kama kweli ameparama tena na kurudiana na yule mwanaume huenda ikawa hata Zawadi si mtoto wangu wa kumzaa.
Kwa upande wa Zawadi, ningekuwa tayari kufa kama ningeambiwa si mtoto wangu kwani nilifanana naye kila kitu. Kila aliyemuona alijua ni mwanangu bila hata ya kumwambia. Nilikaa sebuleni kumsubiri nikijipa moyo kuwa huenda amekwenda kwenye sherehe na kuchelewa kurudi.
Nilikaa sebuleni mpaka alfajiri ilipoingia bila kumuona mke wangu wala kivuli chake. Nilijiuliza mke wangu atakuwa wapi? Kutokana na kulala usingizi wa mang’amung’amu niliamka asubuhi kichwa kikiwa kizito. Kwa vile niliacha kiporo cha kazi, niliposhtuka nilioga harakaharaka nikitegemea huenda mke wangu akatokea kabla ya kwenda kazini kama alivyofanya siku za nyuma lakini haikuwa hivyo.
Mpaka naondoka, sikumuona mke wangu na kumuachia funguo jirani nikiamini huenda jioni nikirudi naweza kumkuta. Nilikwenda hadi kazini nikiwa nimechoka sana, nilificha uchovu wangu na kufanya kazi kwa nguvu japo kila nilipokuwa peke yangu nilisinzia na kuwafanya wafanyakazi wenzangu kunitania eti nilikesha na shemeji bila kujua msiba mzito uliokuwa moyoni mwangu, baada ya bomu lililokuwa limetulia kulipuka upya.
Baada ya kazi nilirudi nyumbani nikiwa na matumaini ya kumkuta mke wangu lakini nilipofika nilikuta mlango umefungwa. Nilikwenda kwa mke wa jirani yangu kuulizia huenda alikuja na kuondoka.
“Karibu shemeji,” alinikaribisha aliponiona.
MKE WANGU ALISABABISHA NIKAWA MCHAWI
SEHEMU YA 12
“Asante, vipi hajarudi mke wangu?”
“Sijamuona kwani alikwenda wapi?” lilikuwa swali juu ya swali.
“Hata najua! Mbona huyu mwanamke ananitesa sana, kosa langu nini kila kukicha niwe mimi tu?” nilijikuta nikibwabwaja kwa uchungu bila kujielewa.
“Kwani kuna nini shemeji?”
“Yule mwanamke kila kukicha amekuwa akinifanyia mambo yaliyokosa ubinadamu kabisa.”
“Lakini mbona tumeishi naye vizuri tena mke wako ni mpole na msikivu sana, tatizo nini?”
Nilijikuta nikifunguka mwanaume na kuuanika ubaya wa mke wangu, mke wa jirani alinionea huruma na kusema:
“Mbona haendani na usemayo?”
“Mke wangu ni chui ndani ya ngozi ya kondoo.”
“Pole sana shemeji, na mtoto kampeleka wapi?”
“Nitajuaje?”
“Kwani kwao wanasemaje?”
“Nao hawajui lolote.”
“Ungesubiri na leo huenda akarudi usiku huu.”
“Mmh! Sidhani.”
Niliagana na mke wa jirani yangu na kuingia chumbani ambako kulikuwa vululuvululu. Baada ya kuoga nilikwenda kununua soda na mkate ili nitulize njaa. Chakula kilinishinda na kulala na njaa. Usingizi wangu ulikuwa wa kushtukashtuka kila mara kwa kuamini labda mke wangu amerudi.
Kila niliposhtuka usingizini nilitulia na kusikiliza huenda kuna sauti ya mtu ikiniita. Niliona chumbani kama nikilala akiita naweza nisimsikie hivyo nikaamua kuhamia sebuleni na kukaa kwenye kochi kumsubiri mke wangu. Muda nao ulikuwa umekwenda, ilikuwa tayari imegonga saa saba na nusu usiku, bado niliamini mke wangu anaweza kurudi.
Mpaka kunakucha hakukuwa na dalili za mke wangu kurudi, hata bila kunawa uso nilikwenda ukweni kuulizia taarifa za mke wangu, labda amerudi na kuogopa kurudi na kufikia kwa mama yake. Nilipofika ukweni nilikuta ndiyo kwanza wanaamka.
“Vipi baba mbona asubuhi asubuhi?” mama mkwe aliniuliza baada ya kuniona asubuhi ile.
“Mama, mke wangu yupo huku?”
“Ina maana alirudi na kuondoka tena?”
“Hapana mama hajarudi kabisa.”
“Toka juzi?”
“Ndiyo mama.”
“Mmh! Mbona mwana huyo ana matatizo, sasa atakuwa amekwenda wapi?”
“Kwani huku hajafika?”
“Sijamuona baba yangu.”
“Basi lazima atakuwa amekwenda kwa mwanaume wake.”
“Jamani, yaani ndiyo kafikia hatua hii?” Mama mkwe alishika kiuno kuonesha naye kachoshwa na taarifa ile.
“Basi mama acha niwahi kazini.”
Niliagana na mama mkwe na kurudi nyumbani ili nijiandae kwenda kazini japokuwa nilikuwa katika wakati mgumu baada ya kumkosa mke wangu kwao. Nilirudi hadi nyumbani kichwa kikiwa kizito, chumba nilikiona kama dunia isiyo na kitu chochote zaidi ya mimi peke yangu. Moyo ulikufa ganzi, nilishindwa kwenda kuoga ili niwahi kazini kwani muda ulikuwa umekwenda sana.
Nilihisi kama mwili unakosa nguvu, kichwa kilianza kuniuma kwa mawazo na mapigo ya moyo yalikwenda kwa kasi. Niliwahi kukaa kwenye kochi kabla sijaanguka, nilijilaza nikiwa na maswali mengi juu ya mke wangu kuondoka nyumbani bila taarifa.
Nilijiuliza tatizo nini hasa ikiwa kila kitu kilikuwa kikienda vizuri, nikiwa bado natafuta sababu ya mke wangu kuondoka bila kuaga na sehemu gani amekwenda, chini ya meza niliona bahasha iliyokuwa imefungwa. Nilijikuta nikipata shauku ya kutaka kujua ile barua ya nani.
Pamoja na mwili kutokuwa na nguvu, nilinyanyuka nilipokuwa nimejilaza na kwenda kuiokota ile bahasha iliyokuwa na jina langu. Moyo ulinilipuka kwani ule ulikuwa mwandiko wa mke wangu. Nilijikuta nikiingiwa na wasiwasi huenda mke wangu alirudi asubuhi ile na kunikosa wakati nimekwenda kwao kumtafuta na kuamua kuondoka na kuacha ujumbe.
Niliichukua ile bahasha na kuifungua, nikakutana na karatasi iliyokuwa imeandikwa kwa wino mwekundu. Baada ya kuifungua, nilikutana na maneno ambayo kidogo yasimamishe mapigo yangu ya moyo. Barua ile ilinikatisha tamaa na kujikuta kila herufi moja niliyokuwa nikisoma ndivyo moyo wangu ulivyokuwa ukikamuliwa bila ganzi. Siwezi kuelezea maumivu niliyoyasikia, ilikuwa sawa na kung’olewa jino bila ganzi.
Mpaka namaliza kusoma, machozi yalikuwa yamefunika macho yangu na sehemu ya karatasi ilikuwa imelowa upande kwa machozi. Barua ilisema hivi:
Kwako Kazala,
Najua utashtuka kupokea ujumbe huu na kukufanya uchanganyikiwe. Najua wewe ni mwanaume na wanaume wameumbwa kukabiliana na matatizo. Najua unanipenda na utaendelea kunipenda, lakini kutokana na kushindwa kwenda na wakati na kunigeuza mwanamke wa kizamani wa kukaa ndani kama samani nimeamua kuishi maisha yangu ya uhuru kama wanawake wengine.
Nimeamua kuondoka, sitaki unitafute hata mama yangu naye sitaki anitafute, nimeamua kuishi maisha niliyoamua kuishi mimi mwenyewe. Nimekuvumilia mengi Kazala lakini huna shukrani. Nyumba yetu imekuwa ikiendeshwa na watu wa pembeni kuliko sisi wanandoa.
Kazala umekuwa ukiwasikiliza watu wa pembeni kuliko mimi mkeo, nilikueleza tutaachana tukiwa tunapenda nina imani kauli yangu imetimia. Najua utajiuliza kuhusu mtoto, Zawadi ni mtoto wako na ataendelea kuwa mtoto wako nimeamua kuondoka naye ili aendelee kupata malezi mazuri. Ila akitimiza miaka saba nitakurudishia mwenyewe ila naomba unisahau kabisa.
Tangu leo ninapoondoka, mwisho wa wiki hii nafunga ndoa ya kidini tena kanisani na kuwa mke wa mtu anayefahamika mbele za Mungu. Nawe mpenzi wangu wa zamani fanya hivyo, tafuta mwanamke anayeendana na wewe ili ufunge naye ndoa, ukichelewa unaweza kuugua ugonjwa wa akili.
Nakutakia maisha mema wewe na huyo mwanamke utakayemuoa, ila nakuonya kitu kimoja. Nyumba haiendeshwi na watu wa pembeni, ukifanya hivyo kila utakayemuoa atakukimbia.
Ni mimi mzazi mwenzako,
Mama Zawadi.
Barua ile ilikuwa pigo mujarabu moyoni mwangu, ilikuwa sawa na kuupasua moyo wangu kwa kisu butu bila ganzi. Akili yangu haikukubaliana na kutaka kurudia kwa mara ya pili lakini kila nilipotaka kusoma machozi yalizuia nisiyaone maandishi.
MKE WANGU ALISABABISHA NIKAWA MCHAWI
SEHEMU YA 13
Nilinyanyuka na kutembea taratibu hadi chumbani na kurudi sebuleni, kichwa kilikuwa kizito hata cha kufanya sikujua na kuona kazi yote niliyoifanya ilikuwa bure. Niliyarudia maneno aliyowahi kuniambia mke wangu na kuyaandika katika barua niliyokuwa nimeishikilia kuwa maneno ya nje yatavunja nyumba yetu tukiwa tunapenda.
Nilijikuta nikianza kumlaumu Simon kwa kuona yeye ndiye chanzo cha nyumba yangu kuvunjika baada ya kukubali ushauri wake ambao mwanzo niliuona kama umenisaidia kumbe ulikuwa bomu lilikuwa likisubiri kulipuka na matokeo yake kuisambaratisha nyumba yangu.
Nilijiuliza nitafanya nini ili kumrudisha mke wangu mikononi mwangu kabla ya mwisho wa wiki haujafika. Nilijiuliza hiyo ndoa itafungwa kanisa gani na siku gani, Jumamosi au Jumapili? Kwangu ulikuwa mtihani mkubwa kujua mke wangu ataolewa kanisa gani ili nikaweke pingamizi.
Mawazo yalinizidi, nikawa naona kichwa kama kinataka kupasuka. Mara giza zito lilitokea mbele yangu, sikujua kilichoendelea hadi nilipokuja kushtuka na kujikuta hospitali, pembeni yangu alikuwepo rafiki yangu Simon ambaye alikuwa akizungumza na daktari. Nilimsikia akimuuliza:
“Vipi daktari siyo tatizo kubwa?”
“Si kubwa, ni wazi mgonjwa aliwaza sana kufikia hatua mishipa kushindwa kufanya kazi vizuri. Lakini sasa hivi atarudi katika hali ya kawaida ila anatakiwa kupunguza kuwaza sana.”
“Sawa daktari.”
Simon alipogeuka alishtuka kuniona namtazama, hata bila ya kunisemesha nilimuona akigeuka na kumwita daktari:
“Dokta.”
“Unasemaje?”
“Naona mgonjwa ameamka.”
Daktari alikuja kitandani na kunisemesha:
“Pole Kazala.”
“Asante,” nilimjibu kwa sauti ya chini.
“Unaendeleaje?”
“Kichwa kinauma kwa mbali.”
“Punguza kuwaza ndugu yangu, unaki – over load kichwa na kusababisha maumivu makali.”
“Nimekuelewa daktari,” nilimkubalia lakini niliamini bila mke wangu kurudi sitaweza.
“Huna ugonjwa mwingine zaidi ya huo na dawa yake ni kupunguza mawazo na kumeza dawa za maumivu tu.”
Nilidungwa sindano ya maumivu na usingizi tena, nikaambiwa niendelee kupumzika mpaka siku ya pili ili nipate muda wa kulala sana kukifanya kichwa kipunguze mawazo. Nilitoka siku ya pili na kuja kuchukuliwa na Simon ambaye alionesha hakwenda kazini siku ile kwa ajili yangu.
Kabla ya kufika nyumbani tulipitia hotelini na kupata kifungua kinywa kisha tulirudi nyumbani. Tulipofika nyumbani Simon alinieleza nipumzike na yeye kupanga baadhi ya vitu vilivyokuwa shaghalabaghala, baada ya kuweka baadhi ya vitu vizuri alikuja kukaa karibu yangu na kuniita jina langu.
“Kazala,”
“Naam.”
“Tatizo nini?”
“Shemeji yako ataniua,” nilijibu huku akishika kifua kuzuia presha iliyokuwa ikipanda.
“Tatizo nini?”
“Ameamua kunikimbia.”
“Tatizo nini?”
“Hata sijui, yaani dawa uliyonipa mwenzangu imeharibu kila kitu,” nilianza kumlaumu Simon.
“Acha lawama za kijinga, pale hukuwa na mke kama mkeo anakuletea mwanaume ndani na kulala naye kwenye kitanda chako bado unalaumu watu? Huu si uzoba?”
“Kama ningemuacha atakavyo asingenikimbia.”
“Ingekuwa mimi nisingeumia, ningeshukuru.”
“Ushukuru nini Simon?” nilishangaa majibu ya Simon.
“Yule mwanamke kuondoka mwenyewe, hukuwa na mke ndugu yangu. Kama angekuwa mwanamke mwenye staha zake angeandika barua kama hii? Kazala aliyekuroga amekufa, si bure kufanyiwa mambo yote haya bado unamlilia mkeo?”
“Ndugu yangu mazoea mabaya, pamoja na yote bado nampenda sana mke wangu.”
“Unampenda? Haya huyo kakukimbia kazi kwako.”
“Utanisaidia vipi?” pamoja na kumnanga mke wangu bado nilimuomba ushauri wa kumrudisha mke wangu.
“Kazala tumekuja kutafuta maisha si wanawake, ujinga wako huo utasababisha ufukuzwe kazi. Hakuna mwajiri atakuvumilia na matatizo yako ya kifamilia yasiyoisha. Kumbuka wazazi wako wanakutegemea matokeo yake unaacha kilichotuleta huku unakuwa bwana penda penda.”
“Nitajitahidi lakini itanichukua muda kumsahau, nilimpenda sana mke wangu.”
Nilikubaliana na Simon niachane na mke wangu kisha nifanye kilichonipeleka kule japo nilijua kwa upande wangu kilikuwa kitu kigumu kumuondoa mke wangu moyoni mara moja. Nilipanga kwa siri Jumamosi na Jumapili nizunguke makanisa yote kwa pikipiki ili nijue ni kanisa lipi mke wangu anafunga ndoa ili niweke pingamizi. Kwa vile mke wangu alikuwa Mkatoliki niliamini lazima ningejua anafunga ndoa kanisa gani.
***
Siku ya Jumamosi ilipofika, nilikodi pikipiki kwa ajili ya kuzunguka makanisa yote ya mjini. Kanisa kubwa lilikuwa katikati ya mji pia madogo yalikuwa pembeni kidogo na mji hayakupungua manne. Niliamini hata kama ningezunguka kutwa nzima nitaweza kufika toka kanisa moja kwenda lingine kwa wakati bila kuchelewa.
Dereva wa pikipiki aliniuliza swali baada ya kuzunguka zaidi ya mara mbili makanisa yote ambayo hayakuonesha dalili zozote za kufungwa ndoa.
“Sikiliza ndugu yangu, tutamaliza mafuta bure, kwa nini tusiende kwenye ofisi za kanisa ili tujue kuna ndoa au hakuna na kama ipo itafungwa saa ngapi? Hiyo itatusaidia kuja kwa wakati kuliko kuzunguka na kukufanya upoteze fedha nyingi.”
Wazo lile nilikubaliana nalo na kuamua kwenda kwenye ofisi za kanisa kuulizia kama kuna ndoa ilikuwa ikifungwa siku ile. Makanisa yote manne yalinieleza kuwa siku ile hakukuwa na ndoa yoyote ila Jumapili kulikuwa na ndoa nne ambazo zote zingefungwa kwenye kanisa kuu tu.
Niliamini katika ndoa zile nne lazima moja itakuwa ya mke wangu kipenzi Suzana, mama Zawadi. Nilimshukuru dereva wa pikipiki ambaye kwa sasa angeitwa bodaboda. Nilikubaliana naye kunifuata nyumbani siku inayofuata na kunipeleka kanisani ili nikaweke pingamizi ndoa ya mke wangu.
Baada ya kurudi nyumbani nilikuwa na mawazo mengi kuhusiana na hiyo kesho na kujiuliza nitakapotoa pingamizi litakubaliwa au ndiyo nitaabika hasa kutokana na ndoa yetu kufungiwa Bomani. Upande mwingine niliamini nitakuwa na nguvu ya kuvunja ndoa ya mke wangu kwa vile ilikuwa ikitambuilika kiserikali na vyeti nilikuwa navyo.
MKE WANGU ALISABABISHA NIKAWA MCHAWI
SEHEMU YA 13
Nilipanga kesho nikienda kuweka pingamizi niende na vyeti vya ndoa ili kutia uzito pale mke wangu atakaponikana. Siri ile sikutaka kumshirikisha Simon kwa kuhofia kunipa ushauri mbaya ambao ungeharibu mipango yangu yote. Ushauri wa Simon mwanzo niliuamini lakini baada ya ushauri wake kusababisha mke wangu kukimbia, sikumuamini tena na kuona ndiye chanzo cha matatizo yangu.
Siku ya pili, baada ya kufuatwa na dereva wa pikipiki niliwasili kanisani saa tatu asubuhi japokuwa ndoa ilikuwa ikifungwa saa saba mchana. Nilikaa pale mpaka saa nne na nusu ndipo magari ya maharusi na ndugu na jamaa walipoanza kuingia. Muda mfupi kanisani pakawa na watu wengi na magari kutokana na harusi nne kufungwa, nilisubiri kwa hamu nimuone mke wangu akitaka kufunga ndoa na kuweka pingamizi.
Nami nilikuwa mmoja wa watu niliowahi ndani viti vya mbele kanisani kusubiri ibada ya ndoa. Kanisa lilijaa watu wengi sana pamoja na maharusi wote. Kwa vile mabibi harusi walikuwa wameziba nyuso zao, iliniwia vigumu kumtambua mke wangu ni nani kati ya wale wanne.
Baada ya taratibu zote kufanyika ndoa zilianza kufungwa moja moja huku nikisubiri kwa hamu kuiona sura ya mke wangu. Ajabu ndoa zote zilifungwa bila kuiona sura ya mke wangu. Nilijikuta napagawa na kujiuliza nilielezwa ndoa nne au tano?
Baada ya ndoa zote kufungwa bila kushuhudia sura ya mke wangu, watu wote walitoka kanisani na kubakia peke yangu. Nilijiuliza mke wangu atakuwa amekwenda kufunga ndoa wapi. Nikiwa nado nimesimama kama sanamu nikiwa bado na matumaini huenda kuna ndoa nyingine ingekuja kufungwa, nilishtuliwa na mhudumu wa kanisa.
“Ndugu vipi mbona huondoki na wenzako?”
“Samahani kaka kuna ndoa nyingine zaidi ya hizi?”
“Hakuna, leo kulikuwa na ndoa nne tu hakuna zaidi ya hizi.”
“Mmh! Sijui watakuwa wamekwenda kufunga ndoa wapi?” nilijikuta nikizungumza peke yangu kwa sauti.
“Kina nani?” mhudumu wa kanisa aliniuliza.
“Ooh! Samahani,” nilijikuta nikijibu na kuondoka bila kuaga mpaka nje ya kanisa.
Nje ya kanisa watu walikuwa ndiyo wanamalizikia kuondoka, nilijikuta nimerudi nyumbani kwa miguu na kumsahau dereva wa pikipiki aliyenipeleka. Kwa kweli nilikuwa nimechanganyikiwa na kuamini kama maneno aliyonieleza mke wangu yana ukweli basi atakuwa amefunga ndoa siku ile.
Usiku ulikuwa mrefu kwangu, usingizi ulinikimbia kabisa. Mawazo yote yalikuwa kwa mke wangu na kuona kama kweli ameolewa basi atakuwa amenifanyia ukatili mkubwa sana. Siku ya pili ilikuwa Jumatatu, sikuweza kwenda kazini, nilikuwa kama mtu niliyefiwa, hata chakula kilinishinda.
Jioni Simon alikuja kunitazama na mmoja wa wafanyakazi wenzangu na kunikuta nimejilaza sebuleni mikono kichwani huku pembeni ya macho yangu yakiweka michirizi na kulowesha kwenye mito ya kochi. Simon alinishangaa sana na kuniuliza:
“Kazala una matatizo gani?”
“Simon wewe si wakuniuliza swali kama hilo, unajua vizuri matatizo yangu,” nilimjibu bila kumuangalia.
“Kazala umetoka nyumbani kufuata mapenzi au kazi?”
“Nimefuata kazi.”
“Unaacha kwenda kazini kwa ajili ya mwanamke, nilikueleza toka zamani kuwa huyu mwanamke si chaguo sahihi kwako, lakini ukaona labda nakuchokonoa majibu sasa umeyaona.”
“Simon usiseme hivyo wewe ndiyo sababu ya mke wangu kunikimbia.”
“Mimi?” Kauli yangu ilimshtua Simon.
“Ndiyo.”
“Mimi nimefanya nini?” alionesha kushangaa.
“Ushauri wako ndiyo sababu ya mke wangu kukimbia.”
“Kweli aliyekuroga amekufa, kitendo cha kumfumania mkeo ni mimi? Si ulitaka kufa kwa mawazo nimekusaidia bado huoni msaada wangu?”
“Msaada gani wakati mke wangu kanikimbia.”
“Mkeo yule sawa na kuku aliyelala nje, si kuku tena ni kwale.”
“Lakini umeona lawama zote zinatokana na ninyi watu wa pembeni kuingilia ndoa yangu.”
“Hao watu wa pembeni unaowalaumu ndiyo waliomponya mwanao aliyekuwa fundi majiko.”
“Pamoja na hayo, lakini ninyi ndiyo chanzo cha mke wangu kukimbia.”
“Kwani shemeji kaenda wapi?” Shedu, mfanyakazi mwenzangu aliyeongozana na Simon aliniuliza.
“Hata najua yule mwanamke kaamua kuniua ningali hai,” nilizungumza kwa sauti ya kukata tamaa.
“Kazala wanawake wamekwisha mpaka uchanganyikiwe kiasi hiki?” Shedu aliniuliza.
“Kwani huyo aliyemchukua mke wangu hakuona wanawake wengine mpaka kamchukua mke wangu? Kibaya zaidi jana kamuoa kabisa.”
“Utani huo! Atamuoaje mke wa mtu?” Shedu alishtuka.
“Mpaka kamtoa kwangu atashindwa vipi kumuoa kabisa?”
“Kwa hiyo Kazala bado unampenda mkeo?” Shedu aliniuliza akinikazia macho.
“Tena sana.”
“Na akirudi utakuwa tayari kumsamehe?”
“Ndiyo, najua si akili yake ni ushawishi wa watu wenye fedha wanaoona maskini kama sisi hatuna haki ya kuwa na wanawake wazuri.”
“Mtu mwenyewe unamjua?”
“Kwa sura namjua ila sijui anakaa wapi?”
“Upo tayari kumeza mfupa?”
“Una maana gani?”
“Najua huna uwezo wa kushindana na yule bwana kwa nguvu na fedha, lakini lipo kimbilio la wanyonge nakwambia mkeo atarudi mwenyewe.”
“Kimbilio la wanyonge! Kimbilio gani?” nilishtuka kusikia vile na kutaka kulijua hilo kimbilio la wanyonge.
“Kwa babu.”
“Kwa babu una maana gani?”
“Kwa mganga wa kienyeji.”
“Kweli ataweza?” nilimuuliza kutaka uhakika.
“Bwana wee tena hawa wanaopenda wake za watu kazi yake ndogo sana, nakwambia ndani ya siku mbili mkeo atarudi, ikivuka haifiki wiki.”
“Kweli?”
“Kweli kabisa, unajua taarifa zako nimezisikia toka kwa swahiba wangu hapa, roho iliniuma na kuona umefanyiwa ukatili, kibaya nasikia jamaa ana mke yaani asiridhike na mkewe aje amchukue wako? Tena nitakupeleka mguu kwa mguu hadi kwa mzee wangu, nakuapia mkeo atarudi,” Shedu alinihakikishia kunirejeshea furaha.
“Kama kamuoa?” niliuliza swali ambalo kwangu lilikuwa tata.
“Nimekueleza mkeo atarudi, si mkeo wa ndoa?”
“Ndiyo.”
“Basi atarudi huyo, tukifika kwa babu kazi imekwisha.”
“Gharama zake?”
“Si kubwa sana, utamudu tu.”
“Huyo babu yupo wapi?”
“Tanga katika Wilaya ya Lushoto Kijiji cha Mlalo kisha unaingia ndani zaidi kuna sehemu inaitwa Tewe, hapo temea mate chini kuna kufuru za ajabu, watu wanaweza hata kumfufua maiti akatembea.”
“Nauli yake si kubwa?”
“Ya kawaida utaimudu.”
“Mmh! Nipo tayari hata kesho.”
“Itabidi muombe ruhusa ya siku mbili ili mwende na kurudi,” Simon aliyekuwa kimya muda wote alichangia.
“Lakini Shedu usemacho ni kweli?” pamoja na Simon kuchangia bado sikumuamini Shedu.
“Kwa nini tuandikie mate na wino upo? We twende halafu uniulize swali hilo baada ya kutoka kwa babu.”
Tulikubaliana kesho nikaombe ruhusa kazini ili twende Mkoa wa Tanga kwa mtaalam.
MKE WANGU ALISABABISHA NIKAWA MCHAWI
SEHEMU YA 13
Siku ya pili nilikwenda kazini kuomba ruhusa. Bosi alinikubalia bila kuniuliza swali lolote. Kwa muda mfupi nilikuwa nimekonda kwa mawazo, usiombe kumpenda mtu asiyejua thamani ya upendo wako kwake. Sikutaka kuomba mkopo kwa vile zilikuwa tarehe za mshahara, wafanyakazi wengi mifuko ilikuwa imenona.
Kwa vile muda ulikuwa bado, baada ya ruhusa tuliondoka siku ileile saa tano na kufika Chalinze saa kumi na mbili jioni. Mwenyeji wangu alinieleza itatubidi tulale pale ili tuondoke siku ya pili kutokana na umbali wa kufika Lushoto. Tulilala Chalinze na kusubiri mpaka siku ya pili tupande basi linalotoka Dar es salaam kwenda Lishoto.
Siku ya pili tulipanda basi lililotoka Dar na kufika Lushoto kwenye Kijiji cha Mlalo saa kumi jioni. Hatukukaa, tulichukua usafiri mwingine wa baiskeli kuingia vijiji vya ndani zaidi mpaka katika Kijiji cha Tewe kilichokuwa kinasifika kwa kuwa na waganga wenye uwezo wa juu.
Tulifika Tewe majira ya saa kumi na moja jioni na kwenda kwa mtaalamu mzee Kidereko. Tulifika katika nyumba moja kubwa kiasi ya matofali na bati iliyokuwa imezungukwa na uzio wa miti ya minyaa. Ndani kulikuwa na nyumba nyingine ndogo nne za miti na udongo na juu zilikuwa zimeezekwa kwa makuti ya mnazi. Tulikaribishwa na wenyeji wetu ambao walimfahamu sana Shedu na kuonesha mwenzangu ni mwenyeji sana pale.
“Jamani Shedu karibu,” dada mmoja aliyekuwa amejifunga kitenge kilichopauka alimchangamkia Shedu na kuonesha jinsi gani Shedu alivyokuwa mwenyeji pale kijijini.
“Asante Mwana, za hapa?”
“Nzuri ka Shedu, karibu mgeni,” nilikaribishwa na mimi huku nikipokewa mzigo wangu.
“Asante.”
Tulipelekwa hadi chini ya mti wa mwembe kulikokuwa na jamvi lililokuwa limechoka na pembeni yake kulikuwa na vigoda.
“Jamani karibuni.”
“Asante, za hapa?” Shedu aliuliza.
“Mmh! Kama unavyoziona, maisha magumu.”
“Mwana magumu wakati unatakata?”
“Inatubidi tuyazoee maisha ya huku kwa lazima, kwa vile hatuna jinsi nina imani nimekuona kidogo nitacheka.”
“Ondoa hofu, mzee yupo wapi?”
Amekwenda porini kuna kazi ya mtu amekwenda kumfanyia, nina imani muda wowote atarejea.”
“Ameondoka saa ngapi?”
“Toka saa tisa usiku.”
“Mmh! Inaonekana ni nzito.”
“Na kweli, kuna mtu alilazwa chini na wabaya wake akaletwa hajitambui na kutibiwa na mzee baada ya kupona aliruhusiwa. Miezi minne baadaye alipigwa kombora lingine lililomkata kauli mpaka watu wakajua amekufa. Taarifa zilipomfikia mzee alikwenda mjini na kumnyanyua kisha alimweleza aje huku amtengeneze vizuri. Alifika jana jioni kama ninyi na kulala hapa usiku ndipo walipoamka na kuelekea porini ambako atamfanyia kinga ambayo itamlinda mtu atakayemgusa ataondoka yeye.”
Nilijikuta nikivutwa na mazungumzo ya Shedu na yule msichana anayeitwa Mwana.
“Namuamini mzee, lazima mtu alale chini.”
“Tena amekasirika sana kitendo cha kupimwa nguvu na mtu.”
“Kidereko tena.”
“Mmh, na ninyi?”
“Ndugu yangu ana shida ndogo.”
“Shedu, shida ndogo ndiyo mpande basi kuja huku, si nasikia mjini kuna wataalam ambao hawana uwezo mkubwa, wakishindwa ndipo mnakuja huku?”
“Mwana kazi zangu zote huzifanya mzee Kidereko kwa hiyo hata rafiki yangu alipopatwa na tatizo sikutaka asumbuke wa waganga uchwara nikaona nimlete kwa mzee.”
“Mmh! Sawa, tena huyo anaingia.”
Kauli ya yule msichana ilifanya wote tugeuke kuangalia kwenye mlango wa uzio na kumuona mzee mmoja aliyekuwa akitembea kwa kujivuta na mkongojo mkononi akiwa na vijana wawili waliokuwa wamebeba kapu na majani mabichi mkononi.
Shedu alinyanyuka na kwenda kumpokea mzee Kidereko.
“Babuuu.”
“Babuuuu.”
Walikumbatiana na kuja nilipokuwa nimekaa, nami nilinyanyuka kumpokea mzee Kidereko.
“Shikamoo babu.”
“Marhahaba karibu.”
“Asante babu.”
Walipokelewa kikapu na majani waliyotoka nayo porini na kupumzika kwenye mkeka. Wote walipumzika kwa kujilaza kuonesha wamechoka sana. Kutokana na kuchoka sana vijana wale baada ya kujilaza usingizi mzito uliwachukua na kuanza kukoroma. Lakini mzee Kidereko alinyanyuka na kuelekea ndani kwake na kutuacha tukiwa tumekaa kwenye vigoda. Muda nao ulikuwa unazidi kuyoyoma, kigiza kilianza kuimeza nuru ya mchana.
“Mzee huyu kiboko,” Shedu alinieleza kwa sauti ya chini.
“Kweli anatisha kwa maelezo mafupi inaonesha anaijua sana fani ya ‘mizizioloji’.”
Saa moja kasoro kililetwa chakula, wali na bata ambacho tulikuwa wote, baada ya chakula ndipo mzee Kidereko alipotuita pembeni kwa mazungumzo.
“Jamani karibuni, sikuweza kuzungumza na ninyi nilipofika tulikuwa hoi sana kama mlivyowaona wenzenu.”
“Ni kweli babu,” Shedu alijibu.
“Mmh! Shedu za siku?”
“Nzuri babu.”
“Mambo yako yanakwendaje?”
“Yanakwenda vizuri.”
“Kazini?”
”Panakwenda vizuri yale mambo yalienda kama ulivyoniahidi.”
“Kwa hiyo asante yangu umeniletea?”
“Ndiyo, tena nimeshukuru jamaa yangu kukubali kuja huku nilete na asante yako.”
“Na mkeo katulia?”
“Kila mtu anashangaa, hata ndugu walioanza kuiandama ndoa yangu wametulia.”
Kauli ile ilinishtua na kujiuliza ndoa ya Shedu ilikuwa na tatizo gani lililopata msaada wa babu? Lakini nilitulia kimya na kupanga kumuuliza tukiwa wawili japo nilianza kuhisi huenda kilichompata ndicho kilichonifikisha pale.
“Mmhu, mwenzio ana tatizo gani?” mzee Kidereko aliuliza.
“Kama langu, lakini la kwake limezidi, mkewe kamkimbia kabisa na inasemekana ameolewa kabisa na mtu aliyemchukua.”
“Mmh! Mjini mbona tabia za kuchukuliana wanawake zimeshamiri, wanadamu bwana! Wanawake wapo wengi lakini wanapenda wake za watu. Tatizo si kubwa kama mngekuja mapema mngeweza kugeuza leo hii. Nitaifanya sasa hivi ili kesho alfajiri muwahi kurudi kwenu.”
“Nitashukuru mzee wangu, kweli mke wangu atarudi?” Nilijikuta nikiuliza.
“Hiyo kazi niachie mimi maadamu umeileta kwangu.”
“Nitashukuru mzee wangu.”
“Unataka aliyemchukua mkeo tumfanyeje?”
“Vyoyote ukakavyoona mzee wangu.”
“Tumuue?”
“Hapana.”
”Tumtie uchizi?”
“Mmh! Hakuna adhabu nyingine?”
“Zipo nyingi utakayotaka mwenyewe.”
“Yeyote ya kawaida la muhimu nimpate mke wangu.”
“Kazala lazima tumtie adabu, mzee mfanyie kama yangu.”
Nilishtuka na kujiuliza kama yake ipo vipi? Ilibidi niulize.
“Ulimpa adhabu gani?”
“Nilimpoteza kwenye sura ya dunia,” Shedu alijibu kwa kujiamini.
“Ha! Unamaanisha ulimuua?”
“Ndiyo! Kanitesa sana yule mshenzi kasababisha mwanangu wa kwanza afe baada ya mke wangu kumuacha na kwenda kwa huyo mwanaume na kusababisha mwanangu afe kwenye beseni la maji.”
“Mungu wangu!” nilishtuka na kushika mdomo.
“Kibaya mtu yule hakuishia hapo, alimchanganya mke wangu kiasi cha kudai talaka. Nilimfuata na kumueleza aachane na mke wangu majibu aliyonijibu yalikuwa ya udhalilishaji. Eti aliniambia kama namuona mke wangu anafaidi kuwa naye na mimi niwe mpenzi wake.”
“Uwe mpenzi wake alimaanisha nini?”
“Eti niwe mkewe.”
“Mungu wangu!” kauli ile ilinishtua sana.
“Kazala wee acha tu, mtu akiwa na fedha ana dharau ndiyo maana jambo lako nililichukua kama langu. Kazala nimeteseka mpaka nilipoletwa huku kwa mzee Kidereko.”
“Ina maana ulikuwa humjui tokea awali?”
“Matatizo ndiyo yaliyonifanya nifike huku, we si unajua kabila langu?”
“Nilishangaa pale uliponileta huku na kabila lako, nikajua baba ndiye Mnyamwezi na mama mtu wa Tanga.”
“Walaa.”
“Yalikuwa mateso ya muda gani?”
“Miezi nane lakini kwangu ilikuwa miaka mia nane.”
“Pole sana, mhu ikawaje?” nilijikuta nikiwa na shauku baada ya kuona matukio yetu yanafanana sana.
“Baada ya kuletwa huku sikutaka adhabu kali, lakini babu aliniambia mtu huyo nikimchelewesha ataniwahi mimi.”
“Kutokana na mateso niliyoyapata na uchungu wa kifo cha mwanangu nilikubali.”
“mmh! Ikawaje?”
“Basi mzee akatengeneza mambo, sikuwepo ila waliokuwepo na kutoa ushuhuda walisema baada ya kwenda nyumba ya wageni na mke wangu ambaye yeye alijimilikisha na kuwa mkewe. Kutokana na maneno aliyoyasema mke wangu, aliyekuwepo kwenye tukio wakiwa faragha.
“Baada ya kumaliza mchezo wao uume haukupoa, uliendelea kusimama kama chuma na kumsababishia maumivu makali sana.
Alipopiga kelele za maumivu ilibidi achukuliwe na kupelekwa hospitali, huko alipigwa sindano za ganzi ili uume upoe lakini wapi, kila dakika maumivu yalikuwa makali, alilia mpaka sauti ikakauka. Nasikia alinitaja mimi ili niende akaniombe msamaha.
“Nguvu zilimwisha mateso yale yaliendelea kwa saa nane, jioni uume ulinywea na yeye kufariki dunia.”
“Mmh! Aliteseka sana.”
“Yeye kwa saa nane mimi miezi minane, kuchanganyikiwa kubaya nakumbuka kuna kipindi nilikuwa natembea nikizungumza peke yangu. Kingine hali yangu ya kimaisha ilikuwa mbaya hapo ndipo nilipozidi kuumia.”
“Baada ya hapo nini kiliendelea?” nilijikuta nikivutwa na simulizi ya Shedu.
“Mke wangu alirudi huku mtaani kila mmoja akiniheshimu mpaka leo hakuna mtu wa kumgusa mke wangu. Hata akija mgeni lazima atapewa taarifa za yule jamaa aliyejitia kidume na kulamba udongo. Basi akipata taarifa ile humkalia mbali mke wangu.”
“Lakini mbona kama adhabu ni kubwa sana.”
“Kazala acha huruma, wanadamu si wa kuwachekea ona anavyoteseka kwa haki yako.”
“Sawa lakini kuua!” bado niliona adhabu ya kuua ni kubwa.
“Kijana acha ujinga, siku zote akuanzae mmalize,” mzee Kidereko alisema.
“Sawa mzee wangu, mi shida yangu kumrudisha mke wangu tu si kuua.”
“Sawa, ila lolote litakalotokea usirudi hapa.”
“Kwa nini babu?”
“Inaonekana hujihurumii, kwa hiyo naomba ukiondoka hapa usirudi labda uje na lingine. Mimi hupenda kufanya kazi mara moja ili usirudi hapa kwa kazi hiyohiyo. Kwa akili ya mkeo hata kama atarudi bado ataendelea kukusumbua. Nakueleza utarudi hapa nguo zipo kichwani.”
“Kwa nini unasema hivyo?”
“We si mtoto mdogo mambo mangapi kakufanyia mkeo nusra ujiue, kweli uongo?”
“Kweli.”
“Sasa kwa nini mtu aliyetaka kukusababishia ujiue unamuonea huruma? Nataka kukueleza huruma ikizidi hugeuka uchawi wa kukuzuru mwenyewe hasa kwa adui yako.”
Nilitulia kwa muda nikiwaza na kuwazua juu ya adhabu wanayotaka kuifanya kwa mwanaume aliyemchukua mke wangu. Kauli za kurudi nguo nimeweka kichwani zilinitisha sana na kujua kurudi pale nitakuwa mwendawazimu.
Niliwa nimezama kwenye dimbwi la mawazo mzee Kidereko alinishtua:
“Sasa amua tufanye kazi kamili au nusu?”
“Mzee Kidereko fanya kazi kamili,” Shedu alisema.
“Shedu usimsemee mwenzako mwache aseme mwenyewe.”
“Mzee Kidereko usimsikilize huyu jamaa, sisi ndiyo tunajua anavyoteseka, tena kurudi na nguo kichwani umemhurumia atabakia jina. Juzi tu amechungulia kaburi.”
“Hata kama yote hayo yamemtokea bado ana hiyari ya kuepukana na tatizo hilo au kuendelea kuteseka.”
“Mzee tumetoka mbali shida yetu ni kulimaliza tatizo hilo hasa tukizingatia sasa hivi kaolewa kabisa,” Shedu alizidi kushadadia.
“Bado mwenye uamuzi wa mwisho ni yeye mwenyewe.”
Ubishani ule ulinifanya nikumbuke mateso mazito aliyonipa mke wangu na dharau ya yule mwanaume, kwanza kumfanya mwanangu achelewe kutembea, pili kulala na mke wangu katika chumba na kitanda changu. Ile ilikuwa ni dharau kubwa sana na mbaya zaidi kumchukua jumla na kumuoa, japo sikuwa na uhakika nalo lakini ile ilikuwa kauli ya mke wangu kwenye barua yake aliyoniandikia siku alipoamua kuondoka.
Moyo uliniuma mpaka machozi yalinitoka na mishipa ya kichwa kusimama. Nilinyanyua sura kuwaangalia wote waliokuwa kimya wakisubiri jibu langu. Moyoni sauti iliingia ikiniambia mtu yule hastahili huruma hata kidogo.
“Babu maliza kazi,” nilijikuta nikitamka kwa sauti.
“Kwa moyo wako au kwa kulazimishwa?”
“Kwa moyo wangu.”
“Kweli?”
“Kweli kabisa.”
“Kazala huo ndiyo uanaume,” Shedu aliuunga mkono uamuzi wangu.
“Basi ngoja tuifanye hii kazi ile kesho muwahi kuondoka.”
“Sawa.”
Tulikwenda kwenye kibanda kimoja ambacho ndicho alikuwa akifanyia kazi zake.
MKE WANGU ALISABABISHA NIKAWA MCHAWI
SEHEMU YA 15
Kilikuwa na vitendea kazi vyake, baada ya kukaa kwenye mkeka aliagiza beseni dogo la maji, baada ya muda lililetwa. Baada ya kuletewa aliweka maji na kuniuliza:
“Huyo bwana unamjua jina?”
“Simjui.”
“Nipe jina la mkeo.”
“Anaitwa Suzana.”
“Jina la mama yake?”
“Maria.”
Baada ya kumpa majina yale alichukua dawa ya unga huku akilitaja jina la mke wangu kwa sauti ya chini, aliunyunyizia ule unga kwenye maji yale. Baada ya muda aliniita na kuniuliza:
“Huyu si mkeo?”
“Ha! Ndiye,” nilishtuka kumuona mke wangu ndani ya beseni lile ikiwa kama natazama video.
“Ni kweli ni yeye?” mganga aliniuliza tena.
“Ndiyo mzee wangu.”
“Na huyo aliyekaa pembeni yake unamjua?”
Nilituliza macho yangu kumuangalia yule mwanaume aliyekuwa amekaa na mke wangu, akiwa kifua wazi na kugundua ndiyo yule mwanaume niliyemuona kitandani na mke wangu.
“Huyu ndiye aliyemchukua mke wangu,” nilisema kwa sauti, macho yakiwa yamenitoka pima.
“Kweli ni yeye?” aliniuliza tena mzee Kidereko.
“Ndiye.”
“Sasa tunamtoa mkeo na kumbakisha mwenyewe kisha nitakuelekeza kitu cha kufanya.”
“Hakuna tatizo.”
Baada ya kusema vile alichukua dawa ya unga na kunyunyizia kwenye maji huku akizungumza kwa sauti ya chini sana ambayo sikusikia anazungumza nini huku nikiangalia kwa macho yangu. Mara nilimuona mke wangu akinyanyuka na kuondoka, akabakia yule mwanaume peke yake kwenye kochi.
“Sasa nuiza kifo chochote unachotaka kimpate.”
“Cha ajali.”
“Nuiza.”
Mganga alinipa unga ule niuweke kwenye maji kwa kuunyunyizia, nilifanya vile huku nikinuiza kutaka yule mwanaume afe kifo cha ajali kwa kuamini kifo kile hakiwezi kuwafanya watu waniwazie vibaya. Baada ya kunuiza kimoyomoyo, nilimwambia nimemaliza. Baada ya kusema vile alichukua kisu kikubwa cha kuchinjia mbuzi na kukiweka kwenye yale maji na kusema:
“Majibu ya kazi yetu tutaangalia asubuhi wakati mnaondoka kama haikukubali itabidi mbaki tufanye tena upya. Lakini kazi zangu ninazowahi kufanya katika mia basi mbili tu ziligoma lakini niliporudia zilikubali.”
Baada ya zoezi lile mganga alichukua beseni la maji na kutoka nalo nje, baada ya muda alituita nje kumfuata. Tulipotoka katika kilinge cha mganga, tulikwenda kwenye sehemu tuliyopangiwa kulala ili asubuhi tuondoke kurudi Dar. Tulilala kwenye mkeka, tukiwa tumejilaza nilimuuliza Shedu.
“Shedu kazi iliyofanyika hiyohiyo tu au kuna nyingine?”
“Kwa nini?”
“Naona tumefanya ya kumuua yule jamaa, vipi kuhusu mke wangu kurudi?”
“Jamaa akifa tu, mkeo anarudi nyumbani.”
“Itawezekana kweli?”
“Kama ingekuwa haiwezekani angekwambia, yule mzee amekwishaona kila kitu.”
“Mmh! Sawa.”
“Usiwe na wasi tukirudi utakubali na wewe mwenyewe utamletea huyu mzee zawadi.”
“Haya.”
Tulilala mpaka alfajiri tulipoamshwa na mzee Kidereko, tulipoamka alitueleza kuwa ngoma imekuwa nzito.
“Vijana ngoma imebuma.”
“Kivipi?”
“Muziki mnene,” alisema huku akituonesha beseni lililokuwa na maji na kisu, lilikuwa kama jana lilivyowekwa.
“Mbona hatuelewi?”
“Jamaa kajitengeneza sana.”
“Umejuaje?”
“Kama ingekubali tungekuta maji haya yamegeuka na kuwa damu.”
“Unafikiri ni kwa nini?
“Jamaa anaonekana yupo sawa.”
“Kwa hiyo?”
“Kuna kazi ya ziada inatakiwa kufanyika, tuliyofanya ilikuwa ya kawaida sana.”
“Sasa itakuwaje?”
“Safari imekufa, tutarudia tena leo jioni.”
Kauli ile ilinitisha na kuiona kama vita yangu na mwanaume aliyemchukua mke wangu ni kubwa sana tofauti na matumaini niliyopewa.
Hatukuwa na jinsi, tulikubali kushinda pale kijijini mpaka jioni tulipongia kwenye kazi nyingine. Safari ile alichemsha maji kwenye chungu, yalipokuwa yakichemka aliweka dawa na kunieleza nishike kisu na kukiingiza ndani ya yale maji yaliyokuwa yakichemka.
Japo ndani ya chungu hakukuwa na kitu kingine lakini kila nilipoingiza kisu kiligoma.
“Vipi mbona huingizi kisu?” mzee Kidereko aliniuliza.
“Kimegoma, inaonesha kuna kitu ndani ya chungu,” nilimweleza mganga baada ya kisu kugoma kuingia.
“Hebu toa kisu,” aliniamuru kukitoa kisu.
Nilitoa kisu, mganga alichukua dawa ya unga na kuiweka kwenye yale maji yaliyokuwa yakichemka kisha aliweka maji yaliyokuwa kwenye chupa ndogo na kunieleza nikiingize tena kisu.
Kisu kiliingia kama kinaingia sehemu iliyokuwa ngumu, ghafla maji kwenye chungu yalibadilika na kuwa damu.
“Endelea kukiingiza kisu kwa nguvu,” mganga alinieleza nitumie nguvu.
Kila nilivyojitahidi kukiingiza ilifika sehemu kikagoma kabisa kwenda mbele wala kutoka nje.
“Chomoa kwanza.”
Nilipochomoa kiligoma kutoka.
“Kimegoma.”
“Hebu,” ilibidi akitoe mwenyewe ndani ya maji ambayo yalikwishaanza kutoa harufu ya damu mbichi. Baada ya kukitoa kisu maji yalirudi katika hali ya kawaida. Hali ile ilimshtua mganga na kumsikia akishusha pumzi nzito na kusema:
“Mmh! Hapa kazi ipo.”
Nilimuona akikuna kichwa na kukitazama chungu ambacho ghafla kiliacha kuchemka japo moto ulikuwa bado unawaka. Nilijikuta nikichanganyikiwa, hata Shedu naye alionekana kushtushwa na tukio lile ambalo bado sikuelewa tatizo lipo wapi.
Share
0 Maoni